Friday, October 08, 2010

Wanaharakati wamshukia Shimbo

Wanaharakati wamshukia Shimbo

na Nasra Abdallah
MASHIRIKA yanayotetea Usawa wa Jinsia, Haki za Binadamu na Maendeleo na Ukombozi wa Wanawake Kimapinduzi (FemAct), yamemjia juu Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo na kumtaka aache mara moja kuingilia mambo ya uchaguzi.
Msimamo huo ulitolewa jana kwenye ofisi za Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), mjini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache tu tangu mnadhimu huyo aliposisitiza umuhimu wa wadau wa uchaguzi kulinda amani na usalama ambazo ni tunu kwa taifa.
Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa FemAct, Bubelwa Kaiza, alisema licha ya tamko hilo kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kuenzi na kulinda amani, hawakubaliani nalo kwa jinsi lilivyotolewa.
Pia uhalali wa wahusika kutoa tamko hilo, kipindi lilipotolewa, mantiki yake, mwelekeo wa maudhui yake na chombo kilichotoa tamko husika.
Alizitaja sababu za kutokubaliana na tamko la vyombo vya ulinzi na usalama kuwa ni pamoja na kukiuka na kwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, Ibara 138 ambapo haibainishi kuwa majeshi ya ulinzi na usalama yatajihusisha moja kwa moja na masuala ya uchaguzi.
Alisema Katiba hiyo haina sehemu inayobainisha Amiri Jeshi Mkuu, yaani Rais, anaweza kutoa amri kwa majeshi ya ulinzi na usalazma kuingilia shughuli za Uchaguzi Mkuu au chaguzi nyinginezo.
Aidha, ibara ya 74 ya Katiba hiyo, haihitaji wala kutambua majeshi ya ulinzi na usalama kama sehemu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hivyo kitendo cha majeshi ya ulinzi kutoa tamko kupitia vyombo vya habari ni dhahiri kinalenga kutoa vitisho, kuchochea, kuingilia mchakato na bila shaka kuvuruga Uchaguzi Mkuu unaokusudiwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.
“Hadi sasa zaidi ya vijembe vya hapa na pale baina ya wanasiasa na vyama vya siasa vinavyoshindana na kujinadi kwa wananchi ili kupata ridhaa ya kuongoza dola ya Tanzania, hakuna wala hakujatokea tishio lolote la kuvuruga amani.
“Vyama vya siasa vimekuwa vikiendelea kutangaza mipango ya sera zao vijijini na mijini kupitia kampeni na wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kuhudhuria mikutano hiyo kusikiliza na kuchambua ahadi mbalimbali zinazotolewa na wanasiasa na vyama vyao, hayo yote yakiwa yanaendelea kwa amani, sisi tunaamini kuwa tamko la vyombo vya ulinzi na usalama lina agenda yake,” alisema mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, alisema kama kweli kungekuwa na tishio la amani na usalama, wangetegemea kuona Jeshi la Polisi, chombo chenye dhamana ya kuhakikisha kunakuwa na hali ya usalama kwa raia na mali zao kinatoa tamko na siyo JWTZ.
Alisema pamoja na kazi zote zilizofanywa na Jeshi la Polisi, mfano kukutana na makundi mbalimbali, kutoa kitabu kinachoelezea wajibu wa raia na polisi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, leo hii kazi hiyo inaonekana si lolote na jeshi kuingilia kati, hali hii haileweki na ni kinyume cha kanuni za msingi za utawala bora.
Kupitia tamko hilo, FemAct, iliwataka wanasiasa kuacha kujitafutia ushindi kwa kutumia mlango wa nyuma, kwani uongozi wa dola sharti upatikane kupitia mashindano ya wazi, kusaka ridhaa ya wananchi kidemokrasia katika uchaguzi unaokubalika kuwa huru na wa haki, siyo kutumia vyombo vya ulinzi na usalama kutisha wapiga kura ili kujihakikishia ushindi.
FemAct pia imependekeza vyombo vya habari, kuendelea kuhabarisha wananchi na wapiga kura juu ya mipango ya sera za vyama vya siasa na ahadi za wagombea kama inavyojiri katika mikutano ya kampeni.
Katika tamko hilo, asasi za kiraia zinatakiwa kuendelea kuelimisha wananchi juu ya masuala mbalimbali yanayoeneza uangavu kwa wapiga kura na wananchi kwa ujumla juu ya sheria, taratibu, kanuni za uchaguzi, haki na wajibu wa kuhudhuria mikutano ya kampeni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), Ananilea Nkya, aliwataka wagombea kutambua wananchi pekee ndio wenye mamlaka ya kumuweka mtu madarakani na kuwataka waandishi wa habari kuwajengea uelewa wa kukubali kushindwa.
Alisema baadhi ya mashirika ya utafiti nayo yanatakiwa kukemewa vikali, kwani baadhi ya tafiti zao zimeonekana kupindua maamuzi ya wananchi, hasa pale yanapoonyesha asilimia ya kushinda kwa chama fulani.
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu, Francis Kiwanga, alisema inashangaza kwa mara ya kwanza JWTZ kutangaza vita na raia badala ya kutangaza vita na maadui wanaovamia mipaka ya nchi.
Wiki iliyopita Luteni Jenerali Shimbo akiwa ameambatana na maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi, akiwamo Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Peter Kivuyo na Mkuu wa Operesheni Maalumu (DCP) Venance Tossi, alitoa tamko kali akidai dalili zimeanza kujitokeza za kutaka kuvunja sheria katika kampeni, kuchochea fujo na uvunjifu wa amani.
source:http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=19999