Friday, September 28, 2012

WANYANG’ANYI WAUAJI WA WALINZI WANASWA NA JESHI LA POLISI MWANZA WAKIWA NA MTUTU WA KIENYEJI



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Liberatus Barlow akionyesha silaha hiyo iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na risasi sita za Short-gun inayohusishwa na matukio ya ujambazi ikiwa ni pamoja na tukio la kumuua mlinzi mmoja na kumjeruhi mwingine kwa kumpiga nondo kichwani maeneo ya Busweru kona Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza.


Silaha hiyo iliyotengenezwa kienyeji kwa ukaribu zaidi.

Silaha hiyo iliyotengenezwa kienyeji, risasi zilizokamatwa na RB ya polisi.

JESHI la Polisi Mkoani Mwanza limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu wa tukio la ujambazi wakiwa na silaha moja ya kienyeji ikiwa na risasi sita za Short-gun na kukili kufanya uhalifu na kumuua mlinzi mmoja na kumjeruhi mwingine kwa kumpiga nondo kichwani maeneo ya Busweru kona Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Liberatus Barlow akizungumza ofisini kwake amesema kuwa  jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata majambazi hao wanaohusishwa na tukio lililotokea Septemba 6 mwaka huu majira ya saa 9:00 usiku katika maeneo ya maduka mawili Busweru kona Kata ya Busweru Wilayani Ilemela ambapo watuhumiwa walimuua mlinzi mmoja Mwita Chariya(40) na kumjeruhi mwingine Mwita Wambura wote wakiwa wakazi wa Mabatini Wilayani Nyamagana.


Kamanda Barlow amesema kuwa baada ya tukio hilo jeshi la polisi liliunda kikosi kazi na kuanza msako wa kuwatafuta wahusika wa tukio hilo huku wakipokea ushirikiano wa raia wema kwa kutumia falsafa ya polisi jamii na ulinzi shirikishi ambapo mnamo Septemba 26 mwaka huu majira ya saa 7:30 walianda mtego na kufanikiwa kumkamata  moja kati ya watuhumiwa  Jonathan Fredrick mkazi wa Nyakato jijini Mwanza akiwa nyumbani kwake. 


Mtuhumiwa huyo baada ya kukamatwa aliwataja wenzake nalo jeshi la polisi likaweka mtego mwingine na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine wawili walio salia Mkubwa Rajab na Jonathan Athuman wote wakazi wa Mabatini.


Watuhumiwa hao licha ya kukiri kufanya matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha likiwemo hilo la kuua mlinzi waliwaonyesha mahala walipoficha silaha hiyo iliyotengenezwa kienyeji.