Migodi ya dhahabu nchini imetakiwa kuiga mfano wa mgodi wa Buzwagi wilayani Kahama katika kutunza na kuweka mazingira ya uzalishaji salama kwa binadamu na viumbe wengine.
Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Mheshimiwa James Lembeli, wakati kamati hiyo ilipotembelea mgodi huo tarehe 30 Oktoba 2014.
Mhe.Lembeli alisema kuwa kamati yake ilifuatilia kwa kina utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kwa migodi ya dhahabu yote nchini na kukuta mapungufu mengi na dosari za utekelezaji. Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa hata hivyo ni mgodi wa Buzwagi pekee ndio uliozingatia maagizo ya Baraza hilo katika kuweka Mazingira bora na salama kwa binadamu kwa kiasi kikubwa.
Lembeli alifafanua kuwa Mgodi wa Buzwagi umeweza kuharibu maji taka ya sumu aina ya cyanide na mabaki ya takataka zingine kutoka mgodini hapo na kuzihifadhi kwa viwango vya kimataifa kama ilivyoagizwa na NEMC.
"Taka sumu za kutoka migodi ya dhahabu zikiachwa zikatiririka hadi kwenye vyanzo vya maji zinaweza kuleta madhara makubwa kwa binadamu na viumbe wengine kama mifugo,ndege na wanyama wa porini"Alieleza Mhe.Lembeli.
Awali akitoa maelezo ya namna mgodi huo unavyohifadhi na kuweka mazingira katika usalama na ubora unaotakiwa kisheria, Meneja Mkuu wa mgodi huo, Bwana Philbert Rweyemamu alisema NEMC imewapa cheti cha kutambua utekelezaji wa kanuni na sheria husika baada ya kufanya ukaguzi wa kina mara kwa mara.
Katika ziara ya mgodi huo unaomilikiwa na kampuni ya African Barrick Gold, wajumbe walionyeshwa bwawa maalumu ya kuhifadhi maji kwa matumizi ya binaadam na pia bwawa la kuhifadhi maji taka ya sumu na madawa yanayotumika kuchenjulia dhahabu.
Meneja Mkuu Rweyemamu aliekuwa akiongoza ziara hiyo alisema bwawa la Buzwagi la kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi ya binaadamu ni bwawa pekee la aina yake hapa nchini ambalo limejengwa kwa teknolojia ya hali ya juu ili kuweza kuhifadhi maji. Alisema bwawa hilo litakua raslimali kubwa kwa jamii ya Kahama hapo mgodi utakapofungwa kwani wataweza kulima mazao kwa mwaka mzima kwa kutumia njia ya umwagiliaji.
Rweyemamu alisema serikali kupitia mkemia mkuu wa serikali imekuwa ikifanya uchunguzi wa kina kwa vyanzo vya maji kuzunguka mgodi huo na kuridhika kuwa hakuna sumu inayovuja kutoka katika mgodi wa Buzwagi.
"Jukumu la kutunza mazingira ni la kila mfanyakazi hapa Buzwagi na idara ya Mazingira ipo tu kwa ajili ya kusimamia utekelezaji " alisema Meneja huyo. Kwa upande wake Mheshimiwa Lembeli alisema kazi ambayo imefanyika katika mgodi wa Buzwagi katika miaka miwili iliopita imekuwa ya kusifika hata katika mahusiano yake na jamii inayozunguka mgodi.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo ya bunge walioshiriki katika ziara hiyo ya mgodi wa Buzwagi ni pamoja na Naibu Waziri (Ofisi ya Waziri Mkuu) Mazingira, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambae nae pia uliumiminia sifa mgodi wa buzwagi kwa kuwa kinara katika utunzaji wa mazingira.
Katika ziara hiyo pia alikuwepo Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Mazingira NEMC Mhandisi Bonaventura Baya ambae aliudhibitisha mgodi wa Buzwagi kuwa wa kwanza kwa utunzaji wa mazingira
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi,Philbert Rweyemamu akiwaelezea Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira jinsi bwawa la uhifadhi wa maji kwa matumizi ya binaadamu lilivyojengwa kitaalam wakati walipotembelea bwawa hilo.
Mhandisi Bonaventura Baya akiusifu mgodi wa Buzwagi baada ya maelezo yaliyotolewa na Meneja Mkuu wa Mgodi kuhusu jinsi mgodi huo unavyozingatia utunzaji wa mazingira.
Naibu Waziri (Ofisi ya Waziri Mkuu) Mazingira, Mheshimiwa Ummy Mwalimu akipewa ufafanuzi zaidi na Meneja wa Idara ya Mazingira wa Buzwagi John Murray.
Wajumbe wa kamati ya Bunge ya Mazingira wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi wa mameneja wa mgodi wa Buzwagi mbele ya bwawa la kuhifadhi maji taka ya sumu.
Wajumbe wakionyeshwa kituo cha afya cha kisasa cha Mwendakulima kilichojengwa na mgodi wa Buzwagi.