Wednesday, February 18, 2015

Chenge: Mimi ni ‘nyoka wa makengeza’..kwa kuwa mimi ni mjanja wa kutafuta fedha



Chenge: Mimi ni 'nyoka wa makengeza'..kwa kuwa mimi ni mjanja wa kutafuta fedha
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.

Asema ni yule mwenye makengeza, Asisitiza kuwa ni mtafuta fedha

Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, 'amefunguka' kuhusu kashfa inayomkabili ya kupata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwenye fedha zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), akisema hastahili kuitwa mwizi, bali anapaswa kuitwa 'nyoka wa makengeza'.
Amesema anapaswa kuitwa 'nyoka wa makengeza' kwa kuwa yeye ni mjanja wa kutafuta fedha kwa ajili ya wananchi wa jimbo lake, ambao wanapaswa kupuuza madai ya wizi yanayoelekezwa kwake, badala yake wamwamini zaidi.
Chenge, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) mstaafu, alisema hayo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mahaha kata ya Bunamala, Wilaya Bariadi mkoani Simiyu juzi.
Alisema kwa muda mrefu amekuwa kimya, lakini ameshangazwa na kitendo cha kuandamwa kuhusiana na kashfa ya akaunti hiyo.
"Wanasema Chenge na Escrow…Pale nimeenda kutafuta kwa ajili ya wananchi wa jimbo langu wala sikwenda kubomoa duka. Bali tunatumia akili kutafuta pesa kwa ajili yenu," alisema Chenge.
Chenge alitoa kauli hiyo wiki chache baada ya kusimama bungeni na kusema amelazimika kufanya hivyo baada ya kumvumilia Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, aliyetaka wabunge wachunguzwe kuhusiana na kashfa ya akaunti hiyo na wa kwanza kuchunguzwa awe Chenge.
Alisema kama Mdee ana ushahidi wa tuhuma anazozielekeza kwake, aupeleke bungeni kama kanuni za Bunge zinavyotaka au tuhuma hizo akaziseme nje ya ukumbi wa Bunge.
"Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningelipenda Bunge hili liendelee kuwa na heshima yake. Pili, naomba sana hayo wanayoyasema wawe na ujasiri wa kwenda kuyasema nje ya ukumbi huu wa Bunge, wasijifichie katika immunity (kinga) ya Bunge," alisema Chenge.
Alisema anayo mengi ya kusema, lakini kwa sababu alisimama kuhusu utaratibu, kumtaja yeye kwa jina moja kwa moja, anaomba aweke ushahidi mezani.
Mdee alitoa pendekezo hilo wakati akichangia mjadala kuhusu taarifa ya PAC na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), bungeni, Januari 30, mwaka huu.
Alisema Chenge amekuwapo katika kashfa mbalimbali za ufisadi, kuanzia ile inayohusu mikataba mibovu.
Kashfa nyingine za ufisadi ambazo alisema Chenge ameshiriki ni pamoja na inayohusu kampuni ya kufua umeme ya Independent Tanzania Limited (IPTL).
Nyingine alisema ni ya hivi karibuni ambayo alipata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 zilizochotwa kifisadi katika akaunti hiyo.
"Tuanze kuchunguzana wabunge, tuanze na Chenge," alisema Mdee.
 Kauli hiyo ya Mdee ndiyo iliyoonyesha kumkera Chenge na kulazimika kusimama bungeni siku hiyo na kutoa kauli hizo.
Kwa mujibu wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), fedha zinazodaiwa kuchotwa kutoka akaunti hiyo, ni zaidi ya Sh. bilioni 300 wakati kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete, ni Sh. bilioni 202.9.
Chenge alitajwa kupata mgawo huo kutoka katika fedha hizo na taarifa maalum ya PAC iliyowasilishwa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe na Makamu wake, Deo Filikunjombe, bungeni Novemba 26, mwaka huu.
Taarifa hiyo ya PAC, ilimtaja Chenge kupata mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwenye fedha zilizochotwa kutoka katika akaunti hiyo.
Wengine waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC kupata mgawo kutoka katika fedha hizo, ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka (Sh. bilioni 1.6), Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja (Sh. milioni 40.4) na Mbunge mstaafu wa Sumbawanga Mjini (CCM), Paul Kimiti (Sh. milioni 40.4).
 Pia wamo aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh. milioni 40.4); aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Enos Bukuku (Sh. milioni 161.7), Jaji Profesa John Ruhangisa (Sh. milioni 404.25), Jaji Aloysius  Mujulizi (Sh. milioni 40.4) pamoja na Mkurugenzi mstaafu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Philip Saliboko (Sh. milioni 40.4).
Wengine ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Ole Naiko (Sh. milioni 40.4), Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lucy Appollo (Sh. milioni 80.8); Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini (Sh. milioni 80.9); Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa (Sh. milioni 40.4) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh. milioni 40.4).
Kutokana na taarifa hiyo ya PAC iliyohusu ukaguzi maalum wa malipo yaliyofanyika katika akaunti hiyo, Novemba 29, mwaka jana, Bunge lilipitisha maazimio nane dhidi ya wote waliohusika na kashfa hiyo.
Ukaguzi huo ulifanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
 Taarifa hiyo ya PAC, ilieleza kuwa mmiliki wa kampuni ya Pan African Power Solutions Ltd (PAP), Harbinder Singh Sethi, mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering & Marketing (VIP), James Rugemalira, walihusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha katika akaunti hiyo kwenda kwa kampuni hizo.
 Wengine waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC kuhusika katika kashfa hiyo ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini aliyesimamishwa kazi, Eliakim Maswi na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, aliyejiuzulu.
Prof. Muhongo alitajwa na taarifa hiyo ya PAC kuwa alikuwa dalali kati ya Rugemalira na Sethi kufanikisha uchotwaji wa fedha hizo kutoka katika akaunti hiyo.
 Wengine waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC kuhusika katika kashfa hiyo, ni pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
 Hivyo, Bunge likaazimia kuwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi watu wote waliotajwa na taarifa hiyo ya PAC kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya akaunti hiyo na wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo.
 Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya PAC, vitendo vilivyofanywa na watu hao vinaashiria makosa mbalimbali ya jinai, kama vile uzembe, wizi, ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi.
 Tayari Prof. Muhongo na Jaji Werema walikwishajiuzulu nafasi zao serikalini, huku Maswi, ambaye amesimamishwa kazi akiendelea kuchunguzwa.
 Pia tayari Prof. Tibaijuka ameshatimuliwa kazi na Rais Kikwete kwa kupokea fedha hizo kupitia akaunti yake binafsi iliyoko benki ya Mkombozi, kinyume cha maadili.
Pia kutokana na kashfa hiyo, Chenge, ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, alijiuzulu nafasi hiyo kutekeleza moja ya maazimio ya Bunge yaliyotaka yeye na waliokuwa wenyeviti wenzake wa kamati za Bunge; Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini), wavuliwe nyadhifa hizo. Wote walijiuzulu nyadhifa hizo.
Mbali na kujiuzulu, Februari 2, mwaka huu, Baraza la Maadili lilitangaza kuwaita kwa nia ya kuwahoji wabunge hao, akiwamo Prof. Tibaijuka, Ngeleja, Mwambalaswa na Chenge, kutokana na tuhuma za kashfa ya akaunti hiyo zinazowakabili.
Wabunge hao watafika mbele ya Baraza hilo, kuanzia Februari 23, mwaka huu.
 Ofisa Habari wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Johanither Barongo, alisema mahojiano hayo yatafanyika kwa wiki tatu na yataongozwa na Jaji mstaafu, Hamisi Msumi na wajumbe wengine wawili, Hilda Gondwe na Celina Wambura.
MIRADI MAENDELEO JIMBONI
Akizungumzia suala la wananchi na miradi ya maendeleo jimboni mwake, Chenge alisema mtaji wa maendeleo ni kila mwananchi kujituma katika kuchangia miradi mbalimbali na kushirikiana na viongozi na serikali kwa manufaa yao.
"Ndugu zangu, ni bora miradi tunayoileta vijijini mwenu mkaitunza ili tuendelee kuwatumikia kwa muda mrefu…na tufanye kazi ya kuilinda miradi hiyo na kuisimamia miradi yote iliyo ndani ya kata hii," alisema Chenge.
Mbunge huyo alitembelea maabara ya Shule ya Sekondari Sapiwi kuangalia maendeleo ya ujenzi wake baada ya Mfuko wa Jimbo kutoa mabati 300 kwa ajili ya kuezekea maabara.
Shilingi milioni 36 zimetumika kugharimia ujenzi huo, huku wananchi wakichangia Sh. milioni 10 na Sh. milioni 74 zikihitajika.
Awali, Ofisa Mtendaji wa kata ya Sapiwi, Telen Nhandi, alisema zipo changamoto zinazoikabili kata hiyo ikiwamo upotoshaji wa watu katika michango ya kuchangia maabara, ukame na kusababisha mazao mengi kuanza kuathirika.
Alisema hali hiyo imesababisha baadhi ya wananchi kushindwa kuchangia katika miradi ya maendeleo.