Saturday, June 13, 2015

Acacia Mining yaingia makubaliano na halmashauri tatu nchini



Acacia Mining yaingia makubaliano na halmashauri tatu nchini
Makamu wa Rais wa Acacia, Deo Mwanyika (wa pili kushoto waliokaa) akitiliana saini ya Makubaliano na wawakilishi wa halmashauri za Wilaya ya Msalala na halmashauri ya Mji wa Kahama. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Patrick Karangwa anaemfuatia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Felix Kimaryo. Wanaoshuhudia ni Kamishna Msaidizi wa Madini- Ukaguzi wa Migodi, Ally Samaje (wa kwanza kulia waliosimama) na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya (wa tatu kutoka kulia- waliosimama).
Makamu wa Rais wa Acacia, Deo Mwanyika (wa pili kushoto waliokaa) akitiliana saini ya Makubaliano (MoU) na wawakilishi wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime, Jeremiah Minja akifuatiwa na Mwenyekiti wa halmashauri ya Tarime, Amos Sagara. Wanaoshuhudia ni Kamishna Msaidizi wa Madini- Ukaguzi wa Migodi, Ally Samaje (wa kwanza kulia waliosimama) akifuatiwa na Mweka hazina wa halmashauri hiyo, Julius Ndyanabo (mwenye shati jeupe).
Kamishna Msaidizi wa Madini- Ukaguzi wa Migodi, Ally Samaje akifafanua jambo kabla ya tukio la utiaji saini ya Makubaliano (MoU) ya ulipaji wa ushuru wa huduma (Service Levy) baina ya Kampuni ya Acacia Mining Limited na halmashauri za wilaya ya Tarime, Kahama na Msalala lililofanyika tarehe 10 mwezi Juni mwaka huu.

Kampuni ya Acacia Mining Ltd imetiliana saini ya Makubaliano (MoU) na Halmashauri za Wilaya ya Tarime, Kahama na Msalala ili kuweza kutekeleza ulipaji wa ushuru wa huduma (service levy) kwa kiwango cha asilimia 0.3 ya mapato ghafi ya kampuni hiyo kwa mwaka mzima kwa mujibu wa sheria ya Serikali za Mitaa.

Tukio hilo limefanyika tarehe 10 Juni, 2015 jijini Dar es Salaam makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, Makamu wa Rais wa Acacia, Deo Mwanyika, Kamishna Msaidizi wa Madini- Ukaguzi wa Migodi, Ally Samaje na baadhi ya watendaji wa wizara hiyo.

Akizungumza mara baada ya tukio hilo, Kamishna Msaidizi wa Madini- Ukaguzi wa Migodi, Mhandisi Ally Samaje alisema lengo la kuingia katika makubaliano hayo ni kuhakikisha ushuru unaolipwa na kampuni hiyo unatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo iliyo chini ya halmashauri hizo.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha ushuru unaolipwa na makampuni unaleta tija katika kuibua na kuendeleza miradi mbalimbali kwenye halmashauri husika ili kuepusha fedha hizo kutumika tofauti na makusudio yake. "Pande hizi zimeingia katika makubaliano ili kuhakikisha fedha inayolipwa na mgodi inatumika kwa malengo iliyokusudiwa na si vinginevyo," alisema Mhandisi Samaje.

Alisema makubaliano hayo pia yamelenga kuongeza uwazi wa matumizi ya fedha zitakazolipwa na mgodi huo katika uendelezaji wa miradi ambayo imeibuliwa kwa makubaliano ya pamoja na ya wazi.

"Makubaliano hayo yanasisitiza sana suala la uwazi na uwajibikaji kwani imeelezwa wazi kuwa fedha hizo zitatumika kufadhili na kuendeleza miradi ambayo imeibuliwa kwa uwazi na kwa ushirikiano na makubaliano maalumu ya mabaraza ya Halmashauri hizo," alifafanua Mhandisi Samaje.

Mhandisi Samaje alieleza kwamba kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi waishio kwenye maeneo ilipo migodi husika ya kuwa hakuna faida ambayo wananchi hao wanapata kutokana na uwepo wa migodi hiyo.

Alisema ili kuondokana na malalamiko hayo na kuhakikisha kunakuwa na tija iliyokusudiwa, miradi itakayofadhiliwa kwa fedha hizo itakuwa chini ya uangalizi (overseer) wa Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI pamoja na Wizara ya Nishati na Madini.

Alisema katika makubaliano hayo, halmashauri hizo zinatakiwa kukaa kwa pamoja na kampuni hiyo kujadili maendeleo ya miradi husika na vilevile kutoa taarifa za maendeleo ya miradi husika mara mbili kwa mwaka kwa waangalizi wa miradi husika ambao ni Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI na Wizara ya Nishati na Madini.

Aidha, kwa upande mwingine, Mhandisi Samaje alisema kwa kupitia makubaliano hayo, Kampuni ya Acacia itawasilisha kwa halmashauri hizo taarifa ya wakandarasi na watoa huduma wengine wanaofanya kazi na kampuni hiyo na pia itasaidia halmashauri hizo kuwafikia ili nao waanze kulipa ushuru huo kwa halmashauri husika.

"Hatua ya kampuni hii kukubali kutoa taarifa za wakandarasi itasaidia halmashauri kuwabana wakandarasi hao ili nao walipe ushuru stahiki kwa maendeleo ya halmashauri hizo na taifa kwa ujumla," alisema.

Mhandisi Samaje alizipongeza pande hizo mbili kwa kuingia makubaliano hayo na kueleza kuwa makubaliano hayo yanatarajiwa kuleta tija katika kuendeleza miradi mbalimbali nchini na hivyo kukuza uchumi wa halmashauri husika na taifa kwa ujumla.

Ilielezwa kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo unaanza mara moja ambapo kampuni hiyo itakuwa inalipa ushuru huo kwa awamu mbili ambazo ni mwezi Julai na mwezi Januari.

Aidha, makabidhiano ya makubaliano hayo yanatarajiwa kufanyika wilayani Kahama tarehe 12 mwezi Juni, mwaka huu na yatashuhudiwa na wadau wote.