Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal jana Desemba 10, 2014, amewahutubia wawakilishi wa Afrika katika Mkutano wa Mazingira Duniani (Cop20) unaofanyika jijini Lima, nchini Peru.
Mheshimiwa Makamu wa Rais anahudhuria mkutano huu akimuwakilisha Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Kiongozi wa Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi. Mkutano huo wa jana ulikuwa na dhima ya Afrika baada ya mwaka 2015: Makubaliano Mapya kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Awali Mheshimiwa Dkt. Bilal aliwaambia wawakilishi wa Afrika katika mkutano uliojumuisha Mawaziri wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya Mazingira katika nchi zao kuwa, Afrika licha ya unyonge wake bado inalo jukumu la kusimama kidete katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na ili kufanikiwa katika jambo hilo ni muhimu kwa Bara hili kuwa na sauti ya pamoja.
Mheshimiwa Makamu wa Rais aliendelea kusema kuwa, Bara la Afrika lina kila sababu ya kuwa na mipango yake ambayo itatumika kushirikisha nchi za nje ya Afrika ili kwa pamoja Dunia iweze kuwa na kauli inayofanana yenye kulenga kukabiliana na majanga yanayotokana na mabadiliko ya Tabia Nchi licha ya kuwepo tofauti za kimaendeleo kati ya Afrika na nchi za mabara mengine.
Awali akizungumza kabla ya Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri wa Mazingira wa Sudan ambaye ni Mwenyekiti wa kundi hili la Afrika Dkt. Hassan Albdelgadir Hillal alisema, kundi la Afrika linapongeza uongozi wa Tanzania kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete kwa namna unavyosimamia agenda hizi za mabadiliko ya Tabia Nchi na kusimamia upatikanaji wa sauti moja kutoka kwa nchi za Afrika.
Dkt. Abdelgadir aliendelea kusema kuwa, Afrika inatakiwa kutumia mkutano huu wa Lima kwa umakini ili kuhakikisha mipango inayofikiwa inapata kutambulika na kuonekana mwakani wakati mkutano kama huu utakapofanyika jijini Paris.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dkt. Binilith Mahenge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa Mazingira kwa nchi za Afrika yeye alibainisha kuwa, viongozi wa nchi za Afrika wamekuwa mstari wa mbele kabisa kuhakikisha kuwa Afrika inasikika na kwamba anatarajia ushirikiano katika ngazi ya Mawaziri kuendelea hata pale atakapokuwa anakabidhi nafasi hiyo kwa Waziri wa Mazingira wa Misri.
Katika mkutano mwingine ambao pia ulikuwa mwendelezo wa Siku ya Afrika katika COP20, Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal alisisitiza kuwa Afrika inatakiwa kuhakikisha vijana na akina mama wanakuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na hali hii ya mabadiliko ya tabia nchi. "Makundi haya ni muhimu sana kwa kuwa ndiyo yanayohusika moja kwa moja na shughuli za kila siku. Hatutaweza kufanikiwa kama tutayaacha makundi haya nyuma," alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais katika Mkutano huo ambao pia ulihutubiwa na Dkt. Fatima Denton, Mkurugenzi wa Harakati Maalum kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kamishenbi ya Uchumi kwqa Afrika (UNECA).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam ya Afrika katika masuala ya Majadiliano ya Mabadiliko ya Tabianchi kutoka nchini Sudan, Nagmeldin El-Hassan, wakati alipokuwa akiwasili katika ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kuzungumza na wawakilishi wa Afrika katika mkutano wa Mazingira Duniani (Cop20) unaoendelea jijini Lima, nchini Peru.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Wawakilishi wa Afrika katika mkutano wa Mazingira wa Dunia (Cop20) (hawapo pichani) alipokuwa akiwahutubia leo Desemba 11, 2014. Katikati ni Waziri wa Mazingira wa Sudan, (kushoto) ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalam ya Afrika katika masuala ya Majadiliano ya Mabadiliko ya Tabianchi kutoka nchini Sudan, Nagmeldin El-Hassan.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na baadhi ya wawakilishi wa Afrika katika mkutano wa Mazingira wa Dunia (Cop20) baada ya kuwahutubia leo Desemba 11, 2014, katika Mkutano wa Mazingira Duniani na majadiliano kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, unaoendelea jijini Lima, nchini Peru.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa Mazingira Duniani, wakimsikiliza Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal, wakati akiwahutubia leo, Desemba 11, 2014, mkutano wa Mazingira Duniani (Cop20) unaoendelea jijini Lima, nchini Peru.
Sehemu ya Wawakilishi wa nchi za Afrika katika mkutano wa Mazingira Duniani, wakimsikiliza Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal, wakati akiwahutubia leo, Desemba 11, 2014, mkutano wa Mazingira Duniani (Cop20) unaoendelea jijini Lima, nchini Peru.