Tanzania ni nchi ya kwanza kwa Afrika Mashariki katika kuvutia uwekezaji kutokana na sera iliyopo ikiwamo kudhibiti mfumuko wa bei.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Bodi wa Mfuko wa Uwekezaji wa Umoja (UTT), Profesa Joseph Kuzilwa, wakati akifungua Mkutano mkuu wa tisa wa mwaka wa wawekezaji wa Mfuko wa Umoja.
Alisema mbali na Tanzania kushika nafasi ya kwanza, pia ni ya nane kwa Ukanda wa Jangwa la Sahara kwa uwekezaji.
Katika mkutano huo, Profesa Kuzilwa alisema mfuko huo umekua kwa kiwango cha asilimia 51.2 kutoka Sh118.3 bilioni mwaka 2012/13 hadi kufikia Sh178.9 bilioni mwaka huu.
"Idadi ya wawekezaji kwenye mfuko huu imeongezeka na kufikia 117,471 kwa mwaka wa fedha ulioshia Juni 30, mwaka huu na kwamba Mfuko wa Umoja pekee umeongezeka kwa kiwango cha asilimia 51.3 kutoka Sh107.20 bilioni hadi kufikia Sh162.2 bilioni na wawekezaji kwenye mfuko huo walioongezeka kutoka 106,266 hadi 107,376," alisema Profesa.
Aliitaja changamoto inayowakabili kuwa ni mabadiliko ya teknolojia yaliyosababisha meneja wa mfuko kuendelea kuwekeza katika tehama ili kuendana na ukuaji wa soko na kufikia matarajio ya wawekezaji.
Alisema utekelezaji wa malengo ya uendeshaji wa mifuko umekamilisha mpango mkakati wa miaka mitano na unatoa vipaumbile na mikakati ya uendeshaji wa mifuko.
"Mikakati iliyopo ni kuendeleza uwekezaji katika Tehama ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wawekezaji pamoja na kuwafikia wawekezaji wengi zaidi na kuendelea kufanya upembuzi wa fursa katika soko la Ukanda wa Afrika Mashariki"aliongeza.
Alisema mfuko ya uwekezaji una aina tano ambazo ni mfuko wa Umoja, Mfuko wa wekeza maisha, mfuko wa watoto, mfuko wa kujikimu na mfuko wa Ukwasi.
Alisema Dhamana ya uwekezaji Tanzania inaendelea kufanya utafiti juu ya njia bora, rahisi na
zilizo na ufanisi katika kuwawezesha wawekezaji katika mfuko wa umoja kupata gawio na matokeo ya utafiti na maandalizi yatawasilishwa kwa wawekezaji pindi itakapokamilika.