Tuesday, August 07, 2012

Msikiti Wachomwa Moto Marekani



NewsImages/6557130.jpg
Mabaki ya msikiti uliochomwa moto kwenye mji wa Joplin kwenye jimbo la Missouri
Tuesday, August 07, 2012 3:19 AM
Msikiti mmoja nchini Marekani umeteketezwa kabisa kwa moto katika kile kilichoelezwa kuwa ni shambulio la chuki za kidini.
Msikiti huo ulioko Joplin kwenye jimbo la Missouri uliokuwa ukitumiwa kama nyumba ya ibada ya waislamu wapatao 125 uliteketea kabisa na hakuna kitu kilichookolewa toka kwenye msikiti huo.

Zimamoto na polisi waliitwa kwenye msikiti huo kwenye majira ya saa kumi kasorobo alfajiri kutokana na moto mkubwa uliokuwa ukiuteketeza msikiti huo.

"Jengo la msikiti limetekea kabisa", alisema msemaji wa polisi Sharon Rhine na kuongeza kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo.

Moto huo uliotokea jumatatu ni mfululizo wa jaribio la kwanza la kuuteketeza msikiti huo kwa moto ambapo tarehe 4 mwezi uliopita bomu la moto wa petroli lilirushwa kwenye paa la msikiti huo huo na kusababisha uharibifu mdogo baada ya moto kuwahi kuzimwa.

Kamera za ulinzi za msikiti huo zilinasa sura ya mtu aliyerusha bomu hilo la petroli na shirika la ujasusi la Marekani, FBI liliahidi zawadi ya dola 15,000 kwa mtu atakayetoa taarifa za chanzo cha shambulio hilo. Lakini hadi sasa hakuna mtu aliyetiwa mbaroni.

Katika tukio hili la jumatatu, kamera za ulinzi ziliteketezwa na moto huo.

"Ni tukio la kushangaza kwa kuwa kulikuwa na moto mwezi uliopita na mwezi huu tena moto mwingine umetokea", alisema afisa wa polisi.

Mwaka 2008 msikiti huo huo ulikumbwa na shambulio jingine la moto ambapo bango la jina la msikiti huo lilichomwa moto.

Wakati huo huo baraza la waislamu la Marekani limeomba polisi kutoa ulinzi kwenye nyumba za ibada baada siku moja kabla ya tukio hilo mwanajeshi wa zamani wa Marekani, aliyetajwa kwa jina la Wade Michael Page, kuwashambulia waumini kwenye hekalu la dini ya Sikh na kuua watu sita na kuwajeruhi watu wengine watatu kabla ya kuuliwa na polisi kwa kupigwa risasi.
Source:NIFAHAMISHE