Sunday, August 17, 2014

Balozi seif atembelea Kijiji cha Mvuleni Kidoti Wilaya ya Kaskazini “A “ Zanzibar



Balozi seif atembelea Kijiji cha Mvuleni Kidoti Wilaya ya Kaskazini "A " Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwahudumia Wananchi wake katika kuwapatia huduma muhimu na za msingi za Kijamii ikielewa fika kwamba inatekeleza Sera na ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo hapo katika Kijiji cha Mvuleni Kidoti Wilaya ya Kaskazini "A " wakati akikabidhi vifaa mbali mbali vya ujenzi kwa ajili ya kuufanyia matengenezo makubwa Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Kijiji hicho. 
Balozi Seif alikabidhi vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na Mabati,Miti na Papi za kuezekea, mbao,matofali, mawe, mchanga pamoja na saruji ikiwa ni awamu ya kwanza ya matengenezo hayo akianza kutekeleza ahadi aliyoitoa Tarehe 20 mwezi uliopita alipofanya ziara fupi kukagua maendeleo na changamoto zinazowakabili wananchi wa Kijiji hicho. 
Balozi Seif alisema Serikali inaelewa dhiki na matatizo ya Kiuchumi na Kijamii yanayowapata wananchi katika maeneo mbali mbali nchini. Hivyo katika kukabiliana na matatizo hayo Serikali itaendelea kuhudumia kadri hali itakavyoruhusu. 
Msimamizi wa matengenezo ya Msikiti huo wa Ijumaa wa Kijiji cha Mvuleni Bwana Khamis Yussuf Kombo kwa niaba ya waumini na wananchi wa kijiji hicho alimpongeza Balozi Seif kwa msimamo wake anaouchukuwa wa kusimamia harakati za kijamii hapa Nchini. 
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa tangi kubwa la kuhifadhia maji safi na salama liliopo katika Kijiji cha Mwanguo Bwereo litakalokuwa na uwezo wa kusambaza huduma ya maji katika Vijiji mbali mbali vilivyomo ndani ya Wilaya hiyo.
 Afisa wa Maji Wilaya ya Kaskazini "A" Ndugu Dude Kidongo Amour aliyepo kati kati akitoa maelezo Mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kuhusu ujenzi wa Tangi kubwa la kuhifadhia maji linalojengwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } liliopo katika Kijiji cha Mwanguo Bwereo.
 Balozi Seif akikamilisha kukagua tangi la kuhifadhia maji safi na salama la Mwanguo Bwereo litakalohudumia huduma hiyo kwa wananachi wa Vijiji mbali mbali vilivyomo ndani ya Wilaya ya Kaskazini "A ".
 Balozi Seif akibadilishana mawazo na Imamu Mkuu wa Msikiti wa Ijumaa wa Kijiji cha Mvuleni SheikhKhamis Duchi Kheir kabla ya kukabidhi vifaa mbali mbali kwa ajili ya matengenezo makubwa ya msikiti huo.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi Imamu wa Msikiti wa Ijumaa wa Mvuleni Sheikh Khamis Duchi Kheir vifaa mbali mbali vya ujenzi wa msikiti huo.
 Balozi Seif akiambatana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd. Haji Juma Haji wakielekeakuzungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mvuleni mara baada ya kukabidhi vifaa vya ujenzi wa msikiti wa Kijiji hicho.
 Balozi Seif akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mvuleni Kidoti mara baada ya kuanza kutekeleza ahadi yake aliyoitoa ya kusaidia matengenezo makubwa ya Msikiti wa Ijumaa wa Kijiji hicho. Kushoto ya Balozi ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd. Haji Juma Haji na Afisa Tawala wa Mkoa huo Dr. Makame Shauri. Picha na Hassan Issa wa OMPR, ZNZ.