Friday, July 27, 2012

HOTUBA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI; WIZARA YA NISHATI NA MADINI

HOTUBA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI; WIZARA YA NISHATI NA MADINI

HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI
NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA
UPINZANI JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012 NA
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA
FEDHA 2012/2013

UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, awali ya yote niungane na wote wenye mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Kanuni Kudumu za Bunge (Toleo la mwaka 2007) kifungu cha
99 (7) wa kuishauri na kuisimamia serikali; kwa kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

Mheshimiwa Spika, nitumie pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi waliouniunga mkono kwa hali na mali katika kipindi chote cha misukosuko ya kusimamia ukweli na uwajibikaji: katika kuifuatilia serikali na kuunganisha wadau wengine kuwezesha maendeleo katika jimbo la Ubungo; wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya ushindi wetu; wakati wa operesheni za 2

kuhamasisha mabadiliko katika maeneo mengine nchini na katika uwakilishi wa wananchi bungeni. Utaratibu wa kupokea maoni na kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo kupitia mikutano na wananchi pamoja na katika mtandao wa http://mnyika.blogspot.com tutaendelea
nao. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.

Mheshimiwa Spika; Sekta za Nishati na Madini zina umuhimu maalum
katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi katika kipindi cha sasa na
muda mrefu ujao. Wakati nishati ikiwa nyenzo ya kuendesha maisha ya
kiuchumi, kisiasa na kijamii ya wananchi na nchi kwa ujumla; madini ni
mtaji na ni kati ya mitaji mikubwa ya kuwezesha maendeleo ya haraka ya
taifa. Hata hivyo, pamoja na Tanzania kujaliwa rasilimali hizi nyingi
ikiwemo watu, ardhi yenye rutuba, maji (bahari, mito na maziwa), kuwa
katika eneo la kimkakati la kijiografia kwa biashara na maliasili,
bado takwimu za hali ya uchumi kwa mwaka 2011 zinaonyesha sehemu kubwa
ya Watanzania wako kwenye lindi la umaskini.

Mheshimiwa Spika, tunajadili sekta za nishati na madini wakati taifa
likiwa kwa mara nyingine tena kwenye tishio la mgawo wa umeme pamoja
na serikali kukanusha kwamba hakutakuwa na mgawo wa umeme. Tunajadili
mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 wakati kwa mara
nyingine tena kukiwa na mvutano 3

baina ya watendaji waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na
Taasisi zake wakiwa katika mvutano ambao umeambatana na kutuhumiana
hadharani kupitia vyombo vya habari juu ya tuhuma za ubadhirifu na
matumizi mabaya ya madaraka. Tunajadili makadirio ya mapato na
matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2012/2013 wakati
kukiwa na tuhuma za vigogo wa serikali kuingiziwa fedha kifisadi
katika akaunti zao za nchini Uswisi na makampuni ya nje ya utafutaji
na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asili huku viongozi wa dini
wakiwa wamezindua ripoti juu ya ukwepaji kodi na upotevu wa mapato kwa
serikali unaogusa pia makampuni kwenye sekta za nishati na madini (The
One Billion Dollar Question).

Mheshimiwa Spika, namuomba kila mmoja wetu atafakari kwa ukweli wa
nafsi na nafasi yake tumefikaje hapa kama taifa na kwa pamoja
tukubaliane kuwa wabunge tuwajibike kuisimamia serikali kuhakikisha
maazimio yote ya bunge kuhusu sekta za nishati na madini ya miaka
mbalimbali yanatekelezwa kwa haraka na kwa ukamilifu. Naamini iwapo
maazimio ya Bunge juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya
Richmond Development Company LLC yangetekelezwa yote na kwa wakati
toka mwaka 2008, maazimio ya bunge juu ya uendeshaji wa sekta ndogo ya
gesi asili ya mwaka 2011 yangezingatiwa yote na kwa haraka, maazimio
kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha
fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011
yangechukuliwa 4

kwa uzito unaostahili; taifa lingeepushwa kurudia mijadala ile ile
kuhusu Wizara hii hii mara kwa mara. Aidha, kambi rasmi ya upinzani
inatoa mwito kwa bunge kupitisha maazimio ya kutaka uwajibikaji wa
serikali kwa kushindwa kutekeleza maazimio ya bunge kwa ukamilifu na
kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara ya 52 (1) Waziri
Mkuu ndiye mwenye madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa
siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano
na ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. Ni muhimu basi,
badala ya kupokea majibu ya Wizara ya Nishati na Madini pekee ambayo
imeendelea kugubikwa na lundo la tuhuma mbalimbali, Waziri Mkuu atoe
kauli bungeni kuhusu kujirudia rudia kwa madai ya ufisadi na uzembe
katika sekta za nishati na madini.

Aidha, pamoja na mabadiliko ya Mawaziri, Manaibu waziri, Makatibu
wakuu na Wakurugenzi wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake ya
mara kwa mara, Rais ashauriwe kutumia nguvu zake za kikatiba za ibara
ya 33, 34, 35 na 36 kuwezesha hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wote
waliotuhumiwa kwa ufisadi, uhujumu uchumi na matumizi mabaya ya
madaraka kwa mujibu wa maazimio ya bunge na taarifa mbalimbali za
serikali ili kurejesha misingi ya uadilifu na uwajibikaji katika sekta
za nishati na madini. 5

Mheshimiwa Spika, hivyo kwa ujumla mjadala wa mapitio ya utekelezaji
wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya
Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ulenge katika
kuliepusha taifa letu kuendelea kutumbukia katika ‘laana ya
rasilimali’ kama ilivyojitokeza katika mataifa mengine. Tuhakikishe
tunalinda uhuru wa taifa letu dhidi ya uporaji wa ardhi na rasilimali
zake yakiwemo madini, mafuta na gesi asili ulio katika tishio la
ubeberu mamboleo, ufisadi na udhaifu wa kimifumo. Aidha, kupitia
mchakato wa katiba mpya wananchi watoe maoni ya kuhakikisha kuwa
rasilimali za muhimu ikiwa ni pamoja na madini, mafuta na gesi
zinawekewa mfumo wa kunufaisha watanzania wote na pia mikataba kuhusu
rasilimali hizo inaridhiwa na Bunge.

Tuchangie mjadala wa sekta hizi nyeti tukikumbuka maneno ya hayati
Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE cha mwaka 1962,
nanukuu: "Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila binadamu
kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo
tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu,
hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au
yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi
tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu
ni ubinafsi mbaya sana" 6

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Julai 2011 niliwasilisha bungeni maoni ya
Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya
mwaka 2010/2011 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na
Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Kufuatia maoni hayo, yapo masuala
machache ambayo Serikali imeyazingatia kwenye utekelezaji na mengine
mengi serikali haikuyazingatia pamoja na umuhimu wake kwa maslahi ya
nchi na maisha ya wananchi. Hivyo kupitia mapitio haya ya utekelezaji,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze hatua ilizochukua juu
ya maoni hayo ambayo baadhi yalijitokeza pia kwenye maoni ya Kamati za
Kudumu za Bunge na michango ya wabunge kwa nyakati mbalimbali. Hakuna
sababu ya kutumia muda mrefu kutoa na kujadili maoni mapya ikiwa
hakuna mfumo thabiti wa kuhakikisha maoni na maazimio yanatekelezwa
kwa wakati na kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipitia kitabu cha pili cha
matumizi ya kawaida ya Wizara ya Nishati na Madini (Volume II Supply
Votes) Fungu la 58 kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na kubaini kwamba
ilikuwa ni bajeti ya mgawo mkubwa wa posho na ufujaji ya zaidi ya
shilingi bilioni 7.9 ya posho na matumizi mengine yasiyo ya lazima.
Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka serikali ifanye marekebisho kwenye
bajeti ili fedha hizo zipunguzwe na kuelekezwa kwenye kuongeza ujenzi
wa miundombinu wa Chuo Cha Madini Dodoma na kuongeza kiwango cha fedha
katika mfuko wa 7

wachimbaji wadogo wa madini. Aidha, yako matumizi mengine ya ujenzi wa
maofisi na gharama kubwa za kisheria yaliyopaswa kuhamishiwa katika
miradi muhimu ya maendeleo ikiwemo ya umeme vijijini. Kwa kuwa Wizara
iliahidi kuufanyia kazi ushauri wa kupunguza matumizi yasiyokuwa ya
lazima, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza kiwango cha
fedha kilichookolewa kutokana na kutekeleza ushauri huo na kutoa pia
maelezo ni kwanini katika makadirio ya mwaka 2012/2013 pamejitokeza
kwa mara nyingine tena matumizi yasiyokuwa ya lazima.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka kiwango cha bajeti
ya Wizara ya Nishati na Madini kuongezwa ili vipaumbele vifuatavyo
viweze kuzingatiwa kwa uzito unaostahili: Kuwekeza fedha za kutosha
kwenye sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya
Umeme na kupunguza gharama za maisha. Hatua hizo ziambatane na
kuwekeza katika Bomba la Gesi, pamoja na ujenzi wa mtambo wa
kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant) ili kuwezesha gesi kutumika
kwenye magari, viwandani na majumbani; kuhakikisha tunazalisha 360MW
za umeme kila mwaka ili kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa
miaka Mitano na kumaliza tatizo la mgawo wa umeme na mwisho kutenga
fedha za kutosha kwa ajili ya usafirishaji na usambazaji wa umeme
vijijini ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi vijijini.

