Habari zilizotufikia hivi punde zinasema Jeshi la polisi mkoani Geita limekamata bunduki saba (pichani) na mabomu kadhaa ya machozi eneo la Ushirombo wilaya ya Bukombe ikisadikiwa kuwa ni kati ya bunduki kumi zilizoporwa na majambazi yaliyovamia kituo cha polisi Bukombe na kufanya mauaji ya askari polisi wawili waliokuwa zamu jana. Bunduki hizo, nne zikiwa SMG na tatu aina ya Shotgun pamoja na panga zimepatikana katika tanuri la kuchomea matofali zikiwa zimefichwa pamoja na mabomu hayo.
Habari zinapasha pia kwamba katika msako huo mkali unaoendelea, Jeshi hilo pia limewatia mbaroni watu wawili wanaohisiwa kuwa ni majambazi yaliyohusika na shabulio hilo, mmoja akiwa kakutwa akiwa na bomu juu ya mti, majira ya jioni ya leo.
Jeshi la polisi nchini tayari limetangaza dau la shilingi millioni 10 kwa mtu yeyote atakaye fanikisha kuwakamata au kuwabaini waliohusika na vitendo hivyo. Taarifa zaidi tutaendelea kuwaletea kwa kadri zitavyopatikana