Idara ya Uhamiaji imewatia mbaroni wahamiaji kadhaa na baadhi yao kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kutimuliwa nchini na kufungwa jela.
Idara hiyo kupitia operesheni maalum iliwakamata wageni 7,423 kwa kuingia nchini kinyume cha sheria.
Naibu kamishna wa uhamiaji Abbas Irovya aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kukemea tabia ambayo imekithiri miongoni mwa watu katika jamii kupokea wageni kisha kuwapa hifadhi pasipo kufuata taratibu kisheria kitu ambacho ni hatari kiusalama.
Aidha, alisema kupitia operesheni walioifanya katika kipindi cha mwaka 2014 kuelekea 2015 waliwakamata wahamiaji na kuwachukulia hatua ambapo waliokutwa na makosa na kuhukumiwa vifungo tofauti jela ilikuwa ni 328 huku idadi ya waliofukuzwa ikiwa ni 2,873, waliotozwa faini 224 na walioachiwa 596.
"Katika kuhakikisha tunapambana na kudhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu nchini, Idara ya Uhamiaji imefungua vituo 47 katika mipaka ili kurahisisha zoezi la kuwatambua na kuwakamata wahamiaji haramu waingiao nchini ambapo wengi wao wakiwa ni wakimbizi kutoka nchi jirani ambazo zimewahi kukumbwa na vita," alisema Irovya.
Aidha, aliongeza kuwa mwaka 2014 kuelekea 2015 idara ya Uhamiaji imetoa uraia kwa wahamiaji 187 idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na ile ya mwaka jana ambapo wahamiaji waliopewa uraia walikuwa 98.
"Pamoja na kuratibu shughuli za utoaji wa uraia kwa wahamiaji hao pia idara hii imekuwa ikiratibu na kufuatilia kwa umakini Watanzania wachukuao uraia katika nchi zingine pamoja na wale waishio nchi za nje kwa shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano pindi yatokeapo matatizo," alisema.