Friday, September 21, 2012

Uzinduzi Wa Kamusi Za Lahaja Za Kimakunduchi Kitumbatu Na Kipemba



Na: Mwashungi Tahir-Maelezo Zanzibar 20/09/2012 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini amesema kuna kila sababu ya kuitumia na kuienzi lugha ya Kiswahili kutokana na umuhimu wake nchini. Dk Mwinyihaji ameyasema hayo alipokuwa akimuakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohammed Shein katika uzinduzi wa Makamusi ya Lahaja za Kitumbatu, Kimakunduchi na Kipemba na Kitabu cha ‘Hazina inayopotea’ huko ukumbi wa salama hall Bwawani mjini Zanzibar. 
Amesema Lugha ya Kiswahili inafaa kuenziwa na kutunzwa ipasavyo kwani ni lugha ambayo inawaunganisha Wazanzibari na nchi nyingi za Kiafrika. Amesema uzinduzi wa Kamusi huo utakuwa ni chachu ya kukiendeleza Kiswahili na kuwataka wanalahaja wote kutoona aibu kuzungumza lahaja hizo katika maeneo yote ikiwemo ya mjini na vijijini. 
Aidha Dk.Mwinyihaji amefurahishwa na uzinduzi wa Kamusi za lahaja hizo hasa ikizingatiwa kuwa wanalahaja wenyewe walikuwepo katika uzinduzi huo jambo ambalo lilivutia katika hafla hiyo “Hii ni fursa tosha ya kuendeleza kwa lahaja hizi ambapo wazanzibar watafaidika nazo watakapozitumia pahala popote iwe mjini au vijijini ” Amesema Dk.Mwinyihaji Amesisitiza Wazanzibar kuzisoma vyema Kamusi hizo ili wapate kuzijua lahaja hizo kwa undani na kuweza kuendeleza umahiri wao katika lugha ya kiswahili . Akizungumzia kitabu cha ‘Hazina inayopotea’ Dk.Mwinyihaji amesema kitabu hicho ni matokeo ya utafiti uliofanywa na kubaini mmong’onyoko wa maadili ya Zanzibar unavyoendelea ambapo pia kitakuwa mchango muhimu wa kuyalinda maadili hayo.
 Aidha ametoa wito kwa Baraza la Kiswahili Zanzibar(BAKIZA) na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) kuendelea kutoa mchango wao katika kuandika vitabu vyenye taauluma ya lugha ya Kiswahili ambavyo vitazidi kukuza na kueneza lugha hiyo nchini. Kwa upande wake Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Zanzibar Said Ali Mbaruku amesema lugha ni sehemu muhimu katika nchi hivyo wazanzibar wana dhima kubwa ya kuilinda na kuienzi lugha ya Kiswahili. Nae Mwakilishi wa Qxford Peter Nyolo na mwakilishi wa UNISEF Erick Kajiri wametoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein kwa kuipa kipaumbele lugha ya Kiswahili nchini na kusaidia maendeleo yake katika Afrika ya Mashariki. Uzinduzi huo wa Makamusi ya Lahaja za Kitumbatu, Kimakunduchi na Kipemba na Kitabu cha ‘Hazina inayopotea’ ni miongoni mwa mikakati ya kuienzi na kutunza lugha ya Kiswahili nchini. 

IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR