Hatimaye mjane wa marehemu Muhidini Gurumo, Pili Kitwana amepokea Sh2 milioni kutoka Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii NSSF kwa ajili ya ununuzi wa Bajaji.
NSSF ilitoa fedha hizo ikiwa ni juhudi za Shirikisho la Muziki nchini (SHIMUTA), ambapo walimuahidi kumpatia mjane huyo kiasi cha fedha ambacho kitamuwezesha kununua bajaji imsaidie kuendesha maisha yake.
"Mwaka huu mwezi wa tano tulimuahidia mama Gurumo tutamsaidia kusaka fedha kwa wadau mbali mbali tuweze kufanikisha azma yetu ya kununua Bajaji, tuliomba NSSF na leo wamempatia mjane wa Gurumo Sh2 milioni."alisema Addo November Rais wa SHIMUTA na kuongeza
"Shirikisho tulishampa Sh1.2 na leo anapatiwa Sh2 milioni lengo letu lilikuwa bajaji lakini anakabidhiwa fedha rasmi yeye ni mtu mzima ataamua mwenyewe fedha hizo kama atazitumia kwa matumizi yake au kwa biashara ni umauzi wake, lakini sisi kama shirikisho bado tunaendelea na juhusi zetu za kuhakikisha tunamsaidia kwa njia moja au nyingine."alisisitiza.
Naye Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa (NSSF), Juma Kintu alisema "tunathamini michango ya wasanii, tunajua bajaji itamsaidia kuingiza mapatoa, hakuna asiyefahamu mchango wa Gurumo kwenye tasnia ya muziki, NSSF tutaendelea kusaidia wasanii wetu pale inapohitajika.
Mwanamuziki mkongwe Kassim Mapili akizungumzia hilo huku akijipigia chapuo asaidiwe dawa za ugonjwa wake wa moyo alisema "Gurumo hakuwa mvivu wa kazi toka enzi za Nuta, Juwata hadi Msondo, alitutoka tarehe kama ya leo, NSSF nisaidieni na mimi nipate hela za kununua dawa nasumbuliwa na ugonjwa wa moyo, nililazwa Muhimbili kwa wiki mbili mpaka sasa natumia dawa.
Hata hivyo, ofisa mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu alisema ombi hilo wamelipokea na kuitaka SHIMUTA kuandika barua rasmi ili waweze kumsaidia mkongwe huyo wa muziki.
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Juma Kintu (wa pili kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya sh. mil 2 kwa mjane wa marehemu Muhidini Gurumo, Pili Kitwana.katikati ni Shirikisho la Muziki nchini (SHIMUTA),Addo November.