Kusuasua kwa utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme 8

Mheshimiwa Spika, ili kushinikiza nyongeza hiyo ya bajeti na
utekelezaji wa vipaumbele hivyo, Kambi Rasmi Bungeni ilipendekeza
bunge kupitisha azimio la kutangaza kwamba ukosefu wa nishati ni janga
la taifa na kupitisha mpango wa dharura na maamuzi ya hatua za haraka
ambazo serikali inapaswa kuzichukua kwa uwajibikaji wa pamoja. Tarehe
18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikubaliana na mapendekezo
yetu na hivyo wakati anatoa hoja ya kuahirisha majumuisho ya mjadala
wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini
akaahidi kwenda kukata fedha kwenye posho na matumizi mengine
yasiyokuwa ya lazima katika bajeti ya serikali ili kuelekeza fedha
kwenye mradi wa dharura wa umeme.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo inaelekea ahadi hiyo ilikuwa hewa kwani
tarehe 13 Agosti 2011 Serikali ikageuka na kuleta mpango wa dharura
tofauti ambao ulijikita katika serikali kuidhamini TANESCO kwenda
kukopa kwenye mabenki ya kibiashara zaidi ya bilioni 400. Pamoja na
kuikumbusha serikali bungeni kutekeleza ahadi hiyo ya Waziri Mkuu,
serikali ilipuuzia ushauri uliotolewa. Matokeo yake mpaka sasa Shirika
la Umeme (TANESCO) halikuwezeshwa kupata kiwango cha fedha
kilichopangwa na utekelezaji wa mipango husika kusuasua.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba Mpango wa Dharura 9

ulipowasilishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011 serikali ilieleza kuwa
imepanga kuongeza MW 572 ifikapo mwezi Disemba 2011. Kati ya hizo, MW
150 ilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano baina ya Shirika la Hifadhi
ya Jamii (NSSF) na TANESCO; ilitarajiwa kuzalishwe MW 50 Septemba, MW
50 Oktoba na MW 50 Novemba 2011. Kimsingi, kauli iliyotolewa bungeni
kuwa mitambo ilikuwa imepatikana haikuwa ya kweli. Hivyo, ahadi ya
kupata umeme huo ilikuwa hewa. Mpaka sasa hakuna hata MW moja ambayo
imezalishwa kwa ushirikiano kati ya NSSF na TANESCO. Ujumbe ulipotumwa
Marekani kwenda kuona mitambo iliyokuwa inaelezwa kwamba ipo haikukuta
mitambo yoyote, walikuta kampuni ambayo haikuwa na uwezo kama
ilivyokuwa kwa Richmond Development LLC; timu hiyo ya wataalamu
ilibidi kwenda Ufaransa nako ikakosa mitambo ya dharura. Hivyo, fedha
nyingi za umma zimetumika kufuatilia ahadi hewa na umeme mpaka sasa
haujapatikana na taifa limerejea kwenye utegemezi wa mitambo ya kukodi
ya gharama kubwa ya umeme kwa sababu ya udhaifu na uzembe wa
kiutendaji. Hivyo, si kweli kwamba mpango wa dharura wa umeme
umetekelezwa kwa mafanikio ya asilimia 64.5 kama inavyodaiwa na
Serikali kwa kupunguza lengo lilopitishwa bungeni, bali mpaka sasa
umetekelezwa kwa asilimia 47.6 tu; katika muktadha huo, serikali
inabidi ieleze kwa ukweli ni kwa vipi mgawo wa umeme utaepukwa kwa
kuzingatia pia barua ya Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO kwa Rais yenye
kueleza uwepo wa tishio la mgawo wa umeme. 10

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine upungufu wa umeme unaojirudia
rudia matokeo ya serikali kushindwa kutekeleza kwa wakati mpango wa
kuweka mitambo ya MW 100 Ubungo (Dar es salaam) na MW 60 Nyakato
(Mwanza) ambayo iliwekwa kwenye mpango wa umeme wa mwaka 2009 ambao
ulicheleweshwa na hatimaye wakati wa Bajeti ya mwaka fedha 2010/2011
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini wote waliahidi kukamilisha
uwekaji wa mitambo hiyo mapema mwaka 2011. Hata hivyo pamoja na miradi
hiyo kuingizwa kwenye mpango wa dharura tarehe 13 Agosti 2011 hakukuwa
na usimamizi thabiti wa kufanya ikamilike kwa wakati. Kuzinduliwa kwa
mtambo wa MW 100 Ubungo katika mwaka wa fedha 2012/2013 ni hatua ndogo
kwa kuzingatia kwamba, ilipaswa mwaka wa fedha 2011/2012 pekee taifa
liongeze jumla ya MW 360 toka kwenye mitambo ya kununua na si ya
kukodi ili kuendana na malengo ya mpango wa taifa wa miaka mitano.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze sababu za kuchelewa
kutekelezwa kwa miradi hiyo na hatua za uwajibikaji zilizochukuliwa
kutokana na udhaifu huo.

Kashfa ya Ununuzi wa mafuta ya kufua umeme

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tulitahadharisha kwamba
mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta 11

kwa ajili ya kufua umeme isitumike kama mwanya wa ufisadi na kuzalisha
"Richmond nyigine". Inaelekea kansa hii ndani ya Serikali inayoongozwa
na CCM ya kuachia dharura ziendelee kwa manufaa ya wachache imesambaa
kwa kiwango cha kuwa vigumu kutibika isipokuwa kwa mabadiliko ya mfumo
mzima wa utawala. Katika siku za karibuni kumekuwapo na malalamiko
kutoka kwa wazabuni ambao wamekosa zabuni ya kuiuzia TANESCO mafuta ya
kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL kutokana na uamuzi wa Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wa kuipatia zabuni
kampuni ya PUMA Energy (Tz) Ltd. (zamani ikiitwa BP (Tz) Ltd.) ambayo
inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 50. Licha ya malalamiko ya
wazabuni hao, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba kuna
kampeni kubwa imefanywa na inaendelea kufanywa ndani na nje ya Bunge
hili tukufu ili uamuzi huu wa Katibu Mkuu Maswi ubatilishwe kwa
maslahi ya makampuni hayo na wapambe wake wa ndani na nje ya Bunge
lako tukufu. Aidha, wanaoendesha kampeni hiyo wanashinikiza Katibu
Mkuu Maswi ajiuzulu kwa kile kinachoitwa kitendo chake cha kukiuka
Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa nyaraka ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inazo, tarehe 10 Juni, 2011 aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa
TANESCO William Mhando alimwandikia Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Ufilisi, Vizazi na Vifo (RITA) – iliyokuwa 12

inasimamia ufilisi wa IPTL – kumtaka aendeshe mitambo ya IPTL ili
kufua MW 100 za umeme ili kuweza kuondoa mgawo wa umeme uliokuwa
unaendelea sehemu mbalimbali nchini. Nyaraka hizo zinaonyesha kwamba
mara baada ya kupata barua hiyo, tarehe 24 Juni 2011, Mtendaji Mkuu wa
RITA alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Manunuzi ya Umma (PPRA) akimwomba mwongozo na ushauri juu ya utaratibu
wa manunuzi ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kwa dharura.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA alitoa mwongozo kwa RITA kwa barua yake ya
tarehe 28 June, 2011 ambapo aliielekeza RITA itumie mamlaka yake chini
ya kanuni ya 42 ya Kanuni za Manunuzi ya Umma zinazohusu Bidhaa, Kazi
na Huduma zisizokuwa na Ushauri Elekezi na Mauzo ya Mali za Umma kwa
Tenda, Gazeti la Serikali Na. 97 la mwaka 2005 (Public Procurement
(Goods, Works, Non-Consultant Services and Disposal of Public Assets
by Tender) Regulations, Government Notice No. 97 of 2005). Kanuni hiyo
inamruhusu Afisa Masuhuli kuamua namna ya kufanya manunuzi kwa dharura
bila kujali mipaka ya mamlaka yake endapo kwa kufanya hivyo
kutahakikisha uchumi na ufanisi wa manunuzi hayo na endapo ataona ni
kwa manufaa ya umma kwamba bidhaa au kazi zenye thamani inayozidi
mamlaka yake zinunuliwe kama suala la dharura. 13

