Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi ya Finland imeanzisha Programu ya'Panda Miti Kibishara' (Private Forestry Programme). Programu hiyo yenye makao makuu Njombe inayo madhumuni ya kuwahamasisha wananchi kupanda miti kwa kuzingatia kuwa miti ni zao la biashara.
Ingawaje Programu hiyo imeshiriki kwa mara ya kwanza katika maonyesho ya Sabasaba ilikuwa kati ya sehemu zilizowavutia watu wengi ndani banda la Maliasili na Utalii. Wananchi walotembelea waliuliza maswali kuhususiana na aina za miti ya mbao inayofaa kupandwa katika sehemu zao na upatikanaji wake.
Programu ya Panda Miti Kibiashara inatekelezwa katika wilaya sita za Ludewa, Makete, Njombe, Kilolo, Mufindi na Kilombero. Programu hii ni ya miaka 16 lakini itatekelezwa kwa awamu za miaka minne kila moja.
Lengo la Programu hiyo ni kuongeza kipato cha wananchi waishio vijijini kwa kupanda miti. Lengo hilo litafanikiwa kama wananchi watalima mashamba ya miti kitaalam kwa kuzingatia matumizi ya mbegu bora na kulihudumia shamba kitaalam ili mazao yatakayopatikana yaweze kuvutia soko la ndani na nje.
Lengo jingine ni kuanzisha shughuli ya kujiongezea kipato nje ya shamba la miti wakati wahusika wakisubiri miti ifikie umri wa kuvunwa. Shughuli hizo ni kama vile kilimo cha matunda na ufugaji nyuki. Aidha wananchi wamehimizwa kuunda vikundi vya Wakulima wa Miti ili iwe rahisi kwa Programu kutoa msaada kwao.
Kwa sasa miche ambayo itapandwa na wananchi walioko katika wilaya zinazohudumiwa na Programu inakuzwa kwenye vitalu ili iwe tayari kupandwa mwezi Desemba mwaka huu na Januari mwakani.
Programu imeazimia kuwa katika kipindi cha awamu ya kwanza ya Programu (mwaka 2014 hadi 2017) jumla ya hekta 15,000 zitapandwa na wananchi waliojiunga na Vikundi vya Wakulima wa Miti.