Thursday, October 09, 2014

Tanzania yaahidi itaendelea kuimarisha Maisha ya Wananchi



Tanzania yaahidi itaendelea kuimarisha Maisha ya Wananchi

Afisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Bibi Ellen Maduhu akisoma hotuba katika Kamati ya Tatu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Na Ally Kondo, New York
Serikali imetahadharisha kuwa endapo mchakato wa kuandaa Agenda ya Maendeleo baada ya Mwaka 2015 unaoendelea hivi sasa katika Umoja wa Mataifa, hautazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, dhamira ya kufikia maendeleo endelevu itakuwa ni ndoto kwa kuwa katika kila idadi ya watu watano duniani, mmoja wao ana ulemavu.
Kauli hiyo ilitolewa na Bibi Ellen Maduhu, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, alipokuwa anahutubia wajumbe wa Kamati ya Tatu ya Umoja huo jijini New York, Marekani siku ya Jumatano tarehe 08 Oktoba 2014.
Bibi Maduhu alieleza kuwa wakati utekelezaji wa Malengo ya Milenia unafikia kikomo mwaka 2015, ni muhimu watu wenye ulemavu wakashirikishwa kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Aidha, ni vema nchi zikawa na utaratibu mzuri kuhakikisha kuwa kundi la watu wenye ulemavu linafaidika na hatua za maendeleo zinazopigwa, kwa kuwa hiyo ni haki yao na ni wajibu wakapatiwa.
Hotuba hiyo ilifafanua mikakati mbalimbali inayochukuliwa na Serikali katika kuboresha maeneo mbalimbali ya kijamii kwa faida ya wananchi wake. Maeneo hayo ni pamoja na elimu, afya, ugatuzi wa madaraka na kuondoa umasikini.
Kwa upande wa elimu, alieleza kuwa Serikali inalipa kipaumbele eneo hilo, kwa kuwa inaamini endapo litaimarishwa ipasavyo na kuwafikia watu wote wakiwemo wanyonge itakuwa ni ukombozi kwa sababu itatoa dira ya kuondoa umasikini.
Kwa kuliona hilo, Serikali imechukuwa hatua mbalimbali za kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya shule ya msingi kwa wote. Mchakato uliopo ni kuhakikisha kuwa elimu ya sekondari nayo itolewe kwa wote. Aidha, Serikali inaimarisha elimu ya ufundi ili iweze kutoa ujuzi kulingana na mahitaji ya sasa. Maboresho hayo pia yanagusa elimu ya juu ambayo inapanuka kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.
Mbali na maboresho hayo yanayofanywa katika sekta ya elimu, Bibi Maduhu alikiri kuwa bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi na kutoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana nazo. Changamoto hizo ni pamoja na ubora wa elimu inayotolewa; watoto kutomaliza elimu zao; upungufu wa walimu bora; ukosefu wa vifaa vya kujifunzia kwa njia ya mtandao na vitabu.
Katika sekta ya afya, Serikali imekuwa ikiendelea kuiboresha sekta hiyo kwa kuhakikisha kuwa watu wote wanapata huduma ya afya ya msingi, licha ya changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa rasilimali watu.
Bibi Maduhu alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wote wanawezeshwa ili waondokane na umasikini, hivyo Serikali imekuwa ikiandaa sera zinazotoa fursa kwa wananchi wote kushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao. Sera hizo ni pamoja na ugatuzi wa madaraka kwenda katika Serikali za mitaa ambako ndipo wananchi wengi wanapatikana.