ZAIDI ya watu 60 wenye uhitaji wamewezeshwa na asasi isiyo ya kiserikali ya Ladies Circle International katika mahitaji mbalimbali ikiwemo elimu, matibabu ,malazi pamoja na mitaji .
Hayo yalisemwa na Rais wa asasi hiyo hapa Tanzania ,Julieth Anthony wakati akizungumza katika uzinduzi rasmi wa asasi hiyo uliofanyika mjini hapa hivi karibuni.
Alisema kuwa , asasi hiyo ilianza kufanya kazi hapa nchini mwaka 2012 ambapo ina jumla ya matawi matatu kwa nchi nzima ,huku asasi hiyo ikiwa kwenye nchi 37 hapa duniani.
Alisema kuwa, lengo hasa la kuanzishwa kwa asasi hiyo ni kuhamasisha wanawake kuwa na moyo wa kujitolea kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii, kusaidia kuhimiza elimu na masomo ya sayansi kwa watoto wa kike wakiwemo yatima .
Aidha lengo lingine ni kuboresha huduma ya mama na mtoto ili kuzuia kifo cha mama na mtoto ,na kuendeleza ujasirimali kwa vijana wanawake pamoja na kufadhili elimu kwa watoto yatima na kuwapatia mahitaji yao.
Julieth alisema kuwa, kuwepo kwa asasi hiyo hapa nchini ambayo inaundwa na wanawake wenyewe kutasaidia sana kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii hususani zinazowakabili wanawake na watoto wa kike kwa ujumla.
Naye Katibu Mkuu wa shirika la Love for all people Tanzania na Mratibu wa uanzishwaji wa asasi hiyo, Anthony Musani alisema kuwa,kuanzishwa kwa asasi hiyo hapa nchini ni baada ya kutembelea nchi za nje na kukuta wakiwa na asasi hiyo ambayo wamekuwa wakisaidia jamii zenye uhitaji ndipo alipoguswa na kuomba kuanzishwa hapa nchini .
Musani alisema kuwa,watu wengi wana uwezo mkubwa sana wa kusaidia jamii zenye uhitaji ila changamoto kubwa inakuja katika kupata wawezeshwaji wa miradi ama vikundi vyao watakavyoanzisha.
Aidha Musani aliwataka wadau mbalimbali wa maendeleo nchini kuhakikisha wanaitumia asasi hiyo ipasavyo kwa kusaidia jamii mbalimbali zenye uhitaji wakiwemo wajane, yatima na hata wenye mahitaji maalumu.
Naye Mgeni rasmi katika uzinduzi huyo,Mbunge wa bunge maalumu la katiba, Yasmin Aloo aliunga mkono uanzishwaji wa asasi hiyo sambamba na kuanzisha mfuko wa kuwezesha asasi hiyo ili kuendeleza mipango yake ya kusaidia jamii.
Aidha aliitaka asasi hiyo kutumia chombo hicho kwa malengo yaliyowekwa ikiwemo kuanzisha kituo cha afya kijiji cha ndani mkoani Dodoma na kuanzisha kituo cha ushauri nasaha na mafunzo ya ufundi kwa watoto wa mitaani waliotelekezwa baada ya kupata mimba katika umri mdogo mkoani Arusha.
Rais wa asasi ya Ladies circle kwa hapa Tanzania ,Julieth Anthony akizungumza katika uzinduzi rasmi wa asasi hiyo uliofanyika jijini Arusha katika hotel ya Naura springs.