Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP ) ametaja ushirikiano wa vyama vitatu vinavyounda kambi rasmi ya upinzani bungeni kwamba ni ndoa ambayo kama wahusika wangekuwa na nia njema, ungeanza siku nyingi tangu Chadema kilipounda baraza lake mwaka 2010. Mwanasiasa huyo ambaye ameunga mkono kauli ya Spika Anne Makinda, kwamba kambi hiyo rasmi ya upinzani imekumbuka shuka kunakucha, amekiri kwamba haelekei na wala hapatani na wana Ukawa; lakini yeye ni mpinzani na mzalendo wa kweli nchini. Mrema alisema hayo mjini hapa akizungumza na mwandishi wa habari hizi. Alimjibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe ambaye katika kutangaza Baraza Kivuli la Mawaziri juzi, alisema mbunge huyo hana dhamira ya kuwa mshirika wa Ukawa na alishaweka wazi kuwa mshirika wa CCM.
Alitaja ushirikiano huo wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, kuwa ni 'ndoa' anayoiombea kila la heri na hawezi kuibashiria mabaya, isipokuwa anachoona ni kwamba kama wangekuwa na nia njema, ndoa hiyo ingeanza siku nyingi tangu Chadema ilipounda baraza mwaka 2010.
"Ushirikiano huu ni jambo lao, wanafikiri litawasaidia. Lakini kwani hatujui walivyokuwa (CUF na Chadema) wakitukanana? Siwezi kuwabashiria mabaya. Wangelikuwa wema, hiyo ndoa ingeanza siku nyingi," alisema Mrema.
Alisema yeye ni mpinzani ambaye kamwe hawezi kushiriki katika mambo ya kubomoa nchi.
"Kwanza mimi sijaomba huo uwaziri kivuli. Hawa watu ni wa ajabu sana... Mbona Maalim Seif (Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Katibu Mkuu wa CUF), yuko kwenye Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar. Mbona CUF hawaambiwi ni CCM?
"Kwanza ukinilinganisha na wao, naona wananionea wivu. Nimeshika madaraka ambayo hawajawahi kuyashika. Mbowe hana sifa za kuniteua. Ana sifa ipi sasa?."
Mrema alitamba kuhusu nafasi za uongozi serikalini alizowahi kushika, ikiwemo ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana na Naibu Waziri Mkuu.
Alisema licha ya kuwa miongoni mwa watumishi waliotukuka, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 akiwa NCCR Mageuzi, alipata kura milioni 1.8 ambazo kwa mujibu wake, hakuna mpinzani anayeweza kuzipata. "Na nilikuwa NCCR Mageuzi. Si watu wangenikataa kuwa mimi ni CCM…Nani amewahi kuvunja rekodi hii ya kura?" Alihoji.
Akiendelea kutamba kwamba hatishiwi na cheo chochote, alisema aliamua kuachana na kile alichoita 'biashara ya jumla' akimaanisha kugombea urais na badala yake, akaingia kwenye 'biashara ya reja reja' kwa maana ya ubunge.
Alisisitiza, "mtu aliyewahi kugombea urais, leo hii unanipa uwaziri kivuli, si badala yake watanipa uwaziri giza?." Hata hivyo alisema kuachwa katika baraza hilo kivuli, si suala la kushangaa, kwani hata walipoliunda mara ya kwanza na kuwabagua CUF, pia yeye hakuwemo.
Akielezea mgogoro kati yake na Upinzani, Mrema alisema umekuwa mkubwa katika Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na kutokukubaliana nao katika mtazamo juu ya muundo wa Muungano.
Alisema katika Bunge Maalumu, wabunge walikubali kutengeneza utaratibu endapo itatokea kutoelewana. Alisema ipo Kamati ya Maridhiano ambayo iliundwa kuwezesha wabunge kuzungumza na kupatana pale itakapotokea hali hiyo.
Licha ya Kamati ya Maridhiano, alisema upo uongozi wa Bunge la Katiba naisitoshe, suala lolote linalohusu bunge hilo, linapaswa lizungumzwe ndani ya bunge hilo limalizike.
"Sasa wenzangu wakaamua kutoka nje mimi sikutoka nje. Ndio naonekana eti mimi ni CCM. Eti niende Kibanda Maiti (Zanzibar); hivi niking'atwa na nyoka Kibanda Maiti, nitawaambiaje wananchi wangu? Nilikuwa wapi na nilikwenda kufanya nini