JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu sita wakiwemo raia wawili wa Kenya, baada ya kukiri kuhusika na wizi wa fedha zaidi ya Sh milioni 500 zilizoibwa Oktoba 23 mwaka huu katika Benki ya Stanbic, tawi la Mayfair, Kinondoni.
Mbali na raia hao wa Kenya, pia polisi inawashikilia wafanyakazi watatu wa benki hiyo akiwemo Meneja Msaidizi, Celestine Mkumbo (46), mtunzaji wa funguo, Anastazia Ringo (46) na mpelelezi wa benki hiyo, Tegemea Ayoub (39) kwa tuhuma za kula njama na wezi waliohusika na wizi huo.
Akizungumza jana, Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na upelelezi uliofanywa na jeshi hilo kwa kuhusisha mbinu mbalimbali za kiintelijensia.
Aliwataja raia wa Kenya waliokamatwa kuwa ni Francis Wanjohi (39) mkazi wa Nairobi na Richard Ottieno (37), mkazi wa Kisumu ambao kwa mujibu wa Kova ni majambazi sugu waliowahi kuhusika na matukio mbalimbali ya uhalifu nchini Kenya.
Aidha, mtuhumiwa mwingine ametajwa kwa jina la Jumanne Lema (40) mkazi wa Boma Ng'ombe, Hai mkoani Kilimanjaro na pia Gongo la Mboto, Dar es Salaam aliyejitambulisha kujihusisha na shughuli za kufanya biashara mbalimbali.
Alisema watuhumiwa hao ukiacha wafanyakazi wa benki, walikamatwa wakiwa wanapanga kufanya tukio jingine la uporaji katika benki ya DTB, tawi la Kinondoni Morocco, iliyopo katika jengo la Kampuni ya simu ya Airtel.
"Baada ya kukamatwa watuhumiwa walihojiwa na kukiri kwamba walihusika kikamilifu katika tukio hilo wakila njama na wafanyakazi mbalimbali wa tawi hilo la benki ya Stanbic kupitia vikao mbalimbali vilivyoongozwa na meneja msaidizi wa benki hiyo, Selestine Mkumbo na mtunza funguo Anastazia Ringo," alisema Kova.
Aidha Kova alisema uchunguzi uliofanywa baada ya kuwahoji watuhumiwa hao ulibaini kiasi cha zaidi ya Sh milioni 300 kilionekana kuchotwa ndani ya benki hiyo kabla ya tukio kutokea huku kiasi kilichobaki kikiibwa siku ya tukio, jambo linaloashiria kuwa tukio zima lilipangwa mapema na kwamba tukio halisi la uporaji lililenga kupoteza ushahidi.
Hata hivyo, alisema awali baada ya tukio la wizi huo kutokea Polisi iliwakamata zaidi ya wafanyakazi 15 wa benki hiyo kwa ajili ya mahojiano na kisha baadae kuwaachia wakati wakiendelea na upelelezi wao kabla ya hatua ya kuwabaini wahusika halisi wa wizi huo.
Jalada lao limefikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kwa ajili ya kuwafikisha mahakamani wahusika taratibu zitakapokamilika.