Friday, June 20, 2014

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yawasaidia Wavuvi wa Kijiji cha Kivunge



Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yawasaidia Wavuvi wa Kijiji cha Kivunge
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa shilingi Milioni Nne ikiwa ni nusu malipo ya gharama ya shilingi milioni Nane ilizoahidi kutoa kwa ununuzi wa Mashua kwa ajili ya kufidia chombo cha Wavuvi wa Kijiji cha Kivunge kilichochomwa moto mwezi Januri mwaka huu wa 2014 katika Kisiwa cha Tumbatu.

Ikasisitiza tena na kuonya kwamba hilo litakuwa ni tukio la mwisho kubebwa na Serikali la kulipa fidia kwa migogoro yoyote itakayosababishwa na wana jamii katika maeneo mbali mbali kutokana na hitilafu wanazoweza kuzikabili wana jamii wenyewe.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akikabidhi fedha hizo kwa mdhamini wa ujenzi wa Mashua hiyo Bwana Ali Makame Madaha { Cheupe } hafla iliyofanyika pembezoni mwa bahari ya Nungwi ilipochongwa mashua hiyo Mkoa wa Kaskazini Ungua.

Akipokea fedha hizo mdhamini wa ujenzi wa chombo hicho cha uvuvi ambae pia ni Katibu wa Kamati Tendaji ya hifadhi ya Mnemba na Chwaka Bwana Ali Makame Madaha { Cheupe } alitahadharisha kwamba ongezeko la wavuvi katika baadhi ya sehemu hapa nchini ndio sababu kuu inayoleta migogoro ya uvuvi kwenye maeneo mbali mbali ya bahari.

Akikabidhi rasmi chocho hicho kwa wavuvi wa Kijiji cha Kivunge na kushuhudia pia na Uongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa wa Mkoa wa kaskazini Unguja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliendelea kuwaasa Wananchi kwamba Serikali kamwe haitakuwa tayari kubeba dhamana ya kulipa fidia ya mali au vyombo watakavyoharibiana kwenye migogoro wanayoweza kuiepuka.

Chombo hicho cha uvuvi walichokabidhiwa wavuvi wa kijiji cha kivunge kina uwezo wa kuchukuwa watu kwenda katika shughuli zao za uvuvi kati ya ishirini na ishirini na tano kwa wakati mmoja.
Balozi Seif akimkabishi rasmi mashua iliyopewa jina Riziki zina Mungu Bwana Dhamiri Makame Juma wa Kijiji cha Kivunge iliyotengenezwa katika Kijiji cha Nungwi.
Mdhamini wa ujenzi wa Mshua ya Riziki zina Mungu Bwana Ali Makame Madaha { Cheupe } alitia saini hati ya kuuza mashua hiyo akishuhudiwa na Balozi Seif kwa ajili ya kupewa wavuvi wa Kivunge.
Balozi Seif ahesabu nusu ya fedha zilizoahidiwa kutolewa na serikali Milioni Nne { 4,000,000/- } kulipia fidia kutokana na mashua ya wananchi wa Kivunge kuchomwa moto katika kisiwa cha Tumbatu.
Mashua ya Riziki zina mola iliyonunuliwa na Serikali kulipwa fidia wavuvi wa Kijiji cha kivunge kufuatiwa mashua yao kuchomwa moto katika kisiwa cha Tumbatu.Picha na Hassan Issa wa – OMPR - ZNZ