Na. Ally Mataula na Rocky Setembo.
Wananchi wamehimizwa kutembelea banda la Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Wito huo umetolewa na Afisa wa Maadili Mwandamizi Bw. Bazilio Mwanakatwe wakati akizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea banda la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika maonesho hayo.
Bw. Mwanakatwe aliendelea kubainisha kuwa lengo kubwa la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kushiriki maonesho hayo ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu na mamlaka ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili nao waweze kufahamu wajibu wao katika jukumu zito la kujenga na kuimarisha Maadili ya Viongozi nchini.
"Suala la maadili ni mtambuka ambalo linahusisha kila Nyanja katika jamii hivyo usimamizi wake na ukuzaji wake unahitaji ushirikiano wa taasisi zote za umma, sekta binafsi, asasi za kiraia pamoja na jamii kwa jumla. Serikali peke yake haiwezi kufikia lengo lililokusudiwa hivyo inahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa umma" alifafanua Bw. Mwanakatwe.
Pamoja na kutoa elimu katika maonesho hayo, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatoa huduma nyingine kama vile kupokea malalamiko moja kwa moja kutoka kwa wananchi yanayohusu ukiukwaji wa Maadili ya Viongozi Umma.
Afisa toka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Bazilio Mwanakatwe akielezea jambo alipokuwa akihojiwa na Mwandishi wa Habari katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Maafisa wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakitoa elimu katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, yanayoendelea hivi sasa kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es salaam.
Aliyekuwa Kamishna wa pili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji (Mst) Steven Ihema, akiuliza swali alipotembelea Banda la Maadili, katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es saam.