Thursday, August 14, 2014

MWANASHERIA NA WAKILI MAARUFU MBEYA APANDISHWA KIZIMBANI.



MWANASHERIA NA WAKILI MAARUFU MBEYA APANDISHWA KIZIMBANI.
Picha na Rashid Mkwinda Blog
WAKILI wa kujitegemea mkoani Mbeya na mjumbe wa Mkutano mkuu wa CCM Taifa(MNEC) Sambwee Sitambala (42)amepandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu mkazi Mfawidhi wilaya ya Mbeya akituhumiwa kwa makosa mawili.
Shitambala amepandishwa leo akituhumiwa kwa makosa ya kuingia kwa jinai na kujenga nyumba katika viwanja viwili namba 27 na 28 Block BB lililopo eneo la Gombe Uyole Jijini Mbeya.
Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi, Gilbert Ndeuruo, wakili wa serikali, Ahmed Stambuli, alisema kuwa Shitambala anashitakiwa kwa kosa la kuingia kwa jinai kinyume cha kifungu  namba 79 ya mwaka 2014 cha kanuni ya adhabu sura ya 16.
Alisema kuwa mshitakiwa kwa nyakati tofauti kati ya Juni 18, 2012 na Novemba 28, 2013 aliingia na kujenga katika viwanja namba 27 na 28 ambavyo vinadaiwa kuwa ni mali ya raia wa Tanzania mwenye asili ya kiasia aliyefahamika kwa jina la Jaswinder Palsingh.
Alisema kulingana na mazingira hayo, mshitakiwa amesababisha maudhi kwa mmiliki wa kiwanja hicho Palsingh na hivyo kushitakiwa kwa kosa la jinai.
Shitambala ambaye alikuwa akitetewa na Wakili wa kujitegemea Tasco Luambano alikana shitaka hilo ambapo Hakimu Ndeuruo alisema kuwa dhamana ya Mshitakiwa iko wazi ikiwa atatimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja na ahadi ya fedha kiasi cha sh. milioni 1.
Kwa upande wake wakili wa serikali Stambuli alisema kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba iko tayari kuanza kusikilizwa na kuiomba mahakama ipange tarehe ya kuanza kuisikiliza kesi hiyo.
Hakimu Ndeuruo aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10 ambapo itaanza kusikilizwa rasmi.
Akizungumza nje ya mahakama mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo Wakili anayemtetea Shitambala,Luambano alisema kuwa kesi hiyo imefika hapo kutokana na maslahi ya baadhi ya watu na kuwa kisheria kesi za aina hiyo zinapaswa kusomwa katika mahakama ya Ardhi.

Alisema kuwa mteja amejenga katika eneo ambalo wamejenga watu wengine wapatao 400 na kuwa hata hivyo kesi hiyo imemhusu mteja wake pekee hali ambayo inaonesha nia mbaya iliyofanywa na mlalamikaji dhidi ya mteja wake.

Na  Mbeya yetu