Saturday, September 27, 2014

Mwanachuo WA Udom jela miaka sita


Mwanachuo WA Udom jela miaka sita
 slide1
Mahakama ya Wilaya ya  Ilala imemhukumu kifungo cha miaka sita jela, Melkiad Kabunduguru(28) baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kukutwa na noti bandia.
Kabunduguru ambaye ni  mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma(Udom) atatumikia kifungo hicho baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa dhidi yake.
Katika shtaka la kwanza la Kabunduguru atatumikia kifungo cha miaka minne baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu huku shtaka la pili la kukutwa na noti 50 za bandia za Sh5000 mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka miwili.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Juma Hassani alisema mshtakiwa atatumikia  vifungo hivyo kwa pamoja baada ya Mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Juma Hassani alidai kuwa mshtakiwa huyo atatumikia kifungo hicho ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye tabia za wizi.
Kabla ya kutoa hukumu hiyo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mwendesha mashtaka, Felista Mosha uliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye tabia za udanganyifu. 
"Mheshimiwa hakimu naiomba mahakama hii tukufu kutoa adhabu kali dhidi ya mtuhumiwa huyu kutokana na kushamiri kwa vitendo vya udanganyifu na kujihusisha na matumizi ya noti bandia wakati akijua kuwa ni kosa la  kisheria," alidai Mosha .
Baada ya Hakimu Hassani kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, alimuhukumu  Mwiganyi kifungo cha miaka sita jela.
Awali, Wakili wa Serikali, Felista Mosha alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 29, mwaka huu katika Barabara la Ally Hassan Mwinyi katika mashine ya kutolea fedha (ATM) ya NMB iliyopo Chuo cha Biashara (CBE) na kujipatia Sh100,000 kutoka kwa Expedith Mtisi kwa madai kuwa angemrejeshea lakini hakufanya hivyo.
Katika shtaka la pili, mshtakiwa alikutwa na noti bandia 50 za Sh5000.