Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwenyekiti wa PAC Zitto Kabwe
---
Nashambuliwa, tunashambuliwa! PAC tunasema "Hatutetereki"
Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Kamati ninayoongoza ya PAC kuwasilisha Bungeni Taarifa Maalumu kuhusu ukaguzi maalumu wa akaunti ya Tegeta Escrow, kumekuwa na kampeni za chini chini zinazoendeshwa kwenye korido za Bunge na kwenye mitandao dhidi yangu binafsi na baadhi ya wabunge waliosimama kidete dhidi ya wizi wa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania akaunti ya Escrow.
Baadhi ya tuhuma nimezipeleka kwenye vyombo vya dola ili zichunguzwe kwani zina vielelezo vya mahala pa kuanzia (kama leseni ya udereva ya mwanamke anajulikana kama Vivian Emmanuel Sirikwa na muhuri wa kampuni ya uwakili inayomilikiwa na Bwana Joseph Mkandege).
Baadhi ya Tuhuma
Baadhi ya tuhuma nitazijibu moja baada ya moja.
Waziri mmoja ambaye ni mtuhumiwa wa wizi wa fedha za Tegeta Escrow anazunguka kwa wabunge akisema tuhuma hizi kupikwa kama njia yake ya kuhamisha mjadala kutoka uporaji wa Tshs 200 bilioni kwenda kwenye masuala binafsi.
Tuhuma hizi zenye kichwa cha habari "Zitto na Filikunjombe wanatumiwa na Kenya na Uingereza kuvuruga na kudhoofisha Uwekezaji nchini mwetu" zinajibiwa hapa chini. Utaona ndugu Filikunjombe ametajwa kwa kichwa cha habari ili kumtaja tu bila sababu yeyote ile.
Tuhuma #1:
Zitto anaye rafiki yake Mkenya aitwae Rapahel Ongangi ambao kwa pamoja wameanzisha Gombe Advisors Co. Ltd (registered on 24 November 2011, Certificate No 87387) kwa ajili ya kufanya biashara na Makampuni ya Gesi na Mafuta yanayofanya kazi nchini hapa.
Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Kamati ninayoongoza ya PAC kuwasilisha Bungeni Taarifa Maalumu kuhusu ukaguzi maalumu wa akaunti ya Tegeta Escrow, kumekuwa na kampeni za chini chini zinazoendeshwa kwenye korido za Bunge na kwenye mitandao dhidi yangu binafsi na baadhi ya wabunge waliosimama kidete dhidi ya wizi wa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania akaunti ya Escrow.
Baadhi ya tuhuma nimezipeleka kwenye vyombo vya dola ili zichunguzwe kwani zina vielelezo vya mahala pa kuanzia (kama leseni ya udereva ya mwanamke anajulikana kama Vivian Emmanuel Sirikwa na muhuri wa kampuni ya uwakili inayomilikiwa na Bwana Joseph Mkandege).
Baadhi ya Tuhuma
Baadhi ya tuhuma nitazijibu moja baada ya moja.
Waziri mmoja ambaye ni mtuhumiwa wa wizi wa fedha za Tegeta Escrow anazunguka kwa wabunge akisema tuhuma hizi kupikwa kama njia yake ya kuhamisha mjadala kutoka uporaji wa Tshs 200 bilioni kwenda kwenye masuala binafsi.
Tuhuma hizi zenye kichwa cha habari "Zitto na Filikunjombe wanatumiwa na Kenya na Uingereza kuvuruga na kudhoofisha Uwekezaji nchini mwetu" zinajibiwa hapa chini. Utaona ndugu Filikunjombe ametajwa kwa kichwa cha habari ili kumtaja tu bila sababu yeyote ile.
Tuhuma #1:
Zitto anaye rafiki yake Mkenya aitwae Rapahel Ongangi ambao kwa pamoja wameanzisha Gombe Advisors Co. Ltd (registered on 24 November 2011, Certificate No 87387) kwa ajili ya kufanya biashara na Makampuni ya Gesi na Mafuta yanayofanya kazi nchini hapa.
Majibu:
Gombe Advisors ni kampuni binafsi isiyofanya faida yaani 'Company Limited by Guarantee'. Haina kazi na kampuni yoyote ya Gesi na Mafuta na wala yenyewe haijuhusishi na biashara hiyo. Gombe advisors haijafanya kazi yoyote ile na kampuni nyingine zaidi ya kusaidia wasanii wa kundi la Kigoma All stars. Upotoshaji hapa unalenga kupindisha mjadala.
