WATOTO wanaoishi kwenye mazingira hararishi na wasiokuwa na wazazi wa kuwasomesha mkoani Mbeya, wamepatiwa msaada wa vifaa na kulipiwa ada ya shule, hali itakayowezesha wanafunzi wapatao 3,500 kuendelea na masomo.
Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya sh milioni 95 ulitolewa jana na Shirika lisilokuwa la kiserikali lenye kutoa huduma za kijamii la mkoani hapa, KIHUMBE kwa kushirikiana na Shirika la Kimarekani la Walter Reed.
Wakipokea msaada huo ambao ni viatu, sare za shule, madaftari, kalamu na seti za vifaa vya hisabati pamoja na ada, walezi wa watoto hao waliyapongeza mashirika hayo kwa msaada huo.
Mkazi wa eneo la Isanga, Raphael Sanga, alisema ni aibu kuona watoto wengi wanaishi kwenye mazingira hatarishi wakati wazazi wao wapo na ukichunguza utakuta wazazi hao walihamia mijini wakidhani kuna unafuu wa maisha.
“Wazazi wanapaswa wajitambue wana wajibu wa kutunza familia zao, tatizo kubwa la wazazi wengine ni kuhamia mijini wao na familia zao wakidhani wataishi maisha bora zaidi kumbe matokeo yake wanashindwa kuwalea watoto wao na kusababisha wakimbilie mitaani na kuishi maisha ya tabu,” alisema Sanga.
Naye Chiku Mdachi, mkazi wa Soweto, alisema msaada huo utawasaidia zaidi watoto yatima kwani wataweza kuendelea na masomo.
Meneja wa Kihumbe, Ptolemy Samwel, alisema zaidi ya sh milioni 96 zimetumika kununulia vifaa mbalimbali huku sh milioni 39 wamezitumia kuwalipia ada wanafunzi wa sekondari, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu wanaosaidiwa na shirika hilo wakati wanafunzi 2500 wamepatiwa viatu vya ngozi kwa ajili ya matumizi ya shule.
Samwel alisema wanafunzi waliosaidiwa ni kutoka wilaya za Chunya, Rungwe, Mbeya vijijini na Jiji la Mbeya ambapo shirika hilo linafanyia shughuli zake.
na Christopher Nyenyembe , Mbeya
|