Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewakumbusha wagonjwa na wafiwa kuwa na subra na uvumilivu, wakielewa kuwa hiyo ni mitihani ya Mwenyezi Mungu.
Akiwa katika ziara ya kutembelea wagonjwa na wafiwa katika Wilaya ya Mkoani, Maalim Seif amesema maradhi ni jumla ya mitihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kwamba wanaopatwa na mitihani hiyo hawana budi kushuru na kuomba dua.
Maalim Seif ambaye yuko kisiwani Pemba kwa ziara ya siku sita ya kuangalia wagonjwa, kutembelea masoko na kufutarisha, amewataka wananchi kuendeleza umoja na mshikamano uliopo kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.
Hapo jana Maalim Seif alifutari pamoja na wananchi wa kijiji cha Piki katika Wilaya ya Wete, na kuwashukuru wananchi wa kijiji hicho kwa kujitokeza kwa wingi kuungana nae katika futari hiyo.
Wananchi hao wameelezea shukrani zao kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa kuamua kufutari pamoja nao, kitendo ambacho wamesema kimeongeza upendo kati yao na viongozi wakuu wa Serikali.
Mapema wagonjwa waliotembelewa wameelezea kufarajika kwao kutokana na kitendo hicho, na kwamba kinaleta picha halisi kwa viongozi kuwajali wananchi wao katika mazingira yote.
Katika ziara hiyo ya Wilaya ya Mkoani, Maalim Seif amewatembelea na kuwafariji wagonjwa wanane pamoja na wafiwa katika vijiji mbali mbali vikiwemo Chambani, Mwambe, Mtambile, Uweleni na Chokocho.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akitembelea na kuwafariji wagonjwa na wafiwa katika Wilaya ya Mkoani Pemba.
Picha na Salmin Said, OMKR
Maalim Seif akiwafariji wagonjwa na wafiwa katika Wilaya ya Mkoani Pemba.
Maalim Seif akiwafariji wagonjwa na wafiwa katika Wilaya ya Mkoani Pemba.