Mheshimiwa Spika, baada ya kupata mwongozo huo wa PPRA, Mtendaji Mkuu
wa RITA alimwandikia Katibu Mkuu Maswi barua ya tarehe 18 Julai, 2011
kumweleza kwamba katika makampuni matano yaliyoonyesha nia ya kuiuzia
IPTL tani 500 za mafuta kwa siku zilizokuwa zinahitajika kuendeshea
mitambo yake kwa mwezi Julai, 2011, kampuni za OilCom na Shell
hazikuwa na akiba ya mafuta wakati ambapo kampuni ya Mogas ilikuwa na
lita laki tatu tu. Kwa upande mwingine, kampuni ya Oryx ilikuwa na
tani 6,000 lakini ilikuwa inauza mafuta hayo kwa dola za Marekani
1,069.30 au shilingi 1,668,456.02 kwa tani. Aidha, kampuni ya BP (sasa
Puma Energy) ilikuwa na tani 9,000 na ilikuwa tayari kuuza mafuta hayo
kwa dola za Marekani 901.02 au shilingi 1,405,864.77 kwa tani. Kwa
kuzingatia maelezo hayo, Katibu Mkuu Maswi alitoa ridhaa kwa RITA
kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka kwa kampuni ya BP
kwa bei iliyotajwa hapo juu.

Mheshimiwa Spika, licha ya ukweli kwamba mafuta ya BP yalikuwa na bei
ndogo ikilinganishwa na bei ya Oryx, tarehe 27 Septemba, 2011
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alisaini mkataba wa kununua mafuta
kutoka Oryx kwa bei ya dola za Marekani 926.98 au shilingi
1,501,707.60 kwa tani. Aidha, wiki moja kabla ya hapo, yaani tarehe 21
Septemba, Mkurugenzi Mtendaji huyo alikwishasaini mkataba mwingine na
kampuni ya Camel Oil kwa bei ya dola za Marekani 905.24 au shilingi
1,466,488.80 kwa tani. Kama 14

inavyoonekana, mikataba yote miwili ilikuwa na gharama kubwa zaidi kwa
tani kuliko bei ya BP. Hata hivyo, mkataba wa BP ulikatishwa na
TANESCO ikaanza kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka
kwa makampuni ya Oryx na Camel Oil.

Mheshimiwa Spika, kitu cha ajabu ni kwamba licha ya mikataba ya
makampuni ya Oryx na Camel Oil kuonyesha bei za shilingi 1,501.70. na
shilingi 1,466.49 kwa lita, TANESCO ilianza kununua mafuta ya
makampuni hayo kwa shilingi 1,850 kwa lita! Kwa maana hiyo, kwa
mikataba ya kununua jumla ya lita 16,110,000 kwa mwezi kutoka kwenye
makampuni hayo, TANESCO ilikuwa inayalipa makampuni hayo jumla ya
shilingi 29,803,500,000 kwa mwezi. Kwa ulinganisho, mafuta yaliyouzwa
na BP kwa mkataba na RITA yaliigharimu Serikali shilingi bilioni
13,140,000,000 kwa bei ya shilingi 1,460 kwa lita. Hii ndio kusema
kwamba kama TANESCO ingeendeleza mkataba na BP badala ya kuuvunja,
gharama ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL ingekuwa shilingi
23,520,600,000 na hivyo TANESCO ingeliokolea taifa shilingi
6,282,900,000 kila mwezi!

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine kumekuwa na taarifa nyingi
kwenye vyombo vya habari kwamba Mkurugenzi Mtendaji Mhando hakutendewa
haki aliposimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi juu ya utendaji kazi
wake. Nyingi ya taarifa hizo zimetolewa bila kuwa na faida ya
kuangalia nyaraka zinazohoji 15

uadilifu na uaminifu wa Mkurugenzi Mtendaji Mhando.

Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi Mkuu Mhando ni mkurugenzi na mwanahisa wa
kampuni binafsi inayoitwa Santa Clara Supplies Co. Ltd. ya Dar es
Salaam. Wakurugenzi wengine ni mke wake Eva Martin William, ambaye ni
Mkurugenzi Mtendaji, na watoto wao. Kwa mujibu wa taarifa ambazo Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo, mnamo tarehe 20 Desemba, 2011, Santa
Clara Supplies iliingia mkataba na TANESCO ambapo Santa Clara Supplies
ilikubaliwa kuwa mgavi wa vifaa vya ofisini vya TANESCO kwa gharama ya
shilingi 884,550,000. Mkataba huu ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji
Mhando kwa niaba ya TANESCO na mkewe Eva Martin William kwa niaba ya
Santa Clara Supplies. Aidha, barua ya TANESCO iliyoitaarifu Santa
Clara Supplies kwamba imepatiwa zabuni hiyo iliyoandikwa tarehe 24
Novemba, 2011 ilisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mhando.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaelekeza
kwamba "… kiongozi wa umma hatajiweka katika hali ambayo maslahi yake
binafsi yatagongana na wajibu wake kama kiongozi wa umma." Aidha, "…
kuhusiana na uwazi kwa wananchi, viongozi wa umma watawajibika
kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha shughuli zao binafsi kwa
namna ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi na umma na
haitatosheleza kwao 16

kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu." Vile vile, "… kuhusiana
na utoaji wa maamuzi, viongozi wa umma watatekeleza wajibu wao
kufuatana na sheria na kwa maslahi ya umma." Zaidi ya hayo, "…
kuhusiana na maslahi binafsi, viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi
binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali
wanayoshiriki katika kuyafanya." Mwisho, "… kuhusiana na maslahi ya
umma, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa, viongozi wa umma watapanga
masuala yao kwa namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi,
iliyojificha au inayoonekana kuwepo na pale ambapo migongano hiyo
inatokea kati ya maslahi binafsi na maslahi ya umma basi itatatuliwa
kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma."

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ushahidi huu wa maandishi, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mbunge yeyote wa chama chochote cha
siasa chenye uwakilishi ndani ya Bunge lako tukufu, anayefuata imani
yoyote ya dini aseme kama, kwa mujibu wa vifungu hivi vya Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, Mkurugenzi Mtendaji Mhando ana sifa za
kuitwa kiongozi mwadilifu wa umma. Hivyo, pamoja na uchunguzi wa
kawaida unaoendelea, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka
Mkurugenzi wa Mashtaka aamuru hatua za uchunguzi wa kijinai
zichukuliwe dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji Mhando kuhusu tuhuma za
ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. 17

Mheshimiwa Spika; hata hivyo hatua hizo dhidi ya Mkurugenzi wa TANESCO
na watendaji waliohusika zisigeuzwe kuwa kafara ya kuficha uzembe na
udhaifu wa Serikali kwa ujumla wake kwa kuwa taarifa za utendaji wa
TANESCO kuhusu mpango wa dharura wa umeme pamoja na ununuzi wa mafuta
uliokuwa ukifanyika zilikuwa zikiwasilishwa kwenye vikao vya Wizara ya
Nishati na Madini na hata vikao vya baraza la mawaziri. Hivyo, ili
ukweli wa kina uweze kujulikana Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza
kuwa bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza masuala
yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za
ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa
mafuta wa ajili ya mitambo ya umeme. Uchunguzi huo uhusishe pia
mkaguzi mkuu kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa
malipo yaliyofanywa na makampuni ya BP (Sasa PUMA Energy), Oryx na
Camel Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali
waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme. Izingatiwe kwamba
masharti ya ibara ya 27(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inamtaka kila mtu "… kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi
na ya pamoja (na) kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu….".

