Friday, June 13, 2014

BONDIA IRAQ HUDU "KIMBUNGA" AFARIKI DUNIA


BONDIA IRAQ HUDU "KIMBUNGA" AFARIKI DUNIA
BONDIA IRAQ HUDU

Na Asha Said

BONDIA wa zamani wa ngumi za kulipwa nchini, Iraq Hudu 'Kimbunga'  amefariki dunia jana mjini Dar es Salaam akiwa ana umri wa miaka 49, baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Akizungumza Dar es Salaam leo, dada wa marehemu Tiba Takadir, amesema kwamba Hudu amefariki jana majira ya saa 11 ya alfajiri kwenye hospitali ya Hindu Mandal, alikokuwa amelazwa. Takadir, alimesema kuwa mazishi ya Hudu yatafanyika kesho Jumamosi kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Alisema kuwa marehemu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la ini na figo kutofanya kazi, ambapo vilimsumbua kwa muda mchache kabla ya kufariki kwake.

"Marehemu alilazwa hospitali Hindu Mandal siku tatu zilizopita, ambapo majuzi jioni alizidiwa na jana asubuhi kukutwa na umauti.

Hudu amezaliwa mwaka 1965 Ujiji Kigoma, na kupata elimu ya msingi mkoani humo na baadae kuja Dar es Salaam ambapo alimaliza shule ya Sekondari na baadae kuanza shughuli za ngumi katika miaka ya 1990 mpaka miaka ya 2000 alipoacha.

Marehemu ameacha watoto watatu, ambao ni Daniel alikuwa akitarajia kufunga ndoa Juni 20, wakati mtoto mwingine Msawila ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita. 

Maandalizi ya msiba yanaendelea nyumbani kwa marehemu Buguruni Lozana Dar es Salaam ambapo kesho saa 7, atazikwa Kisutu.