Tuhuma #2:
Zitto amemsaidia Ongangi kupata uraia wa Tanzania na kwa sasa ni raia wa pasipoti. Zitto na Ongangi walimtafutia CEO wa Shell aitwae Axel Knospe nyumba na gari ya kukodi.
Majibu:
Raphael ni mtu binafsi ambaye anafanya shughuli zake hapa nchini, amesoma hapa nchini na ameoa na ana mtoto. Tuhuma hizi hazina msingi wowote ule maana ni uwongo. Wanaotoa tuhuma hizi waonyeshe hiyo pasipoti ya Bwana Ongangi kuthibitisha madai yao.
Tuhuma #3:
Mikataba ya STATOIL iliyokuwa inarushwa kwenye mitandao ya jamii na kuchapishwa kwenye magazeti ya Kenya ya hapa nchini (The Citizen na Mwananchi) mwandishi mkuu alikuwa huyo CEO wa Shell.
Majibu:
Mkataba uliovujishwa wa StatOil ulivujishwa na waandishi wa habari wa Norway. Uchambuzi wa mkataba huo nimeufanya mwenyewe kwa kutumia utaalamu wangu niliosomea wa kuchambua mifumo ya kodi kwenye sekta ya mafuta na gesi. Kwa namna yoyote ile, huyo anayetajwa kuwa CEO wa kampuni ya Shell hahusiki. Tuhuma hii wanaoitoa watoe ushahidi usio na chembe ya mashaka.
Ikumbukwe kuwa mkataba wa StatOil utaipotezea Tanzania mapato ya dola za Marekani bilioni 12 (takribani Tshs 20,400,000,000,000/=) katika kipindi cha miaka 15 baada ya gesi kuanza kuchimbwa.
Uamuzi wa Kamati ya PAC kutaka mikataba yote ya Gesi kuwa wazi una lengo la kuchambua kuona kama mikataba yote nchini haipotezi mapato kwa nchi. Uamuzi huo umewakasirisha sana baadhi ya waliohusika kuingia mikataba Serikalini maana wanajua kuna madudu kwenye mikataba na wanataka umma wa watanzania usijue!
Tuhuma #4:
Kampuni ya SHELL imechukizwa sana kucheleweshwa kwa kupata kibali cha kutafuta gesi na mafuta kule Pemba. Vilevile SHELL haina uwekezaji mkubwa Tanzania Bara kwani ilishindwa kwenye tenda zenye vitalu vyenye gesi nyingi upande wa Bara.
Majibu:
Ukweli ni kuwa Kampuni ya Shell ina vitalu 4 huko Zanzibar na tayari ina makubaliano na Serikali ya Zanzibar kuhusu utafutaji mafuta huko katika vitalu namba 9,10,11 na 12. Shell inafanya kazi na kampuni ya Petrobras ya Brazil kwenye kitalu namba 6 na namba 8. Taarifa hizi zipo wazi kwenye tovuti ya TPDC. Tuhuma nyepesi namna hii dhidi ya kampuni kubwa kama Shell zinaonyesha dharau na kiburi kinachotokana na uelewa mdogo wa mambo wa watu wanaotuhumu.
Tuhuma 5:
Ongangi anapokea maelekezo kutoka Serikali ya Kenya kuhujumu uwekezaji nchini mwetu.
Majibu:
Nazifahamu mbinu nyingi zinazotumika kufanya propaganda, lakini mbinu hii imeshindwa ikiwa mapema sana. Ni vema wanaotoa tuhuma hizi wazithibitishe vinginevyo ni mwendelezo wa propaganda zisozingatia diplomasia ndani yake dhidi ya jirani zetu wa Kenya. Hizi ni propaganda hatari ambazo hata hao wanaotuhumiwa wakisikia watatudharau sana.
Tuhuma #6 (juu ya Uingereza):
Uingereza imekuwa inamfadhili Zitto kwa miaka mingi kwa mambo yake ya kisiasa kwa hiyo sasa hivi Ubalozi wa Uingereza unamlipa Zitto na Kafulila kuhakikisha kwamba Standard Chartered ya Uingereza inalipwa deni lake lisilotambulika kisheria nchini mwetu.
Majibu:
Nimetangulia kusema hapo awali kuwa kuna propaganda ambazo haziangalii hata diplomasia; nyingine ni hii. Pamoja na kukanusha uzushi huu, ni vizuri wanaotoa tuhuma za namna hii kuthibitisha. Mimi binafsi sijawahi kufadhiliwa kisiasa na Taifa lolote lile. Inaelekea kuna wanasiasa wanaofadhiliwa na mataifa mengine ambao kwakuwa kwao ndiyo maisha wanaamini na wengine tupo kama walivyo.
