MSHAMBULIAJI Gonzalo Higuain amefunga bao lake la kwanza katika michuano ya kombe la dunia inayoendelea nchini Brazil, bao pekee lililoipa ushindi Argentina dhidi ya Ubelgiji kwenye mchezo mkali wa robo fainali.
Kwa kushinda 1-0, Argentina imetinga nusu fainali ambapo itakumbana na mshindi kati ya Holland na Costa Rica.
Mashabiki elfu 20 wa Argentina waliojazana kwenye Uwanja wa Taifa mjini Brasilia, walikuwa wakishangilia kwa nguvu huku wakipunga jezi zao juu ya vichwa vyao.
Walikuwa wakiimba huku wakiwapiga vijembe watani wao wa jadi, Brazil na kuwakumbushia namna Claudio Caniggia alivyowatungua mwaka 1990.
Lakini kama hiyo haitoshi, mashabiki wao wakawa wanawakejeli wenyeji wa kombe la dunia kuwa Messi ni bora kuliko Pele.
Upo uwezekano mkubwa wa mahasimu hao kukutana kwenye hatua ya fainali, lakini Brazil watakuwa bila mshambuliaji wao tegemeo Neymar aliyeumia kwenye mechi dhini ya Colombia.
Higuan alifunga bao hilo dakika ya 8 kwa mpira ulioanzia kwa Lionel Messi aliyemsogezea Di Maria aliyetoa pasi kwa mfungaji.
Licha ya kwamba Messi hakufunga katika mchezo huo, lakini alionyesha kiwango cha juu na kuwa tishio kwa safu ya ulinzi ya Ubelgiji.
Kiungo shambuliaji tegemeo wa Ubelgiji, Eden Hazard hakuwa na siku nzuri ambapo alishindwa kung'ara na aliishia kutolewa dakika ya 75 na nafasi yake kuchukuliwa na Chadli.
Argentina: Romero, Zabaleta, Demichelis, Garay, Basanta, Biglia, Mascherano, Lavezzi (Palacio 71), Messi, Di Maria (Perez 33), Higuain (Gago 81).
Belgium: Courtois, Alderweireld, Van Buyten, Kompany, Vertonghen, Fellaini, Witsel, Mirallas (Mertens 59), De Bruyne, Hazard (Chadli 75), Origi (Lukaku 59).