Mratibu wa Uhurumarathon Tanzania Innocent Melleck akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam juu ya kukamilika kwa maandalizi yam bio hizo zinazotarajiwa kufanyika jumapili hii jijini Dar Es Salaam katika viwanja vya Leders Club kushoto ni katibu mkuu wa shirikisho la Riadha la Taifa Selemani Nyambui.
MAANDALIZI ya mbio za Uhuru, Uhuru Marathon, zinazotarajiwa kufanyika Desemba 7 (jumapili) jijini Dar es Salaam yamekamilika, huku wanaridha kadhaa kutoka ndani na nje ya nchi wakithibitisha kushiriki mbio hizo zenye lengo la kuulinda uhuru wetu, kudumisha umoja, amani, upendo na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema, maandalizi yote yamekamilika, huku wanariadha wa hapa nchini kutoka nje ya Dar es Salaam wakiwa wamewasili tayari kwa ushiriki wao.
Melleck pia alisema, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ulinzi umeimarishwa kwa kiwango kikubwa ili kuhakikisha usalama unakuwa mkubwa kwa washiriki wote na barabara zitakazotumika zitafungwa katika kipindi hicho.
"Kila kitu kimekamilika na washiriki kutoka nje ya Dar es Salaam wameanza kuwasili kwa ajili ya mbio hizo na tunawahakikishia usalama utakuwa mkubwa mno katika kipindi chote cha mbio hizo n mpaka kufikia jana (juzi) tayari washiriki waliojitokeza walikuwa 4000," alisema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Tanzania (RT), Selemani Nyambui alisema, wanariadha maarufu wa hapa nchini watakaoshiriki ni pamoja na Fabian Joseph na Dickson Marwa, huku Jacqueline Sekini aliyeshinda mbio hizo kwa upande wa wanawake mwaka jana, naye akiapa kutetea ubingwa wake.
"Wapo wanariadha wengi watakaoshiriki, lakini nataka kutoa angalizo kwa wanariadha kutoka Kenya, sisi tumetumwa mwaliko kwa wa chama husika na wao ndio watutumia majina ya wanariadha kumi, watano wa kiume na waliobaki wa kike, hatutapokea mwanariadha kutoka nchi hiyo ambaye hatujapewa jina lake," alisema.
Nyambui alisema, tayari waamuzi watakaosimamia mbio hizo wapo tayari na akasisitiza ni lazima taratatibu zote zitafuatwa ili kupata mshindi halali.
Mbio hizo zinatarajiwa kuanzia viwanja vya Leaders Club na zitakuwa za kilomita 21, kilomita 5 na kilomita 3 ambazo ni maalumu kwa ajili ya viongozi wa kitaifa, dini na taasisi mbalimbali.
Aidha Melleck alisema, tayari namba kwa washiriki zimeanza kutolewa na wanaweza kuzipata katika viwanja vya Leaders Club.
Mgeni rasmi katika mbio hizo anatarajiwa kuwa Rais Jakaya Kikwete.