Monday, August 06, 2012

UPELELEZI KESI YA KUTUKANWA MWIGILU WAKAMILIKA.


Afisa sera na utafiti CHADEMA makao makuu Waitara Mwita Mwikwabe (37) akiwa amepumzika kwenye chumba cha mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida.(Picha na Nathaniel Limu).

Upelelezi wa kesi ya kutoa matusi kwa Mbunge wa Iramba magharibi, Mwigullu Lameck Nchemba, inayowakabili vigogo wawili wa Chama Cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA) umekamilika.
Kutokana na kukamilika huko, kesi hiyo inayovuta hisa ya wakazi wengi wa mkoa huu, itasikilizwa uchambuzi wa awali Septemba 3 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini hapa.

Vigogo hao wanaotuhumiwa kutenda kosa hilo Julai 14 mwaka huu saa 10 ni Afisa Sera na Utafiti wa CHADEMA makoa makuu, Mwita Waitara Mwikwabe (37) na mshauri wa CHADEMA na mhadhiri wa chuo kikuu Dar-es-salaam, Dk Kitila Mkumbo (41).
Wakili wa kujitegemea wa mjini hapa anayewatetea washitakiwa hao, Raymond Kimu, aliiomba mahakama hiyo ipange kesi hiyo kusikiliza uchambuzi wa awali Septemba 3 mwaka huu, kwa vile mshitakiwa Dk Kitila atakuwa na mikutano muhimu kati ya sasa na Septemba 1 mwaka huu.
Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Ruth Massamu alikubaliana na ombi hilo.
Kwa mujiubu wa mwanasheria wa serikali, Seif Ahmed, washitakiwa walimtukana Mbunge Mwigullu kuwa ni malaya, mzinzi na mpumbavu huku wakijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Seif alisema kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Nguvumali.
Katika hatua nyingine, vijana nane wakazi wa kijiji cha Nguvumali ya Ndago jimbo la Iramba Magharibi wanaotuhumiwa kumuuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (CCM) kata ya Ndago, Yohana Mpinga (30), kesi yao imeahirishwa hadi Agosti 13, mwaka huu.
Washitakiwa hao ni Manase Daudi (40), Williamu Elia (33), Frank Stanley (20), Charles Leonard (36), Tito Nintwa na Fillipo Edward (30).
Mwanasheria wa serikali mwandamizi, Neema Mwanda, alidai mbele ya hakimu Massamu kuwa mnamo Julai 14 saa kumi alasiri katika kijiji cha Nguvumali, washitakiwa wote kwa pamoja walimpiga kwa kutumia fimbo na mawe  mwenyekiti huyo kusababisha kifo chake.
Vile vile jumla ya washitakiwa 12 wanaotuhumiwa kufanya vurugu katika mkutano huo wa hadhara wa CHADEMA katika kijiji cha Nguvumali na kusababisha kuvunjika kwa amani na utulivu kesi yao imeahirishwa hadi Agosti 13 mwaka huu itakapotajwa tena.
Ilidaiwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.