Wednesday, November 05, 2014

Chama cha Wafanyakazi wa Sekta Binafsi wazindua Dau-Pesa



Chama cha Wafanyakazi wa Sekta Binafsi wazindua Dau-Pesa
Huduma ya kutuma pesa Tanzania imezidi kuimarika baada ya kuazishwa kwa huduma mpya ya kutuma pesa. Huduma hiyo iliyopewa jina la Dau-Pesa leo imezinduliwa na Chama cha Wafananyakazi wa Sekta Binafsi ambapo huduma hiyo itawawezesha Watanzania kulipia huduma mbalimbali ikiwemo Luku, Dawasco, DSTV, na Zuku. 

 Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa Dau-Pesa Dkt. Dauda Salmin alisema huduma hiyo imetengenezwa ili kufanya kazi kwa njia tatu. ''Njia ya kwanza, mteja anaweza kuweka au kutoa pesa kwa kutumia simu ya mkononi ambapo mitandao ya Vodacom, Tigo, Airtel na Zantel itamuwezesha mteja kutumia Dau-Pesa,'' alisema Dkt. Salmin. 

 ''Mteja anayetumia simu anachotakiwa kufanya ni kupiga namba *150*47# na kufuata maelekezo ili kutumia huduma aitakayo,'' aliongeza Dkt. Salmin. Kiongozi huyo alieleza njia ya pili ya kutumia Dau-Pesa ni kupitia mashine za Dau-Pesa zijulikanazo kama Point of Sale (POS) machines.

 ''Mashine hizi zimefungwa katika benki tofauti tofauti nchini ili kumuwezesha mteja kufanya muamala. Katika kufanikisha hili tumeungana na Benki ya Wanawake Tanzania pamoja na Benki ya Convenant ambapo mteja ana uwezo wa kuweka au kutoa pesa kupitia benki hizi kupitia mashine ya POS. Njia ya tatu ni kupitia kadi ya Dau-Pesa. 

 Kwa mujibu wa Dkt. Salmin, wateja wa Dau-Pesa watapewa kadi ambayo itawawezesha kulipia bili kwa kutembelea benki zao. ''Dau-Pesa ni huduma ya kiteknolojia yenye lengo la kumrahisishia mteja huduma ya kutuma, kuweka, kutoa pesa pamoja kufanya malipo ya aina yoyote." Pia Dau-Pesa inapatikana Kenya na Rwanda huku ikiwa na mpango wa kusambaa nchi zote za Afrika Mashariki ndani ya miezi 12 ijayo.
Dkt. Dauda Salmin, Kiongozi wa Dau-Pesa (katikati) akielezea jambo kwa wageni (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa huduma hio jijini Dar es Salaam. Kushoto kwake ni Kheri Tuwa, Afisa wa Masoko kutoka benki ya Covenant, wala kulia kwake ni Aaron Nyanda, Afisa Mkuu wa Masoko kutoka Benki ya Wanawake ya Tanzania. Huduma ya Dau-Pesa imezinduliwa Tanzania siku ya leo, na itawezesha wateja kulipia huduma mbalimbali ikiwemo Luku, Dawasco, DSTV, na Zuku.