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani tuliitaka Serikali katika
mwaka wa fedha 2011/2012 itoe taarifa kuhusu utekelezaji wa 18

mpango wa uboreshaji wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) sanjari
na kutoa ripoti ya tathmini ya utekelezaji wa mpango maalum wa
kurekebisha hali ya kifedha ya shirika (2006-2010). Hata hivyo, katika
mwaka husika wa fedha utendaji wa TANESCO na hali yake ya kifedha
imeendelea kususua huku ukigubikwa na tuhuma za ubadhirifu na udhaifu
wa kiutendaji hali ambayo imepelekea pia mkurugenzi mtendaji na
maafisa wengine waandamizi kusimamishwa na kuchunguzwa. Kambi Rasmi ya
Upinzani inaona kwamba hali hii ni matokeo ya udhaifu katika uteuzi na
usimamizi wa serikali kwa mashirika ya umma na inataka uwajibikaji
kutokana na hali hiyo kudumu kwa muda mrefu. Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka serikali iwaeleze watanzania ni mikataba mingapi mibovu yenye
kuipa mzigo mkubwa wa kifedha TANESCO na kuongeza gharama kwa wananchi
imefanyiwa mapitio katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, udhaifu wa kutokutekeleza
mipango ya uzalishaji wa gesi na makaa ya mawe kwa wakati umesababisha
utegemezi mkubwa kwenye matumizi ya mafuta katika mitambo ya kuzalisha
umeme wa dharura. Takribani nusu ya umeme unaozalishwa nchini hivi
sasa unazalishwa kwa kutumia dizeli, mafuta ya ndege na mafuta mazito
hali ambayo imeongeza mahitaji makubwa ya uagizaji wa mafuta toka nje
ya nchi. Hii imesababisha mahitaji makubwa ya fedha za kigeni kwa
ajili 19

ya kuagiza mafuta na hivyo kuchangia katika kuporomoka kwa thamani ya
shilingi. Aidha, ongezeko kubwa la uagizaji toka nje limeathiri urari
wa biashara na hivyo kuchangia katika mfumuko wa bei. Hivyo,
Watanzania hivi sasa wanabeba mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa na
gharama za maisha kwa ujumla kutokana na ufisadi kwenye mikataba,
ubadhirifu katika matumizi, uzembe katika uongozi na upungufu katika
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwenye sekta ya nishati.

Mheshimiwa Spika, mzigo huu usingekuwa mkubwa iwapo Serikali
ingetekeleza katika mwaka wa fedha 2011/2012 maoni ya Kambi Rasmi ya
Upinzani ya kuhakikisha nyongeza ya fedha kwenye bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini kwa upande wa sekta ndogo ya Gesi kwa ajili ya
mitambo ya umeme na kuharakisha kuwekeza katika Bomba la Gesi pamoja
na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant).

Kutokana na hatimaye Serikali kuzindua ujenzi wa Bomba la gesi katika
mwaka wa fedha 2012/2013 na ahadi ya Wizara ya Nishati na Madini kuwa
ujenzi huo utakamilika katika kipindi cha miezi kumi na nane ijayo,
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali kutoa kauli ya uhakika kwa
taifa; je, katika kipindi hiki cha mpito imeweka mikakati gani ya
kuhakikisha mitambo ya kufua umeme iliyopo inayotumia gesi itapata
gesi inayohitajika kuliondoa taifa katika upungufu wa 20

umeme.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012 tuliitaka Serikali
iache kutoa kisingizio cha ‘ufinyu wa bajeti’ katika kutekeleza maoni
na mapendekezo ya kuongeza fedha za Miradi ya maendeleo ya sekta za
nishati na madini na tulipendekeza vyanzo vya nyongeza vya mapato kwa
ajili ya sekta tajwa ikiwemo: kupunguza misamaha ya Kodi ikiwemo
kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa Kampuni za Madini peke hatua
ambayo ingeongeza mapato ya mapato ya shilingi bilioni 59; Kutoka
Vyanzo vipya vya mapato tulivyovianisha; kwa upande wa sekta ya madini
kwa kurekebisha kodi sekta ya madini peke yake tungeweza kukusanya
shilingi bilioni 240 katika mwaka wa fedha 2011/2012. Kambi rasmi ya
Upinzani inataka maelezo toka kwa Serikali ni kwa kiwango gani ushauri
huo umezingatiwa.

Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu
makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 ulionyesha uwezo mdogo
na kasi ndogo ya kufikisha umeme vijijini kwa upande wa Wakala wa
Umeme Vijijini (REA). Kasi ndogo ya kusambaza umeme ilielezwa pia
mijini kutokana na idadi kubwa ya maombi ya wananchi wanaotaka
kufungiwa umeme huku Shirika la Umeme (TANESCO) likiwajibu kuwa halina
uwezo kwa sasa mpaka lipate miradi. Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka
ufanyike ukaguzi wa kiufanisi kuhusu utekelezaji wa miradi ya
usambazaji wa umeme; hivyo, 21

serikali inapaswa kueleza iwapo ukaguzi husika ulifanyika na hatua
zilizochukuliwa na serikali katika kuongeza kasi ya usambazaji wa
umeme.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze
katika mwaka wa fedha 2011/2012 imetekeleza kwa kiwango gani mkakati
wa kupunguza gharama za manunuzi na pia kupunguza kiwango cha uagizaji
wa nguzo na vifaa vingine kutoka nje ili kutumia rasilimali za ndani
ili kuchangia katika kukuza uzalishaji na uchumi wetu. Izingatiwe
kwamba malalamiko yameendelea kuhusu mazingira ya kupitishwa kwa
zabuni za ununuzi wa nguzo, transforma na nyaya za umeme kwa kiwango
kikubwa toka nje ya nchi huku viwanda vya ndani mathalani TANALEC ABB,
East African Cables (hususani kampuni tanzu ya Tanzania Cables) na
vingine vikididimia. Hali hii imesababisha pia kukwama kwa
utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya kusambaza umeme kutokana kwa kile
kinachoelezwa kuwa ni vifaa kutokupatikana kwa wakati toka nje ya
nchi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imesikitishwa na kasi ndogo
ya serikali wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/212
kuhusu kupunguza gharama wanazotozwa wananchi za kuunganishiwa huduma
ya umeme suala ambalo linapunguza kasi ya uunganishwaji wa umeme. Bado
tumeendelea kupokea malalamiko toka kwa wananchi wanaotakiwa na
TANESCO kulipia nguzo na gharama nyingine za kuunganishwa 22

umeme kwa viwango ambavyo ni vigumu kwa wananchi wa kawaida kumudu.
Hivyo, tunaitaka Serikali ieleze hatua za ziada inazokusudia kuchukua
pamoja na kutekeleza maoni yetu ya kutaka TANESCO ibadili mfumo wa
ankara ili kuruhusu kuingiza kwa mteja gharama hizo kidogo kidogo
katika kipindi hiki cha mpito. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani
inawahimiza wananchi kutumia Kanuni za Sheria ya Umeme zilizotolewa
kwenye gazeti la Serikali tarehe 4 Februari 2011 (GN 63) ambazo
kifungu cha nne kinaeleza namna mteja atakavyofidiwa na kampuni ya
usambazaji pale ambapo mteja anajigharamia mwenyewe kuvutiwa umeme ili
fursa hiyo iweze kutumika ipasavyo; hata hivyo kanuni hizo zinahitaji
pia kufanyiwa marekebisho kwa kuwa zimeweka mkazo katika fidia
kutolewa kutokana na malipo ya wateja wengine badala ya mapato ya
Shirika kwa ujumla wake.

Gesi Asilia

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Julai 2011 Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa
nchi yetu imejaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la
umasikini wa wananchi na kwamba taifa letu lina fursa ya kuwa nchi
kiongozi katika gesi Afrika na kushindana kimataifa ikiwa tutaweka
mstari wa mbele upeo, umakini na uadilifu katika sekta ya nishati
kuepusha laana ya rasilimali. Hata hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa
mwaka wa fedha 2011/2012 yanaonyesha bado serikali haichukui hatua
thabiti kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi katika sekta
ndogo ya gesi asili hivyo hatua za haraka zisipochukuliwa 23

katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kuendelea rasilimali inaweza kuwa
chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa taifa letu limekuwa likitegemea
mradi mkubwa wa Songosongo kwa shughuli za uendelezaji, uzalishaji, na
usafirishaji ambao uko chini ya Kampuni ya Songas. Hata hivyo, kampuni
ya Songas imeiajiri Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAT),
ambayo ni mshirika wa TPDC katika uzalishaji, usambazaji na ugavi wa
gesi asili. Kambi Rasmi ya Upinzani ilieleza bungeni tarehe 15 Julai
2011 kuhusu tuhuma za ufisadi na ukiukwaji wa mikataba katika sekta
ndogo ya gesi na kutaka kuundwa kwa kamati teule ya bunge kuchunguza
suala hilo. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilifanya
uchunguzi wa masuala husika na taarifa kuwasilishwa bungeni; hata
hivyo mpaka sasa maamizio ya bunge kufuatia taarifa hiyo
hayajatekelezwa kwa ukamilifu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kueleza ni kwanini mpaka sasa kiasi cha dola milioni 20.1
zilizopunjwa kifisadi hazijareshwa na serikali iache kutumia
kisingizio cha kuundwa kwa Timu ya Majadiliano (GNT) kuchelewesha
utekelezaji wa maazimio.

