Friday, June 27, 2014

ATCL yasaini mkataba kushirikiana na Interair




ATCL yasaini mkataba kushirikiana na Interair
 Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lazaro (katikati) akipeana mkono na  Meneja wa Kanda wa Interair, Angelo Cossi  mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya makubaliano yaliyosainiwa kati ya shirika la ATCL na shirika la Interair la Afrika ya Kusini, yatakayowezesha kuwepo na safari tatu kwa wiki kati ya Dar es Salaam na Johannesburg Afrika ya Kusini. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa ATCL Bw. Juma Boma (kushoto). . 
 Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lazaro (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam jana kutangaza makubaliano yaliyosainiwa kati ya shirika lake na shirika la Interair la Afrika ya Kusini, yatakayowezesha kuwepo na safari tatu kwa wiki kati ya Dar es Salaam na Johannesburg Afrika ya Kusini. Wakishuhudia kushuto ni Meneja wa Kanda wa Interair, Angelo Cossi na Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa ATCL Bw. Juma Boma (kushoto)

=======  ====== ========
SHIRIKA la Ndege la Taifa la Air Tanzania (ATCL) limesaini mkataba wa ushirikiano na kampuni ya Interair ya Afrika Kusini, itakayowezesha shirika hilo kuwa na safari tatu kwa wiki kati ya Dar es Salaam na Johannesburg, Afrika ya Kusini ikiwa ni kama ratiba ya mwanzo.

Taarifa hiyo imetolewa siku chache tu baada ya mashirika hayo mawili kusaini makubaliano ya kufungua soko la kitanzania kwa Interair na kulifufua soko la Afrika ya Kusini kwa shirika la Ndege la Air Tanzania kwa kupitia safari zitakazofanyika siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa, ikiwezeshwa na ushirikiano huo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya ATCL jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa ATCL, Kapteni Milton Lazaro alisema ushirikiano huo na Interair ni sehemu ya mkakati madhubuti wa kuboresha shirika hilo, kama siyo kwa safari za moja kwa moja basi kupitia ushirikiano wa aina hiyo, ili kuweza kurejesha huduma za shirika hilo katika njia zote lililokuwa likiruka, likianzia Afrika ya Kusini.  

"Kwa kutumia ndege za Interair, abiria wetu sasa watakuwa na uwezo wa kusafiri kwenda na kutoka Johannesburg katika siku zifuatazo; itawasili jijini Dar es Salaam kila Jumatatu na kuondoka kwenda Johannesburg Jumanne, kuwasili Dar es Salaam Jumatano na kuondoka siku hiyo hiyo, kuwasili Dar es Salaam Ijumaa na kuondoka kwenda Johannesburg siku ya Jumamosi," alisema.

Kapt. Lazaro alibainisha kuwa mashirika hayo mawili sasa yanatoa fursa kwa wasafiri kutoka nchi hizo mbili kuyafikia masoko, wanaotaka kutumia na kupata uzoefu wa siku kuu za kipekee wanazo kuwa wakizisoma kuhusu Afrika ya Kusini au Tanzania, na pia kutoa fursa za ongezeko la ushirikiano wa kibiashara na kidiplomasia.

"Kwa kupitia makubaliano haya mapya, tuna uhakika kuwa ratiba itakidhi haja kwa wasafiri wote katika sehemu hizi mbili, na kutoa chanzo cha mapato kitakacho changia katika ukuaji wa shirika la Air Tanzania, Sekta ya Utalii Tanzania na uchumi wetu wa ndani," alisema Kapt. Lazaro. Aliongeza kuwa ATCL katika siku za usoni itatanua safari zake mpaka Arusha, Zanzibar, Mwanza, Mbeya, Comoros na baadae katika maeneo mengine yote inayofanyia shughuli zake. 

Kwa upande wake, Meneja Interair wa Kanda ya Afrika Mashariki, Bw. Angelo Cossi, alisema: "Ushirikiano na Air Tanzania ni muungano nzuri kwa sababu ya faida itakayopatikana ambayo itafaidisha mashirika haya mawili. 

"Shirika la Interair la Afrika ya Kusini ni moja kati ya mashirika ya ndege nchini Afrika ya Kusini yanayomilikiwa kibinafsi yenye mafanikio. Shiriki hili, mwanachama wa Chama cha Kimataifa cha Usafiri wa Anga (I.A.T.A), na Chama cha Mashirika ya Ndege Afrika (AFRAA) limejiimarisha kama moja kati ya mashirika makubwa katika ukanda. Ushirikiano na Air Tanzania utawapatia wateja wa Interair, njia mpya bora ya kusafiri kwenda Tanzania na kutoka Tanzania, Johannesburg inakuwa karibu zaidi na ni ya rahisi kufika kwa wateja wa Air Tanzania," alisema.

Alisema Interair ya Afrika ya Kusini ambayo ina makao yake makuu Johannesburg, Afrika ya Kusini, kwa sasa ina ndege aina za Boeing 727, 737 na 767, ambazo zinatoa huduma ndani ya Afrika na katika visiwa vya Bahari ya Indi. Alikuwa na matarajio kwamba ushirikiano huo utausaidia shirika lake kutengeneza jina thabiti katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.