Monday, August 11, 2014

Watanzania wanaoishi Visiwani Comoro waanzisha rasmi Jumuiya yao



Watanzania wanaoishi Visiwani Comoro waanzisha rasmi Jumuiya yao
Jana tarehe 10 Agosti 2014, Watanzania wanaoishi katika Muungano wa Visiwa vya Comoro waliamzisha rasmi Jumuiya yao. Lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo ni kuwaunganisha wanachama wake, kuwawezesha kushirikiana katika kutambua fursa za maendeleo na kutoa mchango kwa taifa lao la Tanzania. 
Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa Mikuta wa Ubalozi wa Tanzania, Moroni. Wakati akifungua mkutano huo, Mhe. Chabaka Kilumanga, Balozi wa Tanzania nchini Comoro aliwaeleza Watanzania hao kwamba Serikali ya Tanzania inathamini sana na kutambua mchango wa raia wanaioshi nje nchi. Kutokana na kutambua umuhimu wao Serikali imeanzisha Idara inayoshughulikia Watanzania wanaoishi Ughaibuni katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. 
Aidha, Kitengo kama hicho kimeanzishwa katika Ofisi ya Rais wa Zanzibar. Sambamba na hilo, Viongozi wote wamekuwa wakikutana na Watanzania wanaoishi Ughaibuni, kila wanapata fursa ya kufanya hivyo, wanapokuwa nje ya nchi. Mkuu wa Utawala wa Ubalozi, Nd. Ali Jabir Mwadini alitoa mada kuhusu misingi ya uanzishaji wa Jumuiya za Kiraia na kubainisha vipengele muhimu vinavyopasa kuzingatiwa husasan katika katiba ya Jumuiya. Mwisho, ulifanyika uchaguzi wa viongozi wa muda waliopewa jukuma la kuandaa katiba.
Viongozi wapya wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi Kilumanga. Mwenye kanzu kushotoni mwa Balozi, Bw. Salum Ali Abdallah (Mwenyekiti), wa kulia kutoka alipo Balozi ni Bw. Khalfan Salum Khalfan (Makamu Mwenyekiti) anayefuatia kulia ni Bibi Rukia Selemani (Katibu).
 Mhe. Balozi Kilumanga pamoja na watendaji wa Ubalozi wakifuatilia mkutano.
 Sehemu ya Watanzania wanaoishi Comoro wakifuatilia hotuba ya Mhe. Balozi Kilumanga.