Saturday, October 04, 2014

TMA KUJENGA VITUO VYA HALI YA HEWA KWENYE MAZIWA YA VICTORIA,TANGANYIKA NA NYASA


TMA KUJENGA VITUO VYA HALI YA HEWA KWENYE MAZIWA YA VICTORIA,TANGANYIKA NA NYASA
Meneja wa Huduma za Utabiri wa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA), Samwel Mbuya (kulia) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu kufungua vituo vya kutolea huduma za hali ya Hewa katika maziwa ya Victoria,Tanganyika na Nyasa.Kushoto ni Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA),Monica Mutoni.

Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA) imedhamiria kufungua Ofisi za Kutolea huduma za hali ya Hewa ili kupunguza ajali katika maziwa hapa nchini. Hayo yamesemwa leo jijini Dar es salaam na Meneja wa Huduma za Utabiri wa TMA Bw. Samwel Mbuya wakati wa mkutano na waandishi wa Habari.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imeona kuna umuhimu wa kujenga vituo vya kutoa huduma za Hali ya hewa nchini katika maziwa ya Victoria,Tanganyika na Nyasa, vituo hivi vitasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali kwa kuwa tutafunga vifaa vya kisasa vya kupima hali ya hewa Alisema Mbuya.

Aidha Mbuya amesema kuwa TMA imeendelea kuboresha huduma za utabiri wa Baharini kwa kuweka maboya maalum katika ukanda wa bahari ya Hindi pamoja na kufungua kituo cha hali ya hewa katika Bandari ya Zanzibar.

Mbuya alibainisha kuwa kwa upande wa usafiri wa anga TMA imeendelea kutoa huduma zenye kukidhi vigezo vyenye hadhi ya Kimataifa ili kuleta usalama kwa watumiaji wa Usafiri huo nchini.

Akizungumzia kuhusu uboreshaji wa mtandao wa vituo,Mbuya alisema kuwa hivi sasa mtandao huo umeongezeka ikiwemo kusimikwa kwa rada mbili za hali ya hewa moja ipo katika eneo la Bangula-Dar es salaam na nyingine iko katika hatua za mwisho huko Kiseke-Mwanza.

Pia Mbuya aliongeza kuwa Mamlaka hiyo imefanikiwa kuongeza wigo wa usambazaji taarifa zake hadi kufikia zaidi ya radio 40 za kijamii lengo likiwa ni kuwafikia wananchi waliopo vijijini.

Dira ya TMA Inalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015 Mamlaka hiyo inatoa huduma katika viwango vya Kimataifa.