Tuesday, July 17, 2012

HOTUBA YA UPINZANI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013 WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI


HOTUBA YA MSEMAJIMKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA VINCENT JOSEPHAT NYERERE (MB), KUHUSUMAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013 WIZARA YA MAMBO YANDANI YA NCHI


(Kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)

UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Kwaniaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, napenda kuchukua fursa hii kuwasilishamaoni yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndaniya nchi kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Aidha, napenda kuwashukuru askari wa Jeshila Polisi na Jeshi la Magereza wanaoishi Kambi iliyoko katika Kata ya Mkendokwa kunichagua kuwa Diwani wao. Vile vile, nawashukuru wananchi wote wa vyamavyote na dini zote Jimbo la Musoma Mjini kwa kunichagua kuwa Mbunge na mteteziwao. Pia napenda kumshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwaimani yake kubwa kwangu kwa kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi katika Wizarahii.

Kwa upekee kabisa, Mheshimiwa Spika,kwa wanaoeneza propaganda kwamba CHADEMA inachukia au kudharau askari polisi wetu,naomba nitoe shukrani zangu kwa mke wangu
Helen
[o1] V. Nyerere, ambaye pia ni askari waJeshi la Polisi.
UTEKELEZAJI WAAHADI ZA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, Katikamwaka uliopita wa fedha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilihoji matukio mbalimbali ya mauaji ya raia yaliyowahusisha askari wa Jeshi la Polisi pamoja na wavyombo vingine vya dola. Aidha, tulihoji matukio mengi ya ukiukwaji wa haki zabinadamu za wananchi wetu hasa katika maeneo yenye migodi mikubwa ya dhahabukama vile Nyamongo, Arusha na kwingineko katika nchi yetu. Vile vile, tulihojisababu za Serikali kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria na za kiutendajiwatuhumiwa wa makosa haya makubwa.
Mheshimiwa Spika,Wakatianatoa hoja yake ya kuahirisha Mkutano wa Bunge la Bajeti la mwaka jana, WaziriMkuu aliahidi kwamba Serikali ingefanya uchunguzi wa matukio yote ya mauaji kwamujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (The Inquests Act), Sura ya 24 ya Sheriaza Tanzania. Kwa maneno yake mwenyewe, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema:"vifo ... ambavyo vimetokea katika mazingira ya kutatanisha chini ya mikono yaVyombo vya Dola, ni lazima vichunguzwe."Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, hadi wakati tunaandika maoni haya, hakunaMahakama ya Korona hata moja ambayo imeitishwa kwa lengo la kuchunguza vifo vilivyotokanana matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeniinaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama kauli yaWaziri Mkuu ilitolewa kwa lengo la kuwahadaa Watanzania. Aidha, Kambi Rasmi yaUpinzani Bungeni inaitaka Serikali itamke ni lini Serikali itaunda Mahakama zaKorona ili kuchunguza matukio yote ya mauaji ya wananchi katika maeneo yotetuliyoyataja mwaka jana.

Mheshimiwa Spika,Kwasababu ya Serikali kutotimiza ahadi yake ya kuchunguza matukio ya mauaji kwamujibu wa Sheria tajwa, vitendo vya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu vimeendeleakutokea katika nchi yetu. Kwa mfano, katika taarifa yake ya Haki za Binadamukwa Mwaka 2011, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinaripoti kwamba "mwenendowa matukio ya ukatili wa polisi na mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria navyombo vya dola umeendelea kuongezeka katika nchi yetu. Kati ya Januari naDesemba 2011 tayari watu 25 wamekwisharipotiwa kuuawa wakiwa mikononi mwapolisi na maafisa wengine wa usalama, wakati ambapo watu wengine 50walijeruhiwa." Taarifa hii inaungwa mkono na taarifa ya Hali ya Haki za Binadamu kuhusu Tanzania iliyotolewa mwaka huu na Wizaraya Mambo ya Nje ya Marekani (State Department)inayoonyesha kuwa bado yapo mauaji yanayotokea mikononi mwa vyombo vya dolaikiwemo jeshi la polisi, utesaji na wananchi wanaotuhumiwa kujikuta wakipatavipigo kinyume na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia.
MAUAJI YENYE SURAYA KISIASA
Mheshimiwa Spika,Kutokana na Serikali kutochukua hatua kukabilianana matukio ya mauaji yanayohusishwa na vyombo vya dola, sasa limezuka wimbi lamauaji na matukio ya majaribio ya mauji yenye sura ya kisiasa katika maeneombalimbali nchini. Matukio hayo ni pamoja na mauji ya kada wa CHADEMA MbwanaMasudi yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Igunga,na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Usa River, Marehemu Msafiri Mbwambo,mara baada ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki.

