Wednesday, November 19, 2014

MWANRI: ZUIENI UBADHIRIFU WA MIUNDOMBINU YA MAJI


MWANRI: ZUIENI UBADHIRIFU WA MIUNDOMBINU YA MAJI

SONY DSCTimu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ikishuka kutoka kwenye tanki la kuhifadhia maji ya Mradi wa Maji wa Ruhuiko Kanisani utakaohudumia zaidi ya wakazi 3000 wa kitongoji ya Kijiji cha Ruhuiko Kanisani na maeneo ya jirani.SONY DSCKiongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kushoto) akizungumza mara baada ya timu yake kukagua Mradi wa Maji wa Ruhuiko Kanisani. Wanaomsikiliza kutoka kulia ni Naibu Katibu Mtendaji (Uchumi Jumla), Prof. Longinus Rutasitara, anayemfuatia ni Msanifu wa Mradi huo Bw. Elezear Ndunguru na Mratibu wa ukaguzi huo Bw. Senya Tuni (Wapili kulia).
…………………………………………………………………
Na Saidi  Mkabakuli
Serikali imetoa wito kwa taasisi za umma kusimamia kwa umakini miundombinu ya miradi ya maji pindi inapokamilika ili kuweza kuwapatia wananchi huduma ya maji ya uhakika mara miradi hiyo inapokabidhiwa kwa kamati za usimamizi wa maji.
Wito huo umetolewa na kiongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati timu hiyo ilipokuwa ikifanya ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu ya maji ya utekelezaji wa program ya maji na usafi wa mazingira katika vijiji 10 vya manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Bibi Mwanri ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia Huduma za Jamii na Masuala ya Idadi ya Watu, alisema kuwa kwa miaka mingi kumekuwepo na ubadhirifu wa miundombinu ya miradi mingi ya maji hali inayorudisha nyuma juhudi za serikali za kuhakikisha kuwa wananchi wanafikiwa na maji safi na salama kote nchini.
"Kumekuwa na tabia mbaya ya ubadhirifu wa miundombinu hii, msikubali waiharibu ama kuiba vifaa vya ujenzi wa miradi yote 10 maana kama munavyoona serikali na wafadhili wamejitolea ili kuhakikisha munafikiwa na huduma hii muhimu," alisema.
Akizungumza wakati timu hiyo ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ilipotembelea na kukagua Mradi wa Maji wa Ruhuiko Kanisani utakaohudumia zaidi ya wakazi 3000 wa kitongoji ya Kijiji cha Ruhuiko Kanisani na maeneo ya jirani, Msanifu wa mradi huo, Bw. Elezear Ndunguru alisema kuwa mpaka sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 55.
"Kasi ya utekelezaji wa mradi huu ni ya kuridhisha kwani mpaka sasa tumeweza kujenga vituo 12 vya kuchotea maji kati ya 15, kinachongojwa kwa sasa ni kukamilika kwa tanki la kuhifadhia maji," alisema.
Msanifu huyo ameongeza kuwa hadi kukamilikwa miradi yote 10 jumla ya shilingi bilioni 2.77 zitatumika na kuweza kuwahudumia zaidi ya wakazi 9000 wa vijiji vitakavyopitiwa na miradi hiyo.
Kwa mujibu wa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo, lengo kuu kwa upande wa maji ni kuongezeka kwa upatikanaji wa maji safi na salama ni mojawapo ya maeneo yanayotiliwa mkazo ili kuweza kuongeza kasi ya maendeleo na kupunguza umaskini miongoni mwa Watanzania.