Monday, December 22, 2014

SITOKUBALI KUONA UJENZI WA MAABARA UNAKWAMA - RC KIGOMA


SITOKUBALI KUONA UJENZI WA MAABARA UNAKWAMA - RC KIGOMA
Na Editha Karlo wa Globu 
ya Jamii, Kigoma 
WAKATI mkoa Kigoma ukiwa umefikia asilimia 90 ya ujenzi wa maabara za sayansi kwenye shule za sekondari mkoani humo MKUU wa mkoa Kigoma Mhe Issa Machibya amesema kuwa hatakubali kuona mtu yeyote anakwamisha jitihada za ujenzi huo na atamshughulikia kikamilifu. 
 Akizungumza wakati akikabidhi maabara kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Buyungu wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma Mhe Machibya alisema kuwa wanaotaka kutumia siasa kwenye suala la maabara na kukwamisha ujenzi wake atashughulika nao. 
 Alisema kuwa ujenzi huo wa maabara ni utekelezaji wa agizo la Raisi Jakaya Kikwete na kwamba kwao ni sharia na inapaswa kutekelezwa kulingana na maelezo na maelekezo yaliyotolewa na Raisi kuhakikisha shule zote za sekondari mkoani humo zinakuwa na maabara za sayansi.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa shukrani za dhati kwa wananchi,madiwani,Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri ambao walitumia muda wao mwingi kuhakikisha kwamba mpango wa ujenzi wa maabara katika shule za sekondari mkoani humo unafanikiwa. 
 Akizungumzia katika makabidhiano hayo Afisa Elimu wa mkoa Kigoma,Salvatory Shauri alisema kuwa jumla ya vyumba 375 vya maabara katika shule 125 za sekondari mkoani humo vilihitaji kujengwa kuwezesha maabara katika shule hizo kufanya kazi. 
 Shauri alisema kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa ujenzi huo licha ya changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza ikiwemo baadhi ya wanasiasa kuwahamasisha wananchi kutoshiriki katika ujenzi huo. 
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kakonko,Peter Toima Kiroya alisema kuwa ujenzi wa maabara katika shule za sekondari mkoani humo umetoa somo kubwa kwa halmashauri na serikali katika kutekeleza miradi ya ujenzi kwa gharama nafuu na kwa viwango vinavyohitajika kwa kutumia mafundi kutoka vijijini kuliko kutumia wakandarasi. 
 Toima alisema kuwa katika ujenzi wa vyumba vya maabara mafunzi kutoka vijiji mbalimbali wamefanya kazi kwa ustadi mkubwa na kwa viwango kulingana na maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na wahandisi wa Halmashauri tofauti na baadhi ya wakandari ambao wamekuwa wakitumia gharama kubwa na baadhi ya miradi ikitekelezwa katika viwango duni.
MKUU wa mkoa Kigoma Mhe Issa Machibya akifunia pazia kuashiria kukabidhi maabara katika  shule ya sekondari Buyungu nwilaya ya Kakonko
MKUU wa mkoa Kigoma Mhe Issa Machibya akikata utepe pamoja na viongozi wengine wa mkoa na wadau wa elimu  kuashiria kukabidhiwa maabara katika  shule ya sekondari Buyungu nwilaya ya Kakonko. Picha na Editha Karlo wa Globu ya Jamii, Kigoma