Aidha, Mheshimiwa Spika, kumekuwa na majaribio ya mauaji ambapo wabunge waCHADEMA Mheshimiwa Highness Kiwia wa Jimbo la Ilemela na Mheshimiwa SalvatoryMachemli wa Jimbo la Ukerewe, walioshambuliwa kwa mapanga mbele ya maafisapolisi na watu wanaosadikiwa kutumwa na makada wa CCM mkoani Mwanza. Vile vile,Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA) alivamiwana wafuasi wa CCM wanaodaiwa kutumwa na Iddi Chonanga, Diwani wa Kata ya Nduli (CCM)katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Mheshimiwa Spika, Matukio ya mauaji au majaribio ya mauajiyenye sura ya kisiasa yamewahusu pia watu ambao sio wanachama au viongozi wavyama vya siasa lakini wanaonekana kupinga matakwa ya watawala. Haya yamemkuta Mwenyekitiwa Jumuia ya Madaktari Dr. Steven Ulimboka ambaye alitekwa nyara na kuteswa kwakikatili na watu ambao taarifa za vyombo vya habari zimewataja kuwa maafisa wavyombo vya dola. Kwa mara nyingine tena, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeniinaitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iamuru kukamatwa kwa watuhumiwawote ambao wametajwa kuhusika na utekaji nyara na jaribio la kumuua Dr.Ulimboka ili kufuta dhana kwamba vyombo vya dola viko juu ya sheria na vinawezakuua au kutesa wananchi bila mkono mrefu wa sheria kuwaangukia.

Mheshimiwa Spika, Tarehe 14 Julai 2012, mtu anayesemekanakuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM katika Kata Ndago, Jimbo la IrambaMagharibi, Yohana Mpinga, ambaye pia ni mtoto wa Mwenyekiti wa CHADEMA katikaKata ya Urughu alifariki dunia kufuatia vurugu zilizotokea baada ya kumalizikakwa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na viongozi wa CHADEMA katika Kata ya Ndago.Kwa vile, tayari baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali ndani ya Bunge hilitukufu wanaelekea kuwa wameshapitisha hukumu kwamba CHADEMA inahusika na kifocha Marehemu Yohana Mpinga, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina haya ya kuelezakuhusiana na tukio hili.
Kwanza, mkutano wa hadhara wa CHADEMAulihudhuriwa pia na maafisa polisi waliokuwepo wakati wote wa mkutano huo.Pili, licha ya kuwepo kwa maafisa polisi hao, kundi la wahuni wanaodaiwakukodiwa na makada wa CCM wa Jimbo la Iramba Magharibi walivuruga mkutano huokwa kupiga mawe watu waliohudhuria mara mbili lakini mara zote polisiwaliokuwepo hawakuchukua hatua zozote dhidi ya kundi hilo la wahuni. Aidha,mara ya wahuni hao kuvuruga mkutano mara ya pili, viongozi wa CHADEMA walitoataarifa rasmi katika Kituo cha Polisi cha Ndago na kufunguliwa jalada nambaNDG/RB/190/2012.

Tatu, mara baada ya kutoa taarifa hiyo kwapolisi, mkutano wa hadhara uliendelea bila fujo yoyote hadi ulipomalizika na msafarawa viongozi wa CHADEMA kuondoka eneo la Ndago na kuelekea Kinampanda ambakokulikuwa na mkutano mwingine wa hadhara. Wakati huo, kundi la askari polisi waKikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) kutoka Kiomboi walishafika katika eneo lamkutano na kukuta mkutano umemalizika. Nne, kwa vile mkutano wa hadhara waCHADEMA ulimalizika kwa amani mbali na matukio ya kihuni yaliyoripotiwa kwa Jeshila Polisi, na kwa vile kulikuwa na kikosi cha FFU na askari polisi wenginekatika eneo la mkutano baada ya msafara wa CHADEMA kuondoka, ni wazi kwamba watuwanaotakiwa kutoa maelezo ya jinsi Marehemu Yohana Mpinga alivyofikwa na mautini Jeshi la Polisi lenyewe.

Aidha, Mheshimiwa Spika, ni Jeshi la Polisi pekee linaloweza kuwaelezaWatanzania kwa nini kikundi cha wahuni waliowarushia mawe viongozi wa CHADEMAna wananchi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara hawakuchukuliwa hatua zozotena polisi waliokuwepo kwa muda wote wa mkutano huo au askari wa FFU waliofikabaada ya msafara wa CHADEMA kuondoka. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwasana na mauaji ya kijana huyo na inatuma salamu za pole na rambi rambi kwafamilia, ndugu na jamaa wa marehemu. Hata hivyo, Kambi yetu inasikitishwa nakushangazwa sana na ushabiki wa kisiasa ambao umejitokeza humu Bungeni na kauliza kutoa hukumu ambazo zimetolewa na baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikalibila hata kusubiri uchunguzi kamili juu ya jambo hili.
MASLAHI YA POLISI NA MAGEREZA
Mheshimiwa Spika, Katikamaoni yake ya mwaka jana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia utamaduniwa Serikali kupuuza maslahi ya askari polisi na wale wa Jeshi la Magereza. Utamadunihuu ni wa muda mrefu sana. Kwa mfano, katika hotuba ya bajeti ya Waziri wa Mamboya Ndani kwa mwaka wa fedha 2006/2007, aliyekuwaWaziri wakati huo alikiri kwamba "... kutokana na kipato kidogo cha askari polisi,inawawia vigumu kukopa katika mabenki nchini kutokana na riba kuwa kubwa nakukosa dhamana za uhakika. Hivyo, askari polisi hawana mahali popote wanapowezakupata fedha za kujiendeleza kiuchumi. Aidha, mishahara na posho wanayolipwaaskari bado haikidhi hali halisi ya mahitaji yao na familia zao."

Mheshimiwa Spika,Tokawakati huo hadi sasa, maslahi ya askari polisi yamekuwa mabaya zaidi kutokanana kushuka kwa thamani ya shilingi na mfumuko wa bei hasa za vyakula kupandawakati ambapo mishahara yao haijaongezeka sambamba na ongezeko la gharamahalisi za maisha. Aidha, katika hali inayoonyesha kutokujali kabisa maslahi nahali za maisha za askari wetu, Serikali imeshindwa kutekeleza ahadi yakeiliyotolewa tarehe17 Novemba, 2011 na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya ndani Mheshimiwa KhamisSued Kagasheki, aliyeliambia Bunge hili tukufu kwamba "... posho yaaskari imepandishwa na ... kwamba (inatakiwa) itoke kwenye shilingi laki mojampaka shilingi laki moja na hamsini.... Ni jambo ambalo tunalo na tumelifanyiakazi na tuna uhakika kwamba, litaweza kutimia…."

