Katika toleo Na. 1734 la gazeti la Jambo Leo la tarehe 10 Juni, 2014 katika ukurasa wa tatu iliandikwa taarifa iliyokuwa na kichwa cha habari "Utafiti wa gesi kuinufaisha Morogoro, Kilimanjaro". Taarifa hiyo ilieleza kuwa wakaazi wa mikoa tajwa watanufaika na ugunduzi wa mafuta na gesi uliofanywa na Kampuni ya Swala katika maeneo hayo.
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) linapenda kuwafahamisha wananchi kuwa taarifa ya kwamba Kampuni ya Swala imegundua gesi na mafuta katika maeneo ya Morogoro na Kilimanjaro sio sahihi. Ugunduzi wa mafuta hufanyika tu baada ya kuchimba kisima cha utafiti na hatimaye mafuta au gesi iweze kutoka yenyewe kutoka ardhini.
Hatua ya kuchimba kisima cha utafutaji hutokana na tafiti mbali mbali za awali za mitetemo ya ardhi na kubaini kama maeneo hayo yana uwezekano wa kuwa na mafuta au gesi ama la. Hata kama eneo linaonesha dalili nzuri za awali ni lazima sehemu hiyo ichimbwe na matokeo
yake ni kuwa na ugunduzi au la. Vilevile ugunduzi huo lazima uonyeshe kutoa kiasi cha rasilimali ambacho kinaweza kuzalishwa kibiashara (economically viable).
Kazi zilizofanyika mpaka sasa na Kampuni ya Swala katika maeneo ya Morogoro – Kilosa na Pangani - Kilimanjaro ni utafiti wa awali wa kukusanya takwimu za mitetemo na kubaini kama maeneo hayo yana kina (thickness) cha kutosha cha miamba tabaka ambayo utafiti wa mafuta na gesi unaweza kufanyika. Hivyo utafiti wa kina unaendelea ili kubaini kama kuna miamba mashapo (prospects) ya kutosha kwa ajili ya kuchimba kisima cha utafiti. Uchimbaji wa kisima hicho unaweza kutoa mafuta au/na gesi au maji matupu. Hatua ya uchimbaji visima bado haijaanza.Hivyo basi si sahihi kwa mtu yeyote kusema kuwa kuna ugunduzi uliofanyika.
Utaratibu wa kutafuta mafuta nchini ni wa kugawana mapato kati ya Mwekezaji na Serikali kupitia Mikataba ya Kugawana Mapato (Production Sharing Agreement-PSA) kama mafuta au gesi ikigundulika. Kampuni isipogundua rasilimali yeyote, Serikali haimrudishii Mwekezaji fedha zake alizowekeza kwenye ufafiti huo, hivyo hasara hiyo ni kwa Mwekezaji mwenyewe.
Shirika lina taarifa kuwa Kampuni ya Swala inauza Hisa zake katika soko la Hisa la Dar es Salaam ili Watanzania washiriki katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi. Suala hili ni jema na Kampuni ya Swala inastahili kupongezwa kwa kuwawezesha Watanzania kushiriki kwenye sekta hii ambayo imeshika kasi katika miaka mitatu iliyopita. Aidha, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania linawashauri Wananchi wafanye maamuzi mazuri na kuwatumia washauri wao kuhusu ununuzi wa hisa hizo kwa kuzingatia mambo yaliyoelezwa hapo juu.
Ikumbukwe kuwa Tanzania tumechimba visima vya utafiti wa mafuta vipatavyo 78 na vyenye gesi ni asilimia 40% tu huko Mkuranga (Pwani), Songosongo (Lindi), Ntorya na Mnazi Bay (Mtwara) na Bahari ya kina kirefu.
Taarifa kuwa katika mikoa ya Morogoro na Kilimanjaro kumefanyika ugunduzi wa mafuta na gesi haina ukweli wowote. Kama rasilimali ya mafuta au gesi asilia ikigundulika mwenye mamlaka ya kutangaza ugunduzi huo ni Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini pekee.
Kwa maelezo zaidi wasiliana na: -
Mkurugenzi Mtendaji,
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania,
BWM Tower A,
S.L.P 2774,
Dar es Salaam.
Barua pepe: tpdcmd@tpdc-tz.com