TAASISI ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET), imeendelea kumweka juu mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, kwa kutoa matokeo ya utafiti wake yanayodai kuwa mgombea huyo atachaguliwa na asilimia 71.2 ya wapiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31. Katika hali ya kutiliwa shaka, utafiti huo uliwahoji watu 2600 tu wakati nchi ina watu milioni 40 huku waliojiandikisha kupiga kura wakiwa ni milioni 19. Taasisi hiyo, ilisema iliwahoji watu hao kutoka katika wilaya za mijini na vijijini huku wakiwa wameteuliwa kwa sampuli nasibu ‘random sample’ ambayo haijali anayeteuliwa ni nani. Hata hivyo, kigezo hicho cha kuteua wahojiwa ndicho kinachouweka utafiti huo, katika hali ya kutiliwa shaka zaidi kwani uzoefu wa tafiti zinazotumia sampuli hiyo unaonyesha kuwa upo uwezekano kwa watafiti kujikuta wamehoji watu wengi wenye mtazamo mmoja huku nchi ikiwa na watu wengi ambao hawajahojiwa lakini wenye mtazamo tofauti na huo. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti Mwenza wa REDET, Dk Benson Bana, alisema miongoni mwa maswali waliyoulizwa wananchi hao wachache ni: “Mwezi Oktoba mwaka huu utafanyika uchaguzi mkuu. Kama uchaguzi huo ungefanyika leo, ungechagua mgombea wa chama gani?” Alisema wahojiwa walitoa maoni na kusema wangemchagua Kikwete, huku Dk. Willbrod Slaa (CHADEMA) akifuatia kwa asilimia 12.3. “Katika maoni waliyotoa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba aliibuka na asilimia 10.1, huku vyama vingine vikipata idadi ndogo ya wahojiwa wakati asilimia 5.6 walisema bado hawajaamua ni mgombea wa chama gani watampigia kura,” alisema Dk. Bana. Wakati REDET ikitoa matokeo hayo, hali halisi ya mwenendo wa ushindani wa wagombea na vyama vyao, inaonyesha dhahiri kuwa Kikwete anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Dk. Slaa wa CHADEMA kiasi cha kuwa vigumu kubashiri mara moja yupi ataibuka mshindi katika uchaguzi huo. Alisema kwa upande wa nafasi za ubunge asilimia 66.7 ya wahojiwa, walisema wangemchagua mgombea wa CCM, asilimia 11.7 CUF huku asilimia 11.5 wangechagua CHADEMA na vyama vingine vikiambulia idadi ndogo. Dk. Bana aliendelea kueleza kuwa katika nafasi za udiwani asilimia 66 walitoa maoni yao na kusema wangewachagua wagombea wa CCM, asilimia 11.5 CUF na asilimia 10.3 wagombea wa CHADEMA. “Baadhi ya waliohojiwa walisema bado hawajaamua ni chama gani cha kukipigia kura katika uchaguzi wa wabunge ambao ni asilimia 7.8 na madiwani ni 10.4,” alisema. Alisema katika matokeo ya utafiti wa Redet wa mwezi machi mwaka huu, yaliyoonyesha wahojiwa wangechagua mgombea wa urais wa CCM kwa asilimia 77.2 ambapo katika utafiti wa Septemba bado anaongoza. Alisema kati ya sifa moja kubwa ambayo wahojiwa walisema wangempigia kura mgombea fulani, sifa ya uzoefu wa mgombea iliongoza kwa kupata asilimia 14.8. Sifa nyingine zilizofuatia ni anayejali wanyonge au maskini ilitajwa kwa asilimia 14.1, mgombea wa chama changu 12.5, mgombea mwadilifu asiyeshiriki rushwa wala ufisadi 9.9 na mgombea mwenye elimu kubwa asilimia 1.9. “Kikwete anatajwa kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 50 katika kila wilaya 43 zilizofanyiwa utafiti huu, kati ya wilaya 9 anatajwa idadi ya asilimia 50 ambazo ni Arusha, Kinondoni, Kigoma Mjini, Kigoma Vijijini, Babati, Mvomero, Ilemela, Micheweni na Mkoani,” alisema. Alisema mgombea wa CHADEMA, anatajwa kuchaguliwa kwa zaidi ya asilimia 50 katika wilaya tatu ambazo ni Kinondoni asilimia 64, Kigoma Vijijini 56, Babati (58), Arusha Mijini (40), Iringa Mjini (20), Bukoba mjini (26), Kigoma mjini (32), Mbulu (36), Serengeti (20), Ileje (34), Mvomero (44) na Ilemela (36). Wadau mbalimbali wa masuala ya kisiasa nchini mara kwa mara wamekuwa wakiitaja REDET kuwa taasisi inayofanya propaganda ya makusudi ya kurubuni wananchi katika masuala ya siasa na uongozi kwa maslahi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), licha ya viongozi wa taasisi hiyo kukanusha. |
source:http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=20025 |