Kwangu itikadi yangu ni 'Uzalendo kwa nchi yangu', ni jambo ambalo halina mbadala wake. Siku zote nasema "Right or wrong, my country first".
Kurudia kurusha tuhuma kwa Ubalozi wa Uingereza nchini ni kudhihirisha kwa mara nyingine kiburi cha kuwa na mamlaka (arrogance of power) walicho nacho wanaotuma tuhuma hizi.
Aidha, wanatuhumu kuwa "Kafulila na Zitto wamehaidiwa 15% ya USD 150 million kama deni likilipwa"
Mtanzania anayeweza propaganda dhaifu kama hizi basi anatakiwa ajitafakari. Hata hivyo ni vema wanaotoa tuhuma hizi wathibitishe bila chembe ya mashaka.
Tuhuma #7:
Mbunge Mkono nae ameshikwa hasira kupoteza kazi ya uwakili pale TANESCO. Kafulila na Zitto wanalipwa na Mkono kuvuruga Serikali kwa hasira za kukosa fedha za kitapeli za TANESCO.
Majibu:
Hizi ni tuhuma ambazo sasa tumezizoea kutolewa. Mambo mepesi hayawezi kujibu mambo ya msingi kama tuhuma za wizi wa fedha zaidi ya Tshs bilioni 200 kutoka Benki kuu ya Tanzania. Kukusanya kila propaganda ili kuuhamisha umma ni kupungukiwa hekima na busara.
Aidha, wanaotuhumu wanadokeza kuwa "Naomba tuwe macho na Wabunge wetu achananeni na madai ya Zitto ya wizi. Huyu mtu anafanya biashara na Kampuni ya SHELL na inasemekana analipwa na Ubalozi wa Uingereza. Serikali ya Kenya na tapeli mkubwa Mbunge Mkono nae anawalipa Zitto na Kafulila".
Watanzania, haya ni maneno ya hasira ya watu wanaokaribia kukamatwa kwa kushiriki wizi wa fedha katika Benki kuu ya Tanzania. Kamwe tuhuma kama hizi haziwezi kutukatisha tamaa katika kupambana ili ukweli ujulikane. Sisi tutapigana kwa ajili ya Taifa, kwa ajili ya mtanzania na tunachotaka ni umma uujue ukweli wa mambo.
Hasira hizi zinatokana na mambo mawili:
Moja ni uamuzi wa kamati ya PAC kuwasweka ndani baadhi ya watendaji wa TPDC kwa kushindwa kutekeleza maamuzi ya Kamati yanayohusu uwazi wa mikataba ya Gesi na Mafuta.
Pili, ni uamuzi wa PAC kuagiza ukaguzi maalumu wa mchakato mzima wa kuanzishwa na kufungwa kwa akaunti ya Tegeta Escrow ambapo zaidi ya shilingi bilioni 200 ziliporwa na zaidi ya shilingi bilioni 12 zinalipwa na TANESCO kila mwezi kwenda kampuni ya PAP inayomilikiwa na Harbinder Singh Seth (50%) na watu wasiojulikana kupitia kampuni ya Simba Trust iliyosajiliwa na kufichwa nchini Australia (50%).
Ieleweke kuwa PAP inalipwa shilingi milioni 400 kila siku kutoka TANESCO izalishe au isizalishe Umeme! Watanzania, PAP itaendelea kulipwa namna hiyo kwa miaka 20 ijayo. Kwa namna ambayo Seth analindwa na baadhi ya watendaji Serikalini na hasa ndani ya Wizara ya Nishati na Madini. Aidha, kuna fununu kuwa kuna maofisa serikalini wanaomiliki hizo 50% za kampuni ya PAP. Seth pia anamiliki kitalu cha gesi Mnazi bay Kaskazini kupitia kampuni ya HydroTanz.
Hasira hizi walizo nazo wanaonituhumu na Kamati yangu zimewapelekea kugushi nyaraka mbalimbali zinazonituhumu mimi na wenzangu ili kutuogopesha na kutukatisha tamaa katika kutafuta ukweli juu ya suala la uporaji wa fedha kutoka Benki kuu. Lengo lao ni kututoa kwenye mstari. Mimi na wenzangu hatutatoka kwenye mstari, tutashirikiana na wabunge wenzetu kuhakikisha ukweli unajulikana na wezi kuchukuliwa hatua kali.
Harbinder Singh Seth aliiangusha Serikali ya KANU nchini Kenya, sasa anachotaka kukifanya kinaweza kuiangusha Serikali ya CCM wakiendelea kumkumbatia.
Watanzania sio mabwege!
Zitto Kabwe
Mwenyekiti PAC
Dodoma, 9 Novemba 2014