John Terry ameadhibiwa na chama cha kandanda cha England, FA, asicheze mechi nne, na vile vile alipe faini ya pauni 220,000, kutokana na matamshi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya mchezaji wa QPR, Anton Ferdinand.
Chama cha FA kilithibitisha Terry alifanya makosa hayo, baada ya kusikiliza kesi dhidi yake kwa kipindi cha siku nne. Msemaji wa John Terry alisema mchezaji huyo "alisikitishwa" na hatua ya FA, kwa kuamua tofauti, kinyume na mahakama, ambayo awali ilisema hana makosa.
Terry ana muda wa siku 14 kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, mara tu atakapopokea maelezo ya adhabu hiyo kupitia maandishi. Adhabu hiyo haitatekelezwa hadi Terry atakapopata nafasi ya kuamua atafanya nini. Taarifa kutoka klabu yake ya Chelsea iliongezea: "Klabu ya Chelsea inafahamu vyema uamuzi uliopitishwa, na inaheshimu uamuzi huo uliotolewa leo na chama cha FA kumhusu John Terry."