Mheshimiwa Spika, Ni ukweli usio na mjadala kwamba askaripolisi na magereza bado wanapokea posho ya kujikimu ya shilingi laki mojabadala ya shilingi laki moja na elfu hamsini iliyoahidiwa na Serikali mbele yaBunge hili tukufu. Aidha, katika mazingira yakushangaza kabisa, mara baada ya Serikali kutoa ahadi Bungeni juu ya poshohiyo, uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi ulituma maelekezo kwa Makamanda waPolisi wa Mikoa kufanya uchunguzi ili kubaini askari wote waliokuwa wanadaiwalipwe posho ya shilingi laki moja na nusu kama ilivyoahidiwa ili askari haowafukuzwe kazi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitakaSerikali ilieleze Bunge lako tukufu ni lini italipa malimbikizo ya baki yashilingi elfu hamsini kwa mwezi kwa kila askari polisi na magereza ambayohaijawalipa askari hao hadi hivi sasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeniinaitaka Serikali ianze kuwalipa askari polisi na magereza posho ya kujikimu yashilingi laki moja na nusu kwa mwezi kuanzia mwaka huu wa fedha, kwa vile ahadiya Serikali iliyotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani haijawahikukanushwa, kubatilishwa au kubadilishwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika,Sio tukwamba Serikali haitekelezi ahadi inazotoa Bungeni juu ya malipo ya askaripolisi na magereza. Serikali pia imekuwa inawakopa watumishi hao bila ridhaayao. Kwa mfano, randama ya fungu la 29 inaonyesha kuwa Jeshi la magerezalinadaiwa jumla ya shilingi bilioni 23.65. Kati ya fedha hizo, watumishi waJeshi la Magereza wanaidai Serikali jumla ya shilingi bilioni10.34 ambazo nimalipo ya stahili zao mbali mbali kama vile fedha za likizo, uhamisho, mafunzo,n.k. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele yaBunge hili kama, na lini, italipa madeni haya ya askari magereza wetu wanaokeshamagerezani usiku na kushinda juani mchana wakiwalinda wafungwa na mahabusuwaliojaa katika magereza ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Kuna hatari kwa askari wa Jeshi la Magereza kufanyakazi katika mazingira magumu ambayo tumeyaeleza katika maoni haya. Mfano ni katikaJimbo langu la Musoma Mjini. Mbali na makazi duni ya askari magereza, vile vilekuna umbali mrefu kati ya kambi ya askari magereza ya Nyasho na Gereza la Mkoalililopo Kata ya Mkendo na askari magereza wamekuwa wakitembea kwa miguu usikuwanapokuwa zamu gerezani. Hii inahatarisha usalama wao kwani wanaweza kuvamiwana kudhuriwa na wafungwa au mahabusu waliokwisha kumaliza adhabu zao lakiniwakawa na visasi na askari hao. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitakaSerikali iwapatie gari askari wa kambi ya Nyasho na makazi mengine ya askarimagereza yaliyoko mbali na magereza wanakofanyia kazi ili kunusuru maisha yaaskari magereza wetu.

Mheshimiwa Spika,Katikamaoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya mwaka jana, tulipendekeza kwamba "...utaratibu wa sasa wa polisi wa ngazi za chini kukatwa shilingi 5,000 kila mwezikwenye mishahara yao, kwa ajili kugharamia mazishi yao na wategemezi wao,ufutwe mara moja, kwani unawanyonya kwa sababu vipato vyao ni vidogo. Badalayake ... serikali ibebe jukumu hilo." Hata hivyo, hadi tunaandika maoni haya,Serikali imeendelea kupuuza mapendekezo haya kwa kisingizio kwamba 'mfuko wa kufa na kuzikana' ni wa hiariilhali askari polisi wanaendelea kukatwa mishahara yao kwa lazima. Kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi yaUpinzani Bungeni inatamka kwamba kukata mshahara wa mfanyakazi bila ridhaa yakewakati hadaiwi chochote na mwajiri wake ni kinyume cha sheria husika za nchiyetu na kitendo cha jeshi la Polisi kuendelea kukata mishahara ya askari polisikwa ajili ya 'mfuko wa kufa na kuzikana' bila ridhaa ya askari polisi wenyewekikome mara moja.

Mheshimiwa Spika,KambiRasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba askari polisi wanaofanya kazi zalindo katika mabenki yote ya biashara hapa nchini hulipwa posho ya shilingielfu kumi kwa siku. Hata hivyo, Serikali haijawahi kutamka hadharani kiasiambacho mabenki hayo hulipa serikalini kwa ajili ya kazi hiyo ya kulindamabenki binafsi. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitakaSerikli kulieleza Bunge lako tukufu kiasi ambacho mabenki ya biashara hulipaserikalini kwa ajili ya huduma ya ulinzi inayotolewa na askari polisi ili Bungelako lifahamu kama askari polisi wanaofanya kazi hiyo wanalipwa inavyostahili.
VITENDEA KAZI VYAPOLISI
Mheshimiwa Spika, Kwamujibu wa ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa,makosa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi hapa nchiniyalikuwa 62,133. Ripoti inasema kwamba kwa mwaka 2011 makosa 63,703 ya jinaiyaliripotiwa katika vituo vya polisi nchini.Kwa kiasi kikubwa, ongezeko hili la uhalifu linasababishwa naaskari wa doria kushindwa kufika kwenye maeneo ya matukio ya uhalifu kwa harakapindi wapatapo taarifa kwa kisingizio cha kukosa mafuta kwa ajili ya magari yadoria.

Hatahivyo, Mheshimiwa Spika, nyaraka zaSerikali zinaonyesha kwamba Bunge lako tukufu limekuwa likiidhinisha fedhanyingi kwa ajili ya mafuta ya magari ya Jeshi la Polisi. Kwa mfano, kwa mujibuwa randama ya Fungu la 28 kwa mwaka huu wa fedha, matumizi halisi ya mafuta kwaajili ya Jeshi la Polisi kwa mwaka wa fedha 2010/2011 yalikuwa shilingi bilioni2.81. Aidha, katika mwaka wa fedha uliopita Bunge lako tukufu liliidhinishashilingi bilioni 2.61 kwa ajili ya mafuta, wakati ambapo kwa mwaka huu wa fedhaSerikali inaomba Bunge liidhinishe shilingi bilioni 2.56 kwa ajili ya mafuta yamagari ya Jeshi la Polisi.

WakatiBunge limekuwa lkiidhinisha mafungu haya makubwa ya fedha kwa ajili ya mafuta,askari polisi wamekuwa wakilalamika kwamba hawapewi fedha za mafuta kwa ajiliya magari ya doria hivyo kusababisha askari polisi kushindwa kufanya kazi zaohizo ipasavyo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ielezezinakopelekwa fedha za mafuta kwa ajili ya Jeshi la Polisi kama gari moja ladoria linapatiwa lita 5 za mafuta kwa kutwa na/au usiku.
IDARA YA UHAMIAJINA PAKACHA LA MIPAKA
Mheshimiwa Spika,Mipakayetu na nchi jirani zinazotuzunguka imekuwa pakacha linalovuja. Ndio maanakatika hotuba yetu ya mwaka janatuliliambiaBunge lako tukufu kwamba "... kumekuwana ongezeko la wageni wengi kutoka nchi za nje ... kiasi cha kujiuliza kamanchi hii ina utaratibu wowote wa kuratibu na kudhibiti uingiaji wa wageni hapanchini." Tulionyesha jinsi ambavyo kumekuwa na ongezeko la wageni haramu kutokanchi za Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi, Rwanda, Kenya,Uganda, Pakistan, Nigeria, China, India na Bangladesh "ambao wanaishi Tanzaniakwa mfumo usio rasmi, bila ya kuwa na hati zinazowaruhusu kufanya hivyo."Tulitahadharisha kwamba "utaratibu wa kuachia kila mgeni kuingia Tanzania nakuishi atakavyo bila ya vyombo husika kujua kuwepo kwake ni hatari kiusalama,hasa katika zama hizi za kusambaa kwa ... ugaidi na uharamia wa kimataifakatika masuala ya fedha, biashara za binadamu ..." n.k.

Mheshimiwa Spika, Manenona tahadhari zetu ziliangukia kwenye masikio ya Serikali kiziwi. Na sasa yaletuliyoyasema yameanza kutimia kwani ni mwezi mmoja tu umepita tangu wahamiajiharamu zaidi ya arobaini kutoka Ethiopia kukutwa wamekufa ndani ya lori lamizigo ambalo kwa vyovyote vile lilitokea nchi jirani. Watu hawa waliingiajenchini na kusafiri hadi katikati ya nchi yetu bila kujulikana na maafisa waUhamiaji, polisi wa usalama barabarani na usalama wa taifa kama kweli nchi yetuiko salama? Ni afisa gani wa Idara ya Uhamiaji aliyewapitisha katika mpaka wetuwa Namanga au Horohoro au Sirari au Kogaja au Borogonja? Na ni askari polisigani aliyewasindikiza hadi Kongwa? Aidha, ni afisa mizani gani wa TanRoadsaliyepitisha lori walimokuwa watu hao bila kulikagua na kujua kilichokuwamo?
KambiRasmi ya Upinzani Bungeni ilitegemea – kwa kuzingatia ukubwa na uzito wa kashfahii – viongozi waadilifu katika Wizara, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi wangewajibikakutokana na uchafu huu. Hata hivyo, hakuna hata mmoja ambaye amefanya hivyo.Kwa vile uwajibikaji wa hiari unaelekea kushindikana, Kambi Rasmi ya UpinzaniBungeni inamtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuwawajibishawale wote waliohusika kuanzia viongozi wa Wizara walioko humu Bungeni nauongozi wa juu wa Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi ili kuondokana na aibuhii ya nchi yetu kuwa transit routeya biashara ya kusafirisha binadamu katika sehemu hii ya Bara la Afrika.

Mheshimiwa Spika,Matatizoya ongezeko la wahamiaji haramu katika nchi yetu linatokana na Idara yaUhamiaji kuendekeza vitendo vya kifisadi katika kuajiri, kupandisha madaraja auvyeo wa maafisa wa Idara hiyo. Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, ajira katikaIdara ya Uhamiaji haizingatii tena elimu, uwezo na weledi wa maafisa husika.Bali, kwa mujibu Taarifa ya Utafiti waMpango Mkakati wa Mageuzi Katika Utumishi wa Uhamiaji (Immigration Service Reform Programme Strategic Plan Research Report)iliyochapishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani tarehe 27 Novemba, 2011, "mara nyingi mgawanyo ya kazi (katika Idara)hautegemei sifa bali unategemea upendeleo, rushwa, kujuana na urafiki vituambavyo viko kinyume na maana halisi ya mgawanyo wa kazi." ("Most of the timeplacement is not based on merits but depends on nepotism, bribery and technicalknow-who, friendship and favouritism that have been contrary to the wholemeaning of placement.")

Mheshimiwa Spika, Ushahidiwa kauli hii unapatikana katika Taarifa hiyo ya Utafiti inayoonyesha kwamba maafisawengi wa ngazi za juu katika Idara ya Uhamiaji ni watu wenye uwezo mdogokielimu kulinganisha na maafisa wa ngazi za chini wa Idara hiyo. Kwa mfano, katikangazi ya Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji kwenda juu hadi kwa Kamishna Mkuu, kunamaafisa kumi wenye shahada ya uzamili (masters degree), wawili wenyepost-graduate diploma (PGD), ishirini na nne wenye shahada ya kwanza, tisawenye stashahada, saba wenye diploma, kumi na moja wenye kidato cha sita na 248wenye elimu ya kidato cha nne. Katika maafisa hawa wa ngazi za juu, kunaKamishna mmoja mwenye elimu ya kidato cha nne wakati kuna Makaimu Kamishna 216wenye elimu hiyo ya kidato cha nne na Kamishna Wasaidizi Wakuu 31.

Kwaupande mwingine, Mheshimiwa Spika, kuanziangazi ya Mrakibu Mwandamizi (Senior Superintendent) kwenda chini mpaka koplokuna maafisa wenye shahada ya uzamili 36, wenye post-graduate diploma wakosaba, wenye shahada ya kwanza wako 340, wenye stashahada wako 78, diploma wakokumi wenye cheti (certificate) wako 52, waliomaliza kidato cha sita wako 585wakati waliohitimu kidato cha nne wako 337. Katika mazingira ambayo maafisawenye uwezo mkubwa wa elimu hawapewi nafasi za juu katika Idara badala yakeuongozi wa juu umejazwa na wenye elimu za mashaka kama inavyoonyeshwa katikaTaarifa ya Utafiti ya Wizara, ni wazi kwamba matukio kama ya maafa ya wahamiajiwaliokutwa wamekufa Jimboni kwa Naibu Spika wa Bunge hili tukufu hayawezikuepukika!

Aidha,Mheshimiwa Spika, katika mazingiraya upendeleo na rushwa katika ajira ya Idara ya Uhamiaji ya aina hii, maafisauhamiaji hawawezi kuacha kutumiwa na wanasiasa wa chama tawala kuwatuhumu washindaniwao kisiasa kuwa sio raia wa Tanzania ili kuwaondoa katika kinyang'anyiro chachaguzi zetu. Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Mheshimiwa Ali Mohamed Keissy alipotakakugombea Ubunge kwa tiketi ya CHADEMA na kuzushiwa tuhuma kuwa siyo raia. Hatahivyo, alipojiunga na CCM bila ridhaa yake tuhuma za kutokuwa raia ziliyeyukana sasa ni Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini katika Mkoa anakotokeaWaziri Mkuu!

Mheshimiwa Spika,KambiRasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bungehili tukufu juu ya mambo haya ambayo yamethibitishwa na Ripoti ya Utafiti yaWizara ya Mambo ya Ndani. Aidha, Kambi inaitaka Serikali itoe kauli kama kunahaja yoyote ya kutumia mamilioni ya fedha za wananchi kusomesha maafisa wa Idaraya Uhamiaji ambao baada ya kufuzu hawapatiwi vyeo na majukumu yanayolingana nauwezo wao wa kielimu.
JESHI LA ZIMA MOTO NA UOKOAJI
Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kuwa umuhimu wa Jeshi hili unaonekana paleyanapotokea majanga ya moto, mafuriko au maafa mengine kama vile tetemeko laardhi ambapo athari za matukio haya ni makubwa sana na mara nyingi hupelekeawananchi kupoteza maisha. Malalamiko ya wananchi katika maeneo mbalimbali juuya Jeshi la Zimamoto kuchelewa kufika katika maeneo ya tukio yamekuwepo kwa miakamingi na yamepigiwa kelele sana hapa Bungeni. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudiaushauri wake kuwa Serikali iboreshe mfumo mzima wa zimamoto katika nchi yetuili kukabiliana na majanga ya moto yanayoongezeka kutokana na kupanuka na kukuakwa miji yetu.

Mheshimiwa Spika, Baadaya maelezo na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ninaombakuwasilisha.
.....................……………………… ……………..

VINCENTJOSEPHAT NYERERE


MSEMAJI MKUU WA


KAMBI RASMI YAUPINZANI BUNGENI


WIZARA YA MAMBO YANDANI YA NCHI


17/07/2012