Taarifa za kugundulika kwa mauaji hayo zimekuja wakati ndugu zake wakimsaka baada ya kupotea katika mazingira ya utatanishi.
Oppong alikutwa na mauti hayo mwishoni mwa mwezi uliopita wakati akiwa wilayani Bagamoyo ambako alikwenda huko kuuza magari matano aliyokuwa ameagiza kutoka Japan kupitia Bandari ya Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Absaloom Mwakyoma, alisema watu waliohusika na mauaji hayo ambao aliwataja majina yao, walijifanya kuwa wateja wa magari hayo.
Alisema Septemba 29, mwaka huu majira ya saa 3:00 usiku taarifa zilifika katika kituo cha polisi Bagamoyo ilipokelewa taarifa ya kuuawa kwa raia huyo na kufukiwa msituni na hivyo jitihada za kufatilia zilianza ikiwa ni pamoja na kuyazuia magari ya marehemu kutolewa bandarini.
"Tuliongea na mke wa marehemu aitwaye Victoria Joseph (38) Raia wa Kenya na kwa mujibu wa maelezo yake marehemu mumewe alikuwa ameagiza magari matano kutoka nchini Japan yapitie Bandari ya Dar es Salaam aweze kuyauza na Septemba 9 waliwasiliana kwa simu na mumewe na alimwambia ameitwa na wateja wake Bagamoyo,"alieleza Kamanda Mwakyoma.
Mwakyoma alisema Victoria alieleza kuwa baada ya hapo mawasiliano kati yake na marehemu yakakatika na alijua ni matatizo ya mitandao, lakini siku zilivyozidi kuongezeka bila mawasiliano alipatwa na hofu ndipo akatoa taarifa katika kituo cha polisi cha Oysterbay na Makao Makuu ya polisi.
Kamanda Mwakyoma alisema hapo kazi ya kufanya upelelezi ilianza kwa ushirikiano wa pande mbili ya Kanda maalumu na Pwani na katika kufuatilia waliwakamata watuhumiwa hao ambao walipohojiwa walikiri kuhusika na mauaji hayo na kuonyesha mahali walipomuulia.
Pia watuhumiwa hao walionyesha na gari walilochukulia mwili wa marehemu ambalo ni Toyota na kwenda kuonyesha walikochimbia kaburi na kuuzika bila kufuata taratibu.
Watuhumiwa hao walisema baada ya kumuua Oppong Sept 10 saa moja jioni walichukua mfuko mweusi wenye zipu wakamviringishia kisha kumuweka kwenye buti la gari hilo hadi pori la Mbegani ambapo waliazima majembe na kumfukia takribani mita 30 pembezoni mwa barabara vichakani.
Alisema baada ya maelezo hayo taratibu za kuomba kibali kutoka mahakama ili kuufukua mwili huo zilichukuliwa na zoezi la kuufukua lilifanyika na wataalamu kutoka taasisi zote za kushughulikia uchunguzi wa sababu za kifo kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali na kwingineko.
Alisema baada ya kufukua mwili huo waliukuta ukiwa na jeraha juu ya jicho la kushoto, alikatwa shingo chini ya meno na majeraha matatu ya kutobolewa tumboni na utumbo ukiwa umetoka nje.
Mwakyoma pia alisema walikuta nguo za marehemu zikiwa zimetupwa shimo la choo karibu na duka la mtu mmoja na kwamba mapanga waliyotumia watuhumiwa hao yalisalimishwa kituo cha polisi Bagamoyo huku chumba kilichotumika kwa mauaji hayo kilisafishwa na simu za marehemu zilifichwa kuficha ushaidi
"Walioshiriki kuutambua mwili wa marehemu huyo ni pamoja na mke wa marehemu Victoria Oppong na kaka wa marehemu Andrew Oppong (40) ambaye ni Mghana mwenye uraia wa Marekani ambaye alifikia nchini kufuatilia taarifa za kupotea kwa marehemu huyo," alisema Kamanda huyo.
Mwili wa marehemu huyo ulikabidhiwa kwa ndugu na kuhifadhiwa katika hospitali ya muhimbili wakati wanafanya taratibu za mazishi, na watuhumiwa wamefikishwa kwenye mahakama ya Bagamoyo.
Chanzo : gazeti Mwananchi