Mheshimiwa Spika, mradi mkubwa wa maendeleo ambao umepangwa katika
mwaka wa fedha ni ujenzi wa bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es
salaam ambapo kwenye kasma 3162 24

umetengewa kiasi cha shilingi 93,000,000,000 huku kiwango kingine cha
fedha za mradi huo kikitarajiwa kupatikana kutokana na mkopo kutoka
nje. Kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha
ya wananchi wa sasa na baadaye, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi
husika ili bunge liweze kuishauri na kuisimamia serikali kuanzia
katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa yanalindwa
katika hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za
uwekezaji huo mkubwa. Aidha, pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya
kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi
huo; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ni miradi ipi
inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa
mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo kuharakisha utekelezaji wa mradi wa
kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na MW 230 wa Somanga Fungu (Kilwa).

Mheshimiwa Spika, pamoja na ujenzi wa Bomba la Gesi, Kambi ya Rasmi ya
Upinzani inasisitiza mradi wa kujenga kiwanda cha kujaza gesi kwenye
mitungi (LPG) na mradi wa usambazaji wa gesi Dar es salaam pamoja na
mradi wa matumizi ya gesi kwenye magari inayotekelezwa na Shirika la
Petroli Nchini (TPDC) inapaswa kuongezewa rasilimali katika mwaka wa
fedha 2012/2013. Kuanza kwa utekelezaji wa mradi kwa ajili ya viwanda
vichache na Kaya 57 25

za eneo la Mikocheni ni hatua ndogo ukilinganisha na mahitaji; hivyo,
utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2012/2013 upanuliwe wigo ili kuhusisha
pia kuwezesha taasisi zingine mathalani Chuo Kikuu cha Dar es salaam
kuweza kuunganishwa katika mtandao wa matumizi ya gesi asili. Hatua
hii itapunguza pia matumizi ya umeme katika maeneo yenye kuweza
kutumia gesi na kubakiza umeme mwingine utakaoweza kutumika kwenye
maeneo ikiwemo ya viwandani yenye upungufu wa nishati mbadala.

Mafuta

Mheshimiwa Spika, taarifa za Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2011
mfumuko wa bei ya nishati na mafuta umeongezeka kwa asilimia 41.0 kwa
mwezi Disemba 2011 ikilinganishwa na asilimia 12.3 katika kipindi kama
hicho mwaka 2010. Kambi Rasmi ya Upinzani inarejea kusisitiza kwamba
(ukiondoa kupanda kwa bei ya chakula kunakotokana na kushuka kwa
uzalishaji na udhaifu katika usambazaji) chanzo kikuu cha hali cha
mfumuko wa bei ni ongezeko la bei ya nishati hususani mafuta, umeme na
gesi, hali ambayo imeshindwa kudhibitiwa kwa mikakati makini ya haraka
na kuelekea kuwa tishio kwa utulivu wa taifa kiuchumi, kijamii na
kisiasa.

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Julai 2011 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya
Upinzani iliitahadharisha Serikali kwamba muswada wa Sheria ya Fedha
uliopitishwa na bunge tarehe 22 Juni 2011 usingeweza 26

kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi kwa kuwa serikali haikupunguza
mzigo mkubwa wa kodi badala yake iliweka kipaumbele katika kupunguza
tatizo la uchakachuaji kwa kuongeza mzigo mkubwa wa kodi katika mafuta
ya taa. Matokeo yake ni kwamba katika mwaka wa fedha 2011/2012 kiwango
cha kodi kwenye bei ya mafuta ya petrol hakikupungua, kodi katika
dizeli ilipungua kwa kiwango cha shilingi 99 huku mafuta ya taa
yakiongezeka kodi kwa shilingi 358 kwa lita na kuongeza mzigo wa
gharama za maisha kwa sababu ya udhaifu wa serikali na vyombo vyake
katika kudhibiti uchakachuaji kwa kusimamia utawala wa sheria.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali ieleze ni
hatua zipi ambazo Serikali imechukua dhidi ya athari za kupanda kwa
bei ya mafuta ya taa kwa wananchi wa kipato cha chini na pia kwa hali
ya mazingira nchini kutokana na ongezeko la matumizi ya kuni na mkaa.
Aidha, ikiwa mkakati huu umeweza kudhibiti uchakachuaji Serikali
inatoa maelezo gani kutokana na kuwepo kwa malalamiko ya kuendelea kwa
aina nyingine za uchakachuaji, na ni kwa nini taifa liendelee kuingia
gharama za vinasaba vinavyowekwa na EWURA wakati inaelezwa kwamba
uchakachuaji umeweza kudhibitiwa baada ya kupandisha bei ya mafuta ya
taa?

Aidha, kama sehemu ya mchakato wa kupunguza gharama za mafuta kufuatia
mabadiliko ya kodi, tozo na mfumo wa uingizaji wa mafuta serikali
ieleze imefikia hatua gani katika mwaka wa fedha 27

2011/2012 kufanya mapitio ya mkataba baina ya EWURA na kampuni ya
Global Fluids International (T) Ltd kuhusu ufanisi na gharama za
kuweka vinasaba na kuleta vifaa maalum vya kupima ubora (XRF).

Mheshimiwa Spika, ukiondoa kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la
dunia na ukubwa wa kodi zinazotozwa na serikali bei ya mafuta inakuwa
juu kutokana na mfumo mzima wa uagizaji, usafirishaji, uingizaji,
uhifadhi na usambazaji. Mfumo uliopo unanufaisha makampuni makubwa
mengi yakiwa ya kigeni na wafanyabiashara wachache wa ndani pamoja na
baadhi ya viongozi wa serikali wasiokuwa waadilifu kwa kulinyonya
taifa na kuongeza gharama za maisha kwa Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Spika, hali hii ndiyo iliyokwamisha kwa miaka mingi kuanza
kwa mfumo wa uagizaji na uingizaji wa mafuta ya pamoja (Bulk
Procurement System) ili kupunguza gharama; hata hivyo hata baada ya
kuanza kwa utaratibu husika katika mwaka wa fedha 2011/2012 tija ya
kutosha ya mfumo huo haijapatikana kutokana na udhaifu wa kimfumo.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza sababu za
kutokurejesha hifadhi ya taifa ya kimkakati ya taifa ya mafuta
(National Strategic Oil Reserve) pamoja na kutokukamilisha mchakato
wote wa kufufua Kampuni ya Taifa ya Mafuta (COPEC) kinyume na ahadi ya
Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka 2011. Aidha, ni kwa nini serikali
haikununua hisa za kampuni ya BP kwa kiwango cha kuwa na umiliki wa
asilimia 100 28

(100%) ili kuongeza miundombinu ya uhifadhi na usambazaji wa mafuta
kwa uchumi na usalama wa nchi. Kwa upande mwingine, Wizara ya Nishati
na Madini ieleze hatua mahususi ilizochukua katika mwaka wa fedha
2011/2012 za kulinda maslahi ya nchi katika kampuni ya TIPER ambayo
serikali ina hisa 50% katika hatua za uingizaji na uhifadhi wa mafuta.

Mheshimiwa Spika, Ili kuongeza tija na ufanisi wa TPDC, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo kuhusu hatua zilizochukuliwa
kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 za kulifanyia marekebisho shirika hilo
ili kuwa na mamlaka itakayohusika na kutoa vibali kwenye leseni na
kusimamia uchimbaji wa mafuta na gesi na kampuni itakayoshiriki katika
biashara ya mafuta na gesi.

Madini

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa
katika mwaka 2011 thamani ya mauzo ya madini nje ilikuwa dola za
kimarekani 1,965.23 milioni ikilinganisha na dola za kimarekani
1,536.93 milioni mwaka 2010, sawa na ongezeko la asilimia 27.9. Hii
ilitokana na kupanda kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia. Hata
hivyo mchango kwenye pato la taifa umekuwa ni asilimia 3.3 tu miaka
karibu mitatu toka kutungwa kwa sheria mpya ya madini mwaka 2010.
Udhaifu wa Serikali katika kusimamia utawala wa sheria unapaswa
kuondolewa kwa bunge kupitisha maazimio ya kuisimamia serikali
kulinusuru taifa dhidi ya hali hii ambayo utajiri 29

wetu unaendelea kuondoka, kwa pamoja na hatua zingine, kuwezesha
mwingiliano baina ya sekta ya madini na sekta nyingine za kiuchumi
katika nchi.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza
hatua iliyofikia katika kuzingatia ushauri tulioutoa wa kutaka Wizara
ya Nishati na Madini ishirikiane na Wizara ya Fedha kuboresha mfumo wa
utoaji wa taarifa za malipo ya kodi kwa kampuni za madini ili malipo
ya kila kampuni na mchangunuo wake yafahamike kwa umma badala ya mfumo
wa sasa ambapo hurundikwa pamoja katika takwimu za idara ya walipa
kodi wakubwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali ieleze
hatua ilizochukua kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 katika kuongeza
kiwango cha mapato ikiwemo ya kodi kutokana na uchimbaji wa madini kwa
kutekeleza mikakati ya kupenya kuta za umiliki na mitaji (capital and
ownership structures) zilizojengwa kwa muda mrefu na makampuni ya
kimataifa kwa kutumia mianya ya udhaifu wa kisheria na ushawishi wa
kifisadi uliosababisha mikataba mibovu katika sekta ya madini nchini.

Mheshimiwa Spika, wakati umefika sasa kwa Serikali kuwasilisha bungeni
ripoti ya tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo ya tume/kamati
mbalimbali ambazo ziliundwa na serikali kwa nyakati 30

mbalimbali kwa kutumia fedha nyingi za walipa kodi lakini mapendekezo
yake bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake. Kwa miaka mingi Serikali
inazo taarifa za makampuni makubwa ya madini kutumia sehemu kubwa ya
uwekezaji wao kama mkopo (debt financing) na kutumia mianya hiyo ya
kisheria na kimikataba kuwezesha wamiliki na wanahisa kupata faida
mapema kuliko kuweka mtaji kwa kuwa riba ya mikopo huondolewa katika
kukokotoa kodi.

Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia tena kuitaka serikali iwaeleze
Watanzania ni trilioni ngapi za mapato tumezikosa kati ya mwaka 1995
mpaka 2010 katika kipindi cha miaka 15 ya kuachia mianya ya upotevu wa
mapato kwa kuruhusu asilimia kubwa ya mikopo kuwa mitaji. Aidha, ni
hatua gani zimechukuliwa kwa waliohusika kuliingiza taifa katika
mikataba mibovu iliyoruhusu makampuni hayo kujitangazia hasara kila
mwaka huku yakipata faida kubwa.

Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu tuna migodi mikubwa mbalimbali kati
yake sita ilianzishwa kati ya mwaka 1998 -2009 kwa ajili ya kuzalisha
dhahabu ambayo ni Golden Pride Mine (1998), Geita Gold Mine (2000),
Bulyanhulu Gold Mine (2001), North Mara Gold Mine (2002), Buhemba Gold
Mine (2002) na Tulawaka Gold Mine (2005), Buzwagi Gold Mine ( 2009).
Buhemba Gold Mine walifunga uzalishaji mwaka 2006 31

Mheshimiwa Spika, migodi yote hii waliwasilisha upembuzi yakinifu
serikalini kabla ya kuanza uzalishaji na kuonyesha kuwa watalipa kodi
ya makampuni (Corporate tax) lakini mpaka sasa ni michache tu ambayo
imeanza kulipa Shilingi Bilioni 32.18 kutoka Resolute Tanzania Limited
na Shilingi Bilioni 145.52 kutoka Geita Gold Mine Limited tu , pamoja
na makampuni haya kunufaika na kupanda kwa bei ya dhahabu kwenye soko
la dunia kwa zaidi ya mara tatu kuanzia mwaka 2002, na wakati huohuo
makampuni haya yakiendelea kuweka uwekezaji mkubwa kwenye miradi yao.
Kutokana na umuhimu wa sekta hii nitaeleza japo kwa kifupi kuhusiana
na baadhi ya migodi hiyo mmoja mmoja:

Mheshimiwa Spika, mgodi wa Bulyanhulu ambao mwanzoni ulitarajiwa kuwa
na maisha ya miaka 15 na walitarajia kuzalisha ounces 400,000 za
dhahabu kwa kila mwaka ila wamekuwa wakizalisha ounces 6.5 milioni za
dhahabu kwa gharama ya kuzalisha ounce 1 kwa dola 130. Aidha
walitegemea kuzalisha madini ya Shaba (Copper ) ounces 7.26 milioni na
madini ya fedha ounces 5 milioni na kwa sasa umri wa mgodi ni miaka 25
, yaani muda umeongezeka kwa kipindi cha miaka 10 zaidi. Mgodi wa
Bulyanhulu uliwekeza kiasi cha dola 550 milioni kwa mchanganuo wa kuwa
dola 300 milioni kwa uwekezaji wa awali kabla ya kuanza uchimbaji na
dola 250 milioni kwa shughuli za uendeshaji wa mgodi. Mgodi huu
ulitegemea kuzalisha kiasi cha dola 900 milioni kutokana na uchimbaji
na uuzaji wa madini ya shaba (copper) pekee na 32

mapato ya dhahabu yalikuwa yamewekewa ukomo wa dola 300 kwa ounce tuu
pamoja na kuwepo kwa badiliko la bei kwa zaidi ya mara tatu yaani sasa
ni dola 950 kwa ounce moja. Ilikadiriwa kuwa mrahaba wa asilimia 3
uliotegemewa kulipwa serikalini ni kiasi cha dola 58 milioni, na fedha
zilizopaswa kulipwa moja kwa moja serikalini zilikadiriwa kuwa ni dola
64 milioni ( mrahaba dola 58 milioni,mrahaba wa moja kwa moja –direct
dividend dola 2 milioni na kodi ya zuio ya dola 4 milioni). Mgodi wa
Bulyanhulu kwa sasa umeweza kuongeza hifadhi ya dhahabu kutoka tani
13.64 milioni na kufikia kiwango cha tani 36.05 milioni mwaka 2007
kiwango ambacho ni asilimia 90 zaidi ya kiwango kilichokadiriwa wakati
wa kusaini mikataba na kuanza uchimbaji. Mpaka mwaka 2007 mgodi huu
ulilipa kiasi cha dola 26.54 milioni kama mrahaba kwa serikali, na
hawajalipa kodi ya makampuni .

Mheshimiwa spika, kuhusu Mgodi wa Geita Gold Mine mgodi huu
ulianzishwa kwa gharama inayokadiriwa kuwa dola 152 milioni kwa ajili
ya uwekezaji wote ambao ulifanywa kabla ya kuanza shughuli za
uchimbaji na gharama za kuendeleza uchimbaji kwenye mgodi husika.
Mgodi hu ulikuwa umeweka malengo ya kifedha kwa bei ya dola 300 kwa
ounce na kuwa thamani halisi (NPV) ni dola 100 milioni,Net cash flow
dola 201 milioni, mrahaba dola 30 milioni,kodi ya makampuni dola 13
milioni,kipindi cha kurejesha gharama miaka 5 na gharama za uzalishaji
ni dola 181 kwa ounce. Kwa mwaka 2000 mapato halisi yalikuwa dola 14
milioni na hii ilitokana na ukweli 33

kuwa kulikuwa na uzalishaji mdogo, na pia bei iliyokuwa imetarajiwa ya
dola 350 kwa ounce haikupatikana ila ilikuwa dola 279.321 kwa ounce
moja. Mwaka 2004 mapato halisi yalikuwa zaidi ya mara nne ya matarajio
nah ii ilitokana na uzalishaji kuwa mkubwa na bei ya dhahabu
kuongezeka kwani likikuwa dola 409.271 kwa ounce ikilinganishwa na
ukadiriaji wa dola 350 kwa ounce uliokuwa umewekwa awali. Ila kwa
ujumla ni kuwa mapato halisi ya mgodi huu kuanzia mwaka 2001 yamekuwa
yakiongezeka mara dufu kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji na bei ya
dhahabu kuendelea kupanda kwenye soko la dunia. Mpaka mwaka 2007 mgodi
huu ulikuwa haujalipa kodi ya makampuni pamoja na uzalishaji
kuongezeka na kuwa mara mbili zaidi ya matarajio na bei ya dhahabu
kuwa kubwa mara tatu zaidi ya matarajio kwenye soko la dunia na hii
iliufanya mgodi huu mapato yake kuongezeka zaidi ya mara tatu na mgodi
uliendelea kutangaza kuwa unapata hasara na haujaweza kurejesha
uwekezaji uliofanywa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mkodi wa Tulawaka katika mgodi huu uwekezaji
uliofanywa ulikadiriwa kuwa ni dola 34.6 milioni na gharama za
uendeshaji zilitarajiwa kuwa dola 325 kwa uzalishaji wa ounce 1,
thamani halisi (NPV) Dola 9.507 milioni,net cash flow dola 29 milioni,
mrahaba dola 5.367 milioni na kipindi cha kurejesha gharama miaka
4(pay back period) na walitarajia kulipa kodi ya makampuni mwaka 2008
ya dola 2.8 milioni. Kwa mwaka 2004 hapakuwa na uzalishaji na hivyo
hapakuwa na mapato yeyote ila 34

kwa mwaka 2004-2007 mapato halisi ya mgodi huu yamekuwa asilimia 72.5
ya zaidi ya makadirio ya awali yaliyowekwa. Mpaka mwaka 2007 mgodi huu
haukuwahi kulipa kodi ya makampuni pamoja na ukweli kuwa uzalishaji
ulikuwa asilimia 7 chini ya matarajio ila mapato halisi yaliongezeka
kwa asilimia 72.5 zaidi ya matarajio yaliyowekwa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mgodi wa North Mara mpaka disemba 2007
ilikadiriwa kuwa kuna ounce 3.6 milioni ukilinganisha na zilizokuwa
zimetangazwa awali wakati mgodi unaanza uzalishaji kuwa ni 2.94
milioni ounce mwaka 2002 wakati wa ufunguzi rasmi wa mgodi. Mgodi huu
mpaka mwaka 2007 ulikuwa umebadilisha wamiliki kwa zaidi ya wamiliki 3
tofauti tofauti na ii inafanya kuwa ngumu sana kuweza kupata taarifa
halisi za mwenendo wa m,apato kutokana na kila mmiliki kuweka
utaratibu wake na kuanza upya kama vile hapakuwa na kilichofanywa na
mmiliki aliyemtangulia. Aidha wamiliki wa awali waliweza kuuza migodi
hii na kunufaika moja kwa moja bila serikali kupata chochote kutokana
na mauziano yaliyofanywa.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa hizi tunaweza kuelewa kuwa uzalishaji
halisi wa dhahabu kwenye migodi hiyo mitano kuanzia mwaka 1999 -2007
ulikuwa 8.388 milioni ounces ukilinganisha na matarajio yaliyowekwa
awali kuwa ni kuzalisha 6.882 milioni ounces ambacho ni asilimia 21.88
zaidi ya matazamio ya awali. Umri kwa 35

ajili ya uzalishaji wa migodi hii umeongezeka kwa wastani wa miaka 4
kwa kiwango cha chini na miaka 10 kwa kiwango cha juu, na hii
ilitokana na kugundulika kwa machimbo mapya ya dhahabu pamoja na
kuongezeka kwa teknolojia ya kisasa zaidi kwenye tasnia hii.

Mheshimiwa Spika, mapato halisi yaliyoweza kupatikana kutokana migodi
hii mitano mikubwa kwa kipindi hicho cha kuanzia mwaka 1999-2007
ilikuwa dola 3.8 bilioni ambazo ni asilimia 64 juu zaidi ya matarajio
yaliyowekwa wakati uwekezaji ukifanywa ambayo ni dola 2.3 bilioni
.Pamoja na mapato hayo ni kuwa fedha iliyolipwa serikalini kama
mrahaba ilikuwa dola 99.6 milioni tu kwa kipindi chote hicho. Kwa
migodi yote hiyo matarajio ya bei yaliyowekwa yalikuwa kati ya dola
300-350 kwa ounce wakati uhalisia ni kuwa bei ilipanda na kufikia
kiasi cha dola 950 kwa ounce 1.

Mheshimiwa wa Spika, mapitio yaliyofanywa na Mamlaka ya ukaguzi wa
madini (TMAA) kuanzia mwaka 2004-2008 nchini yalionyesha kuwa mgodi wa
TanzaniteOne Tanzanite Mine (TTM) umekuwa ukilipa mrahaba kwa kutumia
viwango vya awali vya makadirio ambavyo viliwekwa wakati mgodi huu
ukianzishwa nchini. Halikadhalika ripoti hiyo inaonyesha kuwa kampuni
hii imekuwa ikitoa taarifa za zisizokuwa za kweli juu ya mauzo
yaliyofanyika nchini na kwenye makampuni makubwa nje ya nchi ili
kuweza kukwepa kulipa mrahaba stahiki serikalini. Tathmini hiyo ya
ukaguzi 36

inaonyesha kuwa kwa kipindi hicho kiasi cha dola 42.7 milioni
kiliongezeka zaidi kulingana na kiwango kilichotangazwa nchini na
kampuni hiyo. Hii maana yake ni kuwa kiasi cha dola 2.1 milioni
kilichopaswa kulipwa kama mrahaba serikalini hakikulipwa kama
inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ya madini kifungu cha 93 (the Mining
Act, Cap., 123) . Suala hili ni kwa mujibu wa barua iliyotumwa kwa
Meneja wa kamapuni ya Tanzanite one iliyoandikwa tarehe 02.10.2009
yenye Kumb.Na DA23/168/01 iliyoandikwa na aliyekuwa Kamishina wa
Madini Mhe.Dalali Kafumu akiwataka wawekezaji hao kulipa hata hivyo
deni hilo halikulipwa kwa wakati. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kueleza hatua ilizochukua huu ya kampuni hiyo. Aidha,
tunaitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu kuhamishwa kwa umiliki
wa kampuni hiyo kwa kuzingatia kwamba baada ya kutungwa kwa Sheria ya
Madini ya mwaka 2010 Serikali iliahidi kwamba uchimbaji katika eneo
hilo ungeachwa kwa wachimbaji wadogo wadogo.

Kambi ya Upinzani , inaitaka serikali kuweka hadharani ripoti na
taarifa zote zilizowahi kutolewa kuhusiana na uwekezaji katika
uchimbaji wa madini nchini kuanzia mwaka 1995 hadi 2010 na kama
serikali imefaidika na nini kutokana na uwekezaji huo.

Pili , tunahitaji mikataba yote iwekwe hadharani kwani kutokana na
taarifa hizi ni hakika kuwa mikataba yetu ni mibovu sana na
tunalipotezea taifa mapato mengi na hivyo kuendelea kudidimiza uchumi
wa taifa. 37

Tatu, Bunge liazimie kuwa mikataba yote mipya ya uchimbaji wa madini ,
mafuta na gesi lazima sasa iletwe Bungeni na kujadiliwa kwa maslahi ya
watanzania , kwani kama tukiendelea na utamaduni wa kusaini mikataba
husika kisirisiri taifa hili litaendelea kupoteza mapato kutokana na
uzembe na ufisadi kwa wanaohusika na mikataba

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuendelea kuporomoka kwa thamani ya
shilingi ya Tanzania, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kueleza hatua iliyofikiwa katika kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa
ya kutaka Wizara ya Nishati na Madini ishirikiane kwa karibu na Wizara
ya Fedha katika kuweka mikakati na usimamizi wa kuhusisha sekta ya
madini katika kuimarisha fedha yetu. Wakati umefika sasa wa kuwezesha
Benki Kuu kutunza sehemu ya hifadhi yetu ya fedha za kigeni katika
mfumo wa madini ya dhahabu. Hivyo Wizara ya Nishati na Madini
ishirikiane na Benki Kuu kuweka mfumo wa kununua dhahabu kwa
wachimbaji wadogo wadogo na pia kutoza sehemu ya mrabaha wa dhahabu
kwa ajili ya uhifadhi kama ilivyoshauriwa na Kambi Rasmi ya Upinzani
pamoja na kamati mbalimbali za bunge. Kambi Rasmi ya Upinzani
inasisitiza kwamba utaratibu huu uende sambamba na kusimamia mfumo wa
kuhakikisha kwamba makampuni hayo yanatunza sehemu kubwa ya fedha za
nje (walau 60%) kwenye benki za ndani ili kusaidia kudhibiti
kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania. 38

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 imeipa majukumu
muhimu STAMICO ya kuwa mwakilishi na msimamizi wa rasilimali za madini
nchini kwa niaba ya serikali. Mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa
fedha 2011/2012 yanadhihirisha kwamba majukumu haya muhimu ya kisheria
hayajawekewa mazingira wezeshi yakutosha ya kimfumo, kirasilimali na
kikanuni takribani miaka miwili tangu kutungwa kwa sheria husika.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuharakisha marekebisho ya
sheria ndogo (Establishment Order) iliyounda STAMICO ili kuendana na
mahitaji ya sasa na kuongeza mtaji wake ikiwemo kurejesha rasilimali
zilizochukuliwa ikiwemo majengo. Serikali izingatie kwamba sera
mkakati katika sekta ya madini iwe ni kuhakikisha Watanzania wana
umiliki katika miradi mikubwa ya madini ama kupitia hisa za makampuni
hayo kuwekwa katika soko la ndani (DSE) au kwa kampuni ya umma
kushikilia sehemu kubwa ya uwekezaji hasa katika madini nyeti ikiwemo
urani.

Mheshimiwa Spika, wwa kuwa katika mwaka wa fedha 2011/2012 Wakala wa
Jiolojia (GST) aliendelea na utekelezaji wa mradi wa kutambua maeneo
ya madini, Wizara ya Nishati na Madini ieleze iwapo utekelezaji wa
mradi huo ulienda sambamba na kufanya tathmini ya kina (mineral
appraisal) ya madini yetu ili kupendekeza mabadiliko ya kisheria na
kimikataba ambayo yatawezesha utajiri wa madini yetu kutumika kama
mtaji na dhamana katika hatua ya kuhakikisha taifa letu linanufaika na
rasilimali zake kama 39

ilivyopendekezwa na Kambi Rasmi ya Upinzani. Aidha, ni kiwango gani
cha mapato kilichopatikana kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kutokana na
kuiwezesha GST kutoza malipo kwa mujibu wa sheria ndogo (Establishment
Order) iliyounda wakala husika. Ili kulinda maslahi ya taifa kuhusu
matumizi ya ramani na ripoti za utafiti na uchunguzi huo katika mwaka
wa fedha 2012/2013 ukaguzi maalum (Special Audit) ufanyike kuhusu
mfumo wa utoaji leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini nchini ili
kudhibiti uporaji (grabbing) unaoendelea katika rasilimali muhimu za
taifa.

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Julai 2011 tulitoa tahadhari juu ya
maamuzi ya serikali ya kuendelea na hatua za mbele katika utafutaji na
uchimbaji wa madini ya urani bila kukamilisha maandalizi ya kisera,
kisheria, kikanuni na kitaasisi yanayohitajika suala ambalo linaachia
mianya ya upotevu wa mapato kwa taifa kama ilivyokuwa kwenye madini
mengine na pia linaweza kuhatarisha usalama. Aidha, Kambi ya Rasmi ya
Upinzani ilitaka maelezo ya kina kuhusu mauzo na mabadilishano ya
umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia (Mantra Resources)
na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato.
Mauzo hayo yamehusisha kuhamishiana umiliki wa maeneo ya Tanzania
Mkuju River (Mbamba Bay) na Bahi Kaskazini (Dodoma). Kambi Rasmi ya
Upinzani inatambua kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilifanya
ufuatiliaji juu ya suala hilo, hivyo Wizara ya Nishati na Madini
inapaswa kueleza kiasi gani cha fedha kimefanikiwa kupatikana na 40

ni hatua zipi Serikali imechukua kwa makampuni mengine ya madini,
mafuta na gesi asili yaliyofanya mauziano katika mwaka wa fedha
2011/2012.

Mheshimiwa Spika, licha ya ahadi ya serikali ya toka mwaka 2010 ya
kumaliza migogoro katika sekta ya madini baina ya wachimbaji wakubwa
na wachimbaji wadogo wadogo ikiwemo kudhibiti migongano kati ya wenye
leseni kubwa na leseni ndogo, migogoro hiyo imeendelea katika mwaka wa
fedha 2011/2012. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwasilisha
bungeni orodha ya maeneo yote yenye migogoro ya madini nchini pamoja
na ratiba ya utatuzi wa migogoro husika. Pia, pamoja na kuandaa
Mkakati wa Kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili mkakati huo usiwe maneno
matupu; Serikali iwasilishe pia mpango kazi na bajeti ya utekelezaji
wa mkakati husika. Aidha, Serikali ianzishe mfumo wa kisheria wa
kuwezesha wananchi waliokuwa wakilimiki ardhi katika maeneo yenye
madini kuweza pamoja na fidia ya mazao na maendelezo kuwa na hisa
katika umiliki wa migodi husika.

Mheshimiwa Spika, kufuatia kushamiri kwa migogoro baina ya wafanyakazi
na wawekezaji katika sekta ya madini, Kambi Rasmi ya Upinzani
inapendekeza Wizara ya Nishati na Madini iweke mfumo wa mashauriano na
Wizara nyingine ili kuharakisha utatuzi wa migogoro husika. Aidha,
kumekuwepo na wimbi la malalamiko ya wafanyakazi walioachishwa katika
migodi wa Bulyankulu, Kampuni ya Caspian katika mgodi wa Mwadui
Shinyanga , masuala ambayo 41

yanahitaji ushirikiano wa wizara na mamlaka mbalimbali katika
kuyashughulikia. Aidha, Wizara ya Nishati na Madini itoe maelezo
kuhusu taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 13 Aprili 2012 kuwa
wafanyakazi ikiwemo wa migodini kupitia vyama vyao walihusishwa kutoa
maoni yaliyopelekea kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits);
suala ambalo Chama Cha Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO) kimelikanusha.
Kwa kuwa ufafanuzi uliotolewa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa
Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa barua yenye Kumb. Na. AE/164/334/Vol II/2
umekataliwa katika migodi mbalimbali, Wizara ya Nishati na Madini
imechukua hatua gani kuepusha migogoro iliyoanza kujitokeza baina ya
wafanyakazi wa migodini na serikali kufuatia kupitishwa kwa vifungu
husika vya sheria vyenye kuagiza mafao kutolewa baada ya kufikisha
umri wa hiyari wa kustaafu wa miaka 55 au umri wa lazima wa miaka 60.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilihoji tarehe 15 Julai 2011
kuhusu tuhuma za Kampuni ya New Almasi (1963) Limited kuchimba almasi
kwa miaka 35 Mkoani Shinyanga licha ya muda wa leseni yake Na. 224
kwisha na leseni yenyewe kufutwa katika rejesta ya leseni za madini.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba mkataba kati ya New Almasi (1963)
Ltd uliingiwa kinyemela kwa lengo la kuwezesha uchimbaji wa almasi
kuendelea katika eneo hilo kinyume cha sheria na ili kuendeleza wizi
wa rasilimali ya nchi yetu. Mamia ya wananchi waishio maeneo jirani na
eneo la New Almas 42

wamekuwa wakinyanyaswa kwa miaka mingi na vyombo vya dola kama vile
polisi, mahakama na vyombo vya utawala kwa madai kwamba ni wavamizi wa
eneo la leseni ya New Almasi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali ieleze hatua ilizochukua kwenye mwaka wa fedha 2011/2012
kuichunguza kampuni hiyo, uhalali wa shughuli zake za uchimbaji almasi
katika eneo la Luhumbo, kiasi cha almasi iliyochimbwa kwa kipindi
chote tokea tarehe 1 Juni 1965 hadi tarehe 8 Mei 2000 na zilizokoenda
fedha zilizotokana na mauzo ya almasi hiyo. Aidha, Serikali ifafanue
utaratibu wa kisheria ambao uliiruhusu Williamson Diamond Ltd.
kuendelea kuchimba almasi katika eneo la Luhumbo pamoja na utata juu
ya uhalali wa leseni katika eneo hilo.

MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA
FEDHA 2012/2013

Mheshimiwa Spika, makadirio ya Matumizi na Mpango wa Bajeti ya Wizara
ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013, ni shilingi bilioni
641,269,000 ikilinganishwa na Shilingi 538, 514,071,000 zilizotengwa
wa Wizara mwaka 2011/2012 baada ya kufanyika kwa uhamisho wa fedha.
Bajeti hiyo imeongezeka kwa Shilingi 102,755,658,000 sawa na ongezeko
la asilimia 19, hata hivyo ongezeko hili ni dogo ukilinganisha na
mahitaji yaliyotajwa na Mpango wa Taifa wa miaka mitano. 43

Mheshimiwa Spika, makadirio ya mapato kwa upande wa makisio ya
makusanyo ya maduhuli kwa mwaka 2012/2013 ni Shilingi 193,007,543,000.
Kati ya makusanyo hayo, jumla ya Shilingi 173,702,263,000 zitakusanywa
na Idara ya Madini, Shilingi 19, 217,277,000 zitakusanywa na Idara ya
Nishati na Petroli, na Shilingi 88,003,000 zitakusanywa na Idara ya
Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu. Kambi Rasmi ya Upinzani
inataka Wizara ya Nishati na Madini ichukue hatua zaidi za kuongeza
mapato kwa kifungu cha 2001 cha Idara ya Madini Kasma 140101 ya Ada za
Madini na Kasma 140353 ya Mrabaha kwa pamoja; maeneo hayo yakiongezewa
usimamizi kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na
kanuni zake yana uwezo wa kulipatia taifa kiasi kisichopungua bilioni
200 katika mwaka wa fedha 2012/2013. Aidha, Wizara ya Nishati na
Madini itoe maelezo iwapo matarajio ya makusanyo katika Sekta ya
Nishati na Petroli kifungu cha 3001 hususani kasma 140274 yanajumuisha
marejesho ya mapato ya mauzo ya gesi asili yaliyopunjwa kati ya mwaka
2004 mpaka 2010. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali izingatie
kuwa mapato katika shughuli za TPDC za utafiti wa mafuta pamoja na
mauzo ya gesi asili yanaweza kabisa kuongezeka ziada ya makadirio ya
makusanyo ya bilioni 19 tu iwapo udhibiti katika gharama na ukaguzi wa
mikataba utaongezeka katika mwaka wa fedha 2012/2013. Pia ili kuongeza
mapato kwa serikali na TPDC Kambi Rasmi ya Upinzani inataka mrabaha wa
asