Monday, August 20, 2012

MILIONI 27 ZATUMIKA KUNUNUA VITABU VYA KIADA



Zaidi ya Sh milioni 27.9 zimetumiwa na Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa ajili ya kununulia vitabu vya kiada katika shule 79 za msingi wilayani hapa, ili kukabiliana na uhaba wa vitabu.

Hayo yalielezwa na Naibu Mkurungezi wa Jiji la Tanga, David Mtatifikolo, katika kikao cha Baraza la Madiwani wakati akiwasilisha taarifa ya miradi iliyotekelezwa na halmashauri hiyo.

Alisema fedha hizo zilitolewa na halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Serikali kuu ikiwa na lengo la kupunguza uhaba wa vitabu katika shule mbalimbali nchini.

"Japo tuna upungufu mkubwa wa vitabu vya kiada katika shule zetu za msingi na sekondari, lakini kwa kuanzia tumeanza na shule za msingi ambazo zina uhitaji mkubwa ukilinganisha na za sekondari zilizopo katika jiji letu," alisema.

Vilevile alisema katika kipindi cha mwaka mmoja waliweza kulipa madeni ya walimu ya Sh milioni 114 walizokuwa wakiidai halmashauri hiyo katika kipindi hicho cha mwaka mmoja.

Mkurugenzi huyo alisema madeni yaliyolipwa ni pamoja na mishahara, likizo, uhamisho na madai mengine yanayohusiana na malimbikizo ya madeni mbalimbali ya walimu.

Naye Diwani wa Kata ya Ngamiani Kusini, Mussa Mbaruku, alisema ipo haja ya taarifa za michango ya wananchi katika sekta ya elimu kuwasilishwa katika baraza hilo, ili kubaini nguvu za wananchi katika miradi ya maendeleo.
Chanzo: Mtanzania