Sunday, July 06, 2014

SOTE TUWAJIBIKE LINAPOKUJA SUALA LA UTAWALA BORA-TANZANIA


SOTE TUWAJIBIKE LINAPOKUJA SUALA LA UTAWALA BORA-TANZANIA
 Na Mwandishi Maalum, New York
Wakati mchakato wa maandalizi ya ajenda na malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015 ukiendelea kushika kasi kwa mijadala mbalimbali inayoendelea hapa Umoja wa Mataifa. Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa upande wake imesisitiza kuwa pamoja na kukubaliana kwamba suala la utawala bora ni muhimu katika utekelezaji wa maendeleo na kupiga vita umaskini, hata hivyo eneo hilo halipashwi kuwa la upande mmoja. 
 "Hoja ya utawala bora ni muhimu sana, ni muhimu sana katika uboreshaji na utoaji wa huduma za afya, elimu na hata upatikanaji wa nishati endelevu kwa watu wetu.Lakini utawala bora hauwezi kuelekezwa au kuwa ni hoja ya nchi moja moja au kanda, bali ni hoja inayokwenda mbali zaidi, utawala bora unatuhusu sote hadi katika ngazi ya kimataifa sote tunapashwa kuwajibika katika eneo hili" akasema Balozi Tuvako Manongi.
Moja ya eneo ambalo alilitolea mfano kama linalohitaji uwajibikaji wa pamoja inapokuja hoja ya utawala bora ni eneo la fedha haramu au kwa maneno mengine utoroshwaji wa fedha kutoka nchi zinazoendelea na kwenda kufichwa nje.
 Akisema ufumbuzi wa tatizo hilo ambalo kwa namna moja ama nyingine lina changia katika ukwamishaji wa maendeleo linahitaji ushirikiano wa pamoja. Muwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, ameyasema hayo mwisho wa mkutano wa siku nne wa Kilele wa Kisiasa ulioadaliwa na Baraza Kuu la Uchumi na Maendeleo la Umoja wa Mataifa ( ECOSOC) na kuwashirikisha nchi wanachama, wanazuoni , wawakilishi wa makundi maalum pamoja na Asasi zisizokuwa za kiserikali. 
Mkutano huo wa siku nne, ulijadili mada mbalimbali lakini zote zikijikita katika mihimili mikuu mitatu inayosimamia maendeleo endelevu kama yalivyoainishwa katika Mkutano wa Kimataifa wa RIO+20 uliofanyika nchini Brazili. Maeneo hayo na ambayo yanatakiwa kutekelezwa sambamba ni maendeleo ya Kijamii, maendeleo ya Kiuchumi na Mazingira.
Pamoja na kuzungumzia hoja ya utawala bora, Balozi Tuvako Manongi pia amesema majadiliano ya DOHA kuhusu fursa za biashara kwa nchi zinazoendelea yapashwa kukamilishwa.
 Kwa kile alichosema majadiliano ya DOHA ni kiungo muhimu katika utekelezaji wa Maendeleo endelevu baada ya 2015.
 " Biashara ni muhimu sana katika maendeleo, na kwa sababu ya umuhimu wake, ujumbe wangu ungependa kusisitiza kwamba majadiliano ya DOHA yanapashwa kukamilishwa kama ilivyoahidiwa huko Bali, Indonesia. Kuhusu nafasi ya sekta binafsi katika kuchagiza maendeleo, Balozi Manongi alisema, akiongezea kuwa sekta binafsi inatakiwa kuwezeshwa kwa kuundiwa sera na mazingira ambayo itaiwezesha kukua , kuimarika na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuchangia utekelezaji wa maendeleo na kupanua wigo wa ajira. 
Kuhusu mchakato mzima wa maandalizi ya agenda mpya za maendeleo na malengo yake, Muwakilishi huyo wa Tanzania, alitahadharisha kuwa, agenda hizo na malengo yake, ni lazima yazingatie hali halisi ya kila nchi, uwezo wake na utayari wa kuyatekeleza, kipi kinahitaji na kipi haikihitaji. Kwa kile alichosema nchi hazifanani ,ni tofauti na hata katika kiwango cha umaskini zinatofuatiana.
  Ujumbe  kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,  Bw. Ahmed Makame Haji wa Tume ya Mipango  na Bihindi Nassor Khatib Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha wakifuatilia majadiliano kuhusu maendeleo endelevu.
Sehemu ya  washiriki wa  Mkutano wa Kilele wa Kisiasa wa siku nne  uliofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ukiwashirikisha wajumbe kutoka mataifa mbalimbali,  wanazuoni,wataalamu wa kada mbalimbali,  makundi maalum na Asasi zisizo za kiserikali.
Muwakilishi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi akichangia wakati wa Mkutano wa siku nne wa Kilele wa Kisiasa uliokuwa ukijadili mada mbalimbali zinazohusiana na  masuala ya maendeleo endelevu. Mkutano huo  uliandaliwa na Baraza Kuu la  Uchumi na  Maendeleo la Umoja wa Mataifa 9 ECOSOC). katika ujumbe wake Balozi aliyeongoza ujumbe wa Tanzania katika  mkutano huo, aliikumbusha  jumuiya ya kimataifa kuwa   suala la utawala bora  ni jumuishi ambapo jumuiya  ya kimataifa pia inahusika nalo. Nyuma ya  Balozi ni Bi Amina Shaaban Mkurugenzi  Mtendaji,  Tume ya Mipango Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.