Tuesday, August 05, 2014

Tanzania, Marekani zasaini makubaliano ya Utekelezaji wa Power Africa Initiative




Tanzania, Marekani zasaini makubaliano ya Utekelezaji wa Power Africa Initiative
Na Teresia Mhagama

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo pamoja na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Mark B. Childress wamesaini Makubaliano ya Awali (MoU) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Marekani kwa ajili ya kutekeleza mpango wa Serikali ya Marekani wa kusaidia maendeleo ya sekta ya umeme barani Afrika, unaoitwa "Power Africa Initiative" ambao umetengewa kiasi cha Dola za Marekani bilioni 7 na serikali ya nchi hiyo, ambapo makampuni binafsi ya nchi hiyo yaliahidi kuwekeza Dola za Marekani bilioni 9.

Mpango huo uliozinduliwa na Rais Barack Obama wa Marekani wakati alipotembelea Tanzania, mwezi Julai 2013, utainufaisha Tanzania pamoja na nchi nyingine kama Ethiopia, Ghana, Nigeria, Liberia na Kenya.

Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Washington DC, USA mnamo tarehe 3 Agosti, 2014. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Bi. Liberata Mulamula.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ( katikati) pamoja na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Mark B. Childress (wa kwanza kulia) wakisaini Makubaliano ya Awali kwa ajili ya kutekeleza mpango wa Serikali ya Marekani wa kusaidia maendeleo ya sekta ya umeme barani Afrika, unaoitwa "Power Africa Initiative". Wa kwaza kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Bi.Liberatha Mulamula.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ( kushoto) pamoja na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Bw. Mark B. Childress (kulia) wakibadilishana nyaraka mara baada ya kusaini Makubaliano ya Awali kwa ajili ya kutekeleza mpango wa Serikali ya Marekani wa kusaidia maendeleo ya sekta ya umeme barani Afrika, unaoitwa "Power Africa Initiative".