Na Sultani Kipingo
Bao la dakika ya nane lililowekwa kimiani na mshambuliaji wa Napoli Gonzalo Higuain lilitosha kuipeleka Argentina kwenye nusu fainali za Kombe la Dunia walipocheza dhidi ya Ubelgiji ambayo ilishindwa kabisa kuonesha cheche zake leo jijini Brasilia.
Higuain alitumia vyema kosa la kizembe la nahodha wa Ubelgiji Vincent Kompany kuipaisha Argentina kwa jaribio lao la kwanza kwenye goli la adui.
Kompany aliupoteza mpira na Lionel Messi akauzima kabla ya kumtilia pande Angel Di Maria upande wa kulia, na nyota huyo wa Real Madrid alibahatika pale pasi yake ilipomgonga beki wa Ubelgiji Jan Vertonghen, na mpira ukajipeleka mbele ya Higuain ambaye hakufanya makosa. Pichani Di Maria na Higuian wakimshukuru Messi ambaye pande lake lilizaa goli lao.