Wednesday, December 10, 2014

TIPER yasaini makubaliano kuchangia vitabu vya masomo ya sayansi Shule ya Sekondari Vijibweni




TIPER yasaini makubaliano kuchangia vitabu vya masomo ya sayansi Shule ya Sekondari Vijibweni
KAMPUNI ya kuhifadhi mafuta ya Tanzania, Tanzania International Petroleum Reserves Limited (TIPER), imesaini makubaliano ya ununuzi wa vitabu  200 vya masomo ya sayansi katika shule ya Sekondari ya Vijibweni iliyopo eneo la Kigamboni, Wilayani Temeke mkonani Dar es Salaam ikiwa ni moja ya mpango wa kampuni hiyo katika kusaidia jamii.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo iliyofanyika shuleni hapo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER hapa  nchini, Daniel Belair alisema hatua hiyo inalenga kuboresha kiwango cha elimu hapa nchini hususani kwenye masomo ya sayansi.

"Ni ukweli ulio wazi kwamba kwa sasa taifa linahitaji zaidi wahitimu wa masomo ya sayansi.Hakuna njia rahisi kufanikisha hilo zaidi ya kuanza kuwaandaa hao wahitimu kuanzia sasa na ndiyo maana na sisi tukaona ni vema tuwe sehemu ya maandalizi hayo,'' alisema Belair.

Katika kuthibitisha adhma yake ya kusaidia vitabu  hivyo, Mkurugenzi huyo alitanguliza jumla ya vitabu 28 vya masomo ya Baioloji, Kemia na Fizikia vyenye thamani ya sh. Milioni 4 huku akiahidi kukabidhi idadi ya vitabu iliyobakia hivi karibuni.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa shule hiyo, Itumbo Kinyonyi licha ya kuishukuru kampuni ya TIPER kwa msaada huo, alisema msaada huo unakuja wakati muafaka ambapo kwa sasa shuke hiyo ipo kwenye mkakati wa kuongeza ufaulu zaidi wa wanafunzi wake hasa kwenye masomo ya sayansi.

"Vitabu hivi vitatusaidia sana hasa katika kufanikisha ufaulu wa masomo ya sayansi.Katika kipindi ambacho tunaboresha mahabara zetu kulingana na agizo la Mh. Rais Kikwete tunabahatika pia kupata na vitabu vya sayansi… ni bahati kiasi gani?!,'' alishukuru Mwalimu Kinyonyi.

Hata hivyo, akizungumza kwenye hafla hiyo, Mwalimu wa taaluma katika shule hiyo, Musa Ungando alisema pamoja na msaada huo shule hiyo bado inakabiliwa na uhaba wa vifaa vya mahabara zikiwemo kemikali na hivyo kutoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo wa TIPER ili kuokoa sekta hiyo muhimu.

"Ni jambo linalotia faraja kuona tatizo la uhaba wa vitabu hasa vya masomo ya sayansi kwa sasa linapata suluhisho…hata hivyo bado tunawaomba wadau wengine waige mfano nao wasaidie kutatua changamoto nyingine zinazoikabili shule ikiwemo vifaa vya mahabara zikiwemo kemikali kwa ajili ya mafunzo ya sayansi,'' alisema Mwalimu Ungando.

Akishukuru kwa niaba ya wanafunzi wenzake, mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule hiyo Ameir Kassim alisema kupatikana kwa vitabu hivyo kutarejesha ari iliyokuwa imeanza kupotea ya wao kusoma masomo ya sayansi.

"Kuja kwa vitabu hivyo kutatuondelea usumbufu tuliokuwa tunaupata wa kubanana wanafunzi wengi kusoma vitabu vichache na wengine  kulazimika kutembea umbali mrefu kwenda shule nyingine kuazima vitabu hivyo kwa wenzetu,'' alisema mwanafunzi huyo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayoifadhi mafuta ya Tanzania, Tanzania International Petroleum Reserves Ltd (TIPER), Bw Daniel Belair, akikabidhi vitabu vya sayansi vikiwemo vya Fizikia, Baolojia na Kemia kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Vijibweni, Bw Itumbo Kinyonyi wakati wa sherehe ya kusaini makubaliano yatakayoiwezesha kampuni hiyo kuchangia vitabu 200 vyenye thamani ya Shilingi milioni nne kwa shule hiyo iliyopo eneo la Kigamboni wilaya ya Temeke. Shughuli hiyo ilifanyika jana katika viwanja vya shule hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayoifadhi mafuta ya Tanzania, Tanzania International Petroleum Reserves Ltd (TIPER), Bw Daniel Belair, na Mkuu wa Shule ya Sekondari Vijibweni, Bw Itumbo Kinyonyi wakionyesha vitabu vya sayansi vikiwemo vya Fizikia, Kemia na Baolojia baada ya kampuni hiyo kusaini makubaliano ya kuafiki kuchangia vitabu 200 vyenye thamani ya Shilingi milioni nne kwa shule hiyo iliyopo eneo la Kigamboni wilaya ya Temeke. Shughuli hiyo ilifanyika jana katika viwanja vya shule hiyo.