Sunday, August 17, 2014

Serikali yawapiga msasa viongozi wa elimu ngazi ya Mikoa



Serikali yawapiga msasa viongozi wa elimu ngazi ya Mikoa
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO 
Serikali itaendelea kutoa mafunzo kwa watendaji wa Halmashauri na Mikoa juu ya usimamizi wa fedha, manunuzi na takwimu katika masuala ya elimu nchini ili kuwajengea uwezo viongozi hao katika masuala ya usimamizi wa fedha za Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari awamu ya pili (MMES II). 
 Kauli hiyo imetolewa mjini Bagamoyo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia wakati akifunga mafunzo ya viongozi wa elimu ngazi ya mikoa. 
 Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuboresha ujuzi na utendaji kazi wao ili kukabiliana na changamoto zilizopo. 
 Waziri Ghasia amewasihi watendaji hao kuwa washirikiane katika kutekeleza majukumu yao, kwani lengo ni kufanya kazi kwa pamoja ambapo kila mtu anafahamu majukumu yake na mipaka yake ili kufikia malengo yaliyokusudiwa. 
 Katika hatua nyingine Waziri Ghasia amesema kuwa kulingana na Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, jumla ya watu milioni 14,796,537 ambao ni sawa na asilimia 34 wa kuanzia  shule za awali, msingi na sekondari zinazosimamiwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. 
Amefafanua idadi hiyo kuwa watu wa umri wa miaka 5 hadi 6 idadi yao ni 2,755,699 ambao ni sawa na asilimia 6.32, miaka 7 hadi 13 idadi yao ni 8,341,701 ambao ni sawa na asilimia 19.12, miaka 14 hadi 17 idadi yao ni 3,699,137 ambao ni sawa na asilimia 8.48. 
Mhe  Ghasia ameongeza kuwa taarifa hizo ni muhimu katika kuiwezesha Serikali kupanga mipango yote ya kuwaendeleza watu hao katika nyanja zote. 
 Mafunzo hayo yaliwashirikisha Maafisa Elimu na Afisa Mipango wa mkoa 16 pamoja na Maafisa Elimu wilaya, Wahandisi, Waweka hazina pamoja na Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu kutoka halmashauri za mikoa hiyo. 
Baadhi ya mikoa ambayo watendaji wake walishiriki mafunzo hayo ni Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Singida, Kigoma, Manyara, Arusha, Mbeya, Kilimanjaro, Kigoma, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Geita.
 1.      Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia akiwaasa washiriki wa mafunzo katika masuala ya usimamizi wa fedha za MMES II kutoka mikoa 16 nchini ambao ndio watendaji wakuu katika usimamizi wa elimu, wamo Maafisa Elimu na Afisa Mipango mkoa pamoja na Maafisa Elimu wilaya, Wahandisi na Waweka hazina kutoka halmashauri za mikoa hiyo. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi.
 Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa elimu ngazi ya mikoa katika masuala ya usimamizi wa fedha za MMES II wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia wakati wa kufunga mafunzo hayo hivi karibuni katika chuo cha Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Bagamoyo.
1.      Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia akiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji wa mafunzo usimamizi wa fedha za MMES II kutoka  Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, TAMISEMI na chuo cha ADEM pamoja na baadhi ya wanasemina hivi karibuni Bagamoyo.