Wednesday, November 26, 2014

Soma Taarifa ya VIP Engineering and Marketing Ltd: Umiliki wa fedha za escrow hauna utata, tatizo ni Mawakili


Soma Taarifa ya VIP Engineering and Marketing Ltd: Umiliki wa fedha za escrow hauna utata, tatizo ni Mawakili

Taarifa ya VIP Engineering and Marketing Ltd: Umiliki wa fedha za escrow hauna utata, tatizo ni Mawakili  
--
Kinachoitwa kwamba ni kashfa ya akaunti ya Escrow ni ngoma ambayo wanaoichezesha wanafanya hivyo kwa matumaini kwamba wakiivutia kwao basi hatimaye watafaidika ipasavyo. Miongoni mwa wanaoishangilia ngoma hii ni baadhi ya mawakili waliokuwa wakiitetea Tanesco na Benki ya Standard Chartered.

Benki ya Standard Chartered inataka kuhakikisha kwamba kunakuwapo na sintofahamu kuhusu akaunti hiyo ya Escrow na kulazimisha imilikiwe ama na Serikali ya Tanzania au Tanesco kwa sababu hiyo inaweza kuisaidia katika lengo lake kuu la kupata fedha isizostahili. Ni wazi kwamba fedha zilizohifadhiwa katika akaunti hiyo ya Escrow si za Serikali wala si za Tanesco kama ambavyo Standard Chartered na wapambe wao wanavyolazimisha iwe. Fedha hizo ni za IPTL.

Migogoro kati ya TANESCO na IPTL ilianza mwaka 1998 baada ya IPTL kukamilisha kwa kiasi kikubwa ujenzi wa mtambo wa 100MW Tegeta Mjini Dar es Salaam. IPTL walitaka Tanesco inunue umeme kwa bei kubwa kuliko ilivyo kuwa halali lakini Tanesco walikataa kwa madai kwamba gharama zilizoainishwa na IPTL zilikuwa kubwa mno kuliko gharama halisi za uwekezaji.

Tanesco katika jitihada za kujinasua iliajiri kampuni ya uwakili ya Mkono & Co. Advocates ili kutoa huduma za kisheria kwa kushirikiana na Huntons & Williams ya Marekani.

Kutokana na tofauti za mitazamo ya gharama za uwekezaji, mawakili hawa waliishauri Tanesco ifungue kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji {ICSID} nchini Uingereza dhidi ya IPTL ili kupinga gharama hizo.

Katika uamuzi wa Julai 2001 uliotolewa na ICSID kwenye kesi iliyofunguliwa na Tanesco dhidi ya IPTL mwaka 1998, mahakama hiyo ilitoa uamuzi kwamba, gharama za uwekezaji zishuke kutoka dola za Marekani milioni 163.53 hadi milioni 121.83.

Uamuzi huo wa mwaka 2001 uliridhia mfumo wa kifedha {financial model} iliyokuwa imekubalika katika kukokotoa viwango {tariff calculation} kati ya Tanesco na IPTL ambayo inaipa IPTL marejesho ya uwekezaji {internal rate of return - IRR} ya asilimia 22.31 badala ya asilimia 23.1 iliyodaiwa na IPTL. Mawakili wa Tanesco Mkono & Co Advocates walishauri kwamba Tanesco itekeleze mfumo huo.

Mwaka 2004, mawakili hao hao wa Tanesco wakiongozwa na Mkono & Co. Advocates waliishauri Tanesco isitekeleze ulipaji wa tozo ya uwezo wa kuzalisha umeme {Capacity Charges} kwa kutumia mfumo wa kifedha uliokubalika mwaka 2001. Kutokana na ushauri huo, Tanesco kwa kuamini ushauri wa mawakili wao mwaka 2006 kwa kupinga thamani ya invoices zilizowasilishwa na IPTL kwa kutumia mfumo wa fedha {financial model} iliyotolewa na ICSID. Kitendo hicho kiliifanya IPTL kuupinga uamuzi huo wa Tanesco wa kutofuata ulipaji wa tariff kwa kutumia mfumo wa fedha wa mwaka 2001.

Baada ya Tanesco kupokea ushauri wa Mkono & Advocates iliutilia mashaka na hivyo kuamua kuomba ushauri kwa kampuni ya Huntons & Williams iliyokuwa ikiishauri Serikali katika mashauri ya nje ya nchi.

Kampuni ya Huntons & Williams ilisisitiza kuwa unaosemekana kuwa ni ugunduzi uliofanywa na kampuni ya Mkono & Co. Advocates ulikosa hoja ya msingi yakuifanya Tanesco ipinge kulipa tozo ya uzalishaji umeme {capacity charge} kama ilivyokubalika mwaka 2001.

Ni wazi kwamba ushauri wa kampuni ya Mkono & Advocates ulikuwa ni wa kuipotosha Serikali na Tanesco kwa manufaa binafsi na kwa mantiki hiyo basi kampuni ya Mkono & Co Advocates ilikusudia kesi kati ya Tanesco na IPTL iendelee ili waendelee kulipwa gharama za kuendelea na kesi.

Ushahidi wa upotoshaji ni mwaka 2012 Mkono & Co. Advocates kuitaka Tanesco kukubali usuluhishi nje ya mahakama katika shauri la Tanesco kukataa kuilipa IPTL capacity charges kwa kigezo kwamba uwezekano wa Tanesco kushinda katika kesi ya kupinga kiwango cha tozo ulikuwa mdogo na unaashiria kuendela kuuiingiza Tanesco kwenye hasara kubwa na kesi zisizokuwa na ukomo.

Aidha, moja ya kesi ambazo zinathibitisha kuwapo kwa mgongano wa kimaslahi wa mawakili ni shauri kati ya Tanesco na Benki ya Standard Chartered ya Hong Kong {SCB-HK} lililoko ICSID.

Shauri hilo linawakilishwa na mawakili wenye asili na historia ya pamoja na kampuni ya Mkono & Co. Advocates. Mkono & Co. Advocates anaiwakilisha Tanesco na kwa upande mwingine Bw. Charles Morison mwenye mahusiano makubwa na kampuni ya Mkono & Advocates kwa kuwa alikwa mwanasheria wake ndiye anaiwakilisha SCB-HK.

Mahusiano haya ya kikazi kati ya mawakili hawa yanaashiria mgongano mkubwa wa kimaslahi na kuifanya Serikali na Tanesco wasinufaike na huduma yao kwa kuwa huduma za mawakili hao zilikuwa zimegubikwa na maslahi binafsi na kuwatwisha Watanzania mzigo mkubwa.

Ukiachilia mbali kizungumkuti hicho cha mgongano wa maslahi tangu kampuni ya Mkono & Co. Advocates kwa pamoja na Huntons & Williams wapewe kazi hiyo ya uwakili na Tanesco mwaka 1998, jumla ya shilingi bilioni 62.9 zimelipwa kwa kampuni ya Mkono & Advocates.

Kadhalika kampuni hizo bado zinaidai Serikali ya Tanzania jumla ya dola za Marekani milioni 4.5.

Ni wazi kwamba gharama zingeweza kuongezeka endapo Serikali na Tanesco wangeendelea kuwatumia mawakili hao kwa kuwa mawakili hao wamekuwa wakishinikiza kujiingiza katika kesi kwa kuipa Serikali na Tanesco matumaini ya kupata ushindi jambo ambalo matokeo yake ni Serikali na Tanesco kuendelea katika kesi zisizoisha kwa hasara kubwa lakini kwa manufaa ya mawakili ambao wamegeuza hizo kesi kuwa miradi yao ya kudumu.

Aidha, kwa mujibu wa Sheria ya Kampuni za Tanzania, ni dhahiri SCB-HK haikusajili hati inayoitwa Deed of Assignment au dhamana nyingine hapa nchini ambazo zingelihalalisha madai ya madeni na dhamana inayodaiwa kuipa benki hiyo uhalali wa kutambulika kisheria kama mdai wa IPTL. 

Baadhi ya mambo yanayoonesha ni jinsi gani mawakili waliipotosha Tanesco ni kwamba SCBHK ilifungua shauri kwenye Mahakama ya Usuluhishi (ICSID ARB/10/20) kimakosa na TANESCO ilipewa ushauri usio sahihi na wanasheria wake kuhusu kesi hiyo.

Jambo linaloshangaza ni kwa vipi mawakili wa TANESCO waliamua kutofuatilia masuala muhimu ambayo yalistahili yafuatiliwe na kujengewa hoja za kisheria. Kwa mfano hoja za kisheria kwamba baadhi ya mashauri mengine hayawezi kusikilizwa nje ya Mahakama za Tanzania lakini mawakili wa TANESCO na Kampuni ya Mkono & Co. Advocates haikutetea hoja hiyo.

Kampuni ya Mkono & Co. Advocates ambayo ilikuwa ni Mawakili wa TANESCO hawakuipasha ICSID kwamba mgororo kati ya TANESCO na IPTL ulimalizika Oktoba 2013. Pia inaelekea kwamba mawakili wa TANESCO walitaka mgogoro uendelee badala ya kufikia mwisho, kwani kila mara walikuwa hawatekelezi kama mteja wao alivyokuwa anataka mambo yawe. 

Mawakili ni waajiriwa waaminifu wa mteja na maafisa wa mahakama. Taaluma yao, licha ya kuwa na umaalumu wake, matakwa ya kutoa ushauri ili mteja awe katika hali ya kujua kila kinachoendelea na pia kama hapana budi kupunguza gharama kama ushauri usingelikuwepo.

Hata hivyo, mawakili wanaofanya kazi wanatakiwa kuwa na uadilifu wa hali ya juu sifa ambazo inaelekea mawakili wa TANESCO wameshindwa kuthibitisha kuwa nazo katika kutimizia wajibu wao kitaaluma. Haya yatajionesha wazi wazi katika kufanya mapitio kwenye maeneo mbalimbali yanayohusu uhusiano wa kibiashara na kiutendaji kati ya TANESCO na IPTL kwa ushauri wa mawakili.

Aidha, katika muendelezo huo huo wa kuivuruga Tanesco Standard Chartered Bank imeiomba ICSID katika shauri ICSID ARB/10/20 kuiamuru TANESCO kuilipa SCB-HK USD 208.3 milioni pamoja na riba ya LIBOR + 4% katika kesi nyingine ya Novemba 14, 2014 deni ambalo uhalali wake unabishaniwa siyo tu na Tanesco bali pia na kampuni ya VIP.

Suala la umiliki wa fedha za escrow halina utata
Kumekuwapo na mchezo mchafu wa kisiasa wa kujaribu kupotosha ukweli kuhusu umiliki wa fedha zilizokuwapo katika akaunti ya escrow iliyojulikana kama Tegeta Escrow.

Ili kuelewa kwamba fedha katika akaunti hiyo zilikuwa zitaendelea kuwa ni za IPTL na kamwe hazijawahi kuwa za Tanesco wala Serikali ni muhimu kutambua ukweli tu kwamba mlipaji wa deni hawezi kuwa mmiliki wa deni analolilipa.

Akaunti ya Escrow ilifunguliwa kutokana na ushauri wa Mkono & Co. Advocates wa mwaka 2004 ambao walitoa hoja kuwa gharama za kununua umeme zilizokokotolewa kwa kutumia asilimia 22.31 ya urejeshwaji wa uwekezaji {IRR} zilikuwa hazikubaliki na hivyo Tanesco walikuwa wakitoa hati ya kupinga malipo kwa kila ankara ya malipo kupinga gharama hiyo kulingana na kifungu Na.6.8 cha mkataba wa ununuzi wa umeme {PPA}. Kifungu hicho kinaeleza kuwa ikiwa upande wowote haukubaliani na usahihi wa malipo katika ankara zilizowasilishwa kwa ajili ya malipo ya gharama za umeme wanatakiwa watoe notisi {Invoice Dispute Notice} kwa upande mwingine.

Vile vile, mawakili wa Tanesco Mkono & Co. Advocates waliishauri kwamba kutokana na pingamizi hilo, ifunguliwe akaunti maalum {Escrow Account} kwa ajili ya kuhifadhi fedha ambazo zilitokana na ankara zilizokuwa zinapingwa.

Ushauri huo ulitekelezwa na Tanesco na mnamo Julai 5, 2006 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini mkataba wa kufungua akaunti maalum kwa ajili ya kuweka fedha zote za ankara zilizopaswa kulipwa kwa IPTL.

Kwa mantiki hiyo Akaunti ya Escrow ilifunguliwa kwa ajili ya kuhifadhi fedha za malipo ya IPTL yaliyokuwa yakisubiri kuthibitishwa na Tanesco kwa pamoja na IPTL kwa pamoja kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 6.8 cha mkataba wa ununuzi wa umeme yaani PPA.

Kwa mantiki hiyo basi ni vema ikafahamika na kueleweka kuwa fedha hizo zilikuwa za IPTL na wala siyo fedha za Serikali wala si za Tanesco.

Ni wazi pia kutambua kwamba wahusika walikuwa na uhuru wa kuweka fedha hizo katika akaunti nyingine yoyote kutegemea na makubaliano yao yaani ya IPTL na Tanesco.

Hivyo basi kitendo cha fedha hizo kuhifadhiwa katika akaunti iliyofunguliwa na kuhifadhiwa katika Benki Kuu haina maana kuwa fedha hizo zilikuwa za Serikali.

Kwa mujibu wa kifungu namba 7.7 cha mkataba wa Akaunti hiyo ya Escrow fedha zilizomo kwenye akaunti hiyo zingeendelea kuhifadhiwa na Wakala wa Escrow {Escrow Agent}, hadi muafaka utakapofikiwa kati ya Tanesco na IPTL kuhusiana na mabishano ya ankara.

Kwa mujibu wa mkataba wa escrow, Benki Kuu ndiyo iliyopewa jukumu la kusimamia na kuendesha akaunti ya Escrow hadi hapo Tanesco na IPTL watakapofikia muafaka na akaunti kufungwa.

Baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania uliotolewa na Jaji Utamwa wa kuiondoa IPTL kwenye ufilisi na kuitambua PAP kama mmiliki wa asilimia 100 wa IPTL, Tanesco ilifanya mazungumzo na IPTL na kukubaliana na kiasi ambacho Tanesco ilikuwa inadaiwa na IPTL.

Baada ya makubaliano kati ya Tanesco na IPTL serikali ilisaini makubaliano na IPTL kuruhusu fedha za akaunti ya Escrow zilipwe kwa IPTL na Benki Kuu ikaagizwa kuzilipa fedha hizo na hatimaye kuifunga akaunti hiyo.

Oktoba 21, 2013 Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini na IPTL walisaini makubaliano ya kutoa fedha zilizomo katika akaunti ya Escrow ili zilipwe kwa IPTL. Makubaliano hayo yaliyojulikana kama Agreement for Delivery of Funds to Independent Power Tanzania Limited yaliambatana na muhtasari wa kikao cha pamoja cha uhakiki wa malipo ya tozo kati ya IPTL na Tanesco pamoja na barua ya Wizara ya Nishati na Madini ikiwasilisha makubaliano hayo na kuiomba Benki Kuu iruhusu malipo hayo kwenda IPTL kama uhakiki ulivyobainisha, na kwa vile matakwa ya kifungu 7.7 cha mkataba wa Akaunti ya Escrow unavyosema yalikuwa yametekelezwa kikamilifu.

Kufuatia maombi ya Benki Kuu kwenda Wizara ya Fedha ya kufunga akaunti ya Escrow kutokana na kumalizika kwa mgogoro kuhusu mali ya uwekezaji na kwa kuzingatia uamuzi wa Mahakama Kuu, mwezi Desemba 2013 akaunti hiyo ya Escrow ilifungwa rasmi.

Wakati wa kufunga akaunti hiyo ya Escrow, Tanesco ilikuwa ikidaiwa na IPTL jumla ya dola za Marekani milioni 79.05 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 125.04 zilizotokana na tozo ya uzalishaji {capacity charges} ambazo hazijalipwa. Kimsingi fedha zilizokuwa katika akaunti ya Escrow wakati wa kuilipa IPTL na kufunga akaunti hiyo zilikuwa kidogo kuliko madai ya IPTL.

Ikumbukwe kwamba kuanzia Septemba 2009 Tanesco iliacha kulipa fedha za tozo ya uzalishaji umeme {capacity charges} kwenye akaunti ya Escrow kwa sababu ya ukata wa TANESCO/ Serikali.

VIP ina Tax Credit kubwa na TRA
Kampuni ya VIP ilipouza hisa zake asilimia 30 kwa PAP mwaka 2013 ilideposit tax credit ya jumla ya TZS 38,186,584,322.-ambazo ni asilimia 30 (30%) ya gharama za mauzo kiasi ambacho ni kikubwa kuliko matakwa ya Sheria ya Capital Gains Tax inayotamka kuwa kiwango kinachotakiwa ni asilimia 10 (10%) kwa sababu VIP iliomba suala la kodi lijadiliwe baadaye ikiwa na washauri wa maswala ya kodi.

Tozo ya uwekezaji wa IPTL ni ya chini

Ukweli usiopingika ni kwamba tozo ya uwekezaji ya IPTL ni senti za Marekani 1.06/kWh ikilinganishwa na za Songas ambazo ni senti za Marekani 4.31/kWh, Symbion senti za Marekani 4.99kWh na Aggreko inayotoza senti za Marekani 5.77/kWh.

VIP inasimamia Maslahi ya Taifa

Wakati wote VIP imetetea maslahi ya Taifa katika IPTL na itaendelea kufanya hivyo hata baada ya kuuza hisa zake kwa PAP. Ikumbukwe kwamba VIP iliiomba Mahakama kuweka masharti katika hukumu ya kesi yake ya kutaka kumaliza mgogoro wa IPTL. Masharti ambayo VIP iliyaomba na Mahakama kuyaridhia ni kutaka wamiliki wapya wa IPTL kampuni ya PAP: Kuongeza uwezo wa uzalishaji wa IPTL mpaka MW 500, kupunguza bei ya umeme wa IPTL kuwa kati ya senti za Marekani 6/kWh na senti za Marekani 8/kWh, PAP kulipa madeni yote halali ya IPTL na kubadilisha matumizi ya mafuta mazito kuendesha mitambo na badala yake itumike gesi asilia.

Imetolewa na 
VIP Engineering and Marketing Limited