MAKOSA mawili yaliyofanywa na wachezaji wazoefu Sergio Ramos na Xabi Alonso yameigharimu Real Madrid na kupelekea kipigo cha 2-0 kutoka kwa Celta Vigo.
Real Madrid sasa imejivua rasmi nafasi ya kutwaa ubingwa wa La Liga kwani hata ikishinda mchezo wake wa mwisho haitaifikia Atletico Madrid.
Ili kutwaa ubingwa, Real Madrid ilikuwa inaombea Atletico Madrid na Barcelona wateleze, jambo ambalo lilitokea lakini bado wakashindwa kuutumia mwanya huo.
Barcelona imetoka sare ya 0-0 na Elche, huku Atletico Madrid nayo ikalazimishwa sare ya 1-1 na Malaga.
Huku kila timu ikiwa imebakiza mechi moja, Atletico Madrid wanaongoza kwa pointi 89, Barcelona wanafutia kwa pointi 86 huku Real Madrid wakikamata nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 84.
Sergio Ramos na Xabi Alonso walishindwa kudhibiti nyendo zao walipokuwa na mpira, Charles akatumia makosa yao kupachika mabao mawili katika dakika za 43 na 64.
Barcelona wataikaribisha Atletico Madrid katika mechi ya mwisho wikiendi ijayo, mchezo utakaoamua nani bingwa wa La Liga.
Atletico ni kama fungu la kukosa vile kwani kama wangeichapa Malaga basi tayari muda huu wangekuwa ni mabingwa wapya wa La Liga.
Atletico wanahitaji sare tu kutwaa ubingwa, lakini wakiruhusu kipigo kutoka kwa Barcelona, ndoto yao ya kusubiri kutwaa taji kwa miaka 18 itakuwa imezimwa.
Kama Barcelona watashinda, timu hizo zitalingana pointi na kwa mujibu wa kanuni za La Liga, wataangalia nani mbabe kwa mwezanke (head to head) katika mchezo wao wa kwanza ambao uliisha kwa sare ya 0-0 hivyo moja kwa moja Barcelona atakuwa bingwa.
Historia inaipa Barcelona nafasi nzuri ya kushinda mchezo huo. Hebu tazama matokeo ya mechi zao tano za mwisho walizokutana kwenye La Liga:
11 Jan 2014: Atletico 0-0 Barca
12 May 2013: Atletico 1-2 Barca
16 Dec 2012 : Barca 4-1 Atletico
26 Feb 2012: Atletico 1-2 Barca
24 Sept 2011: Barca 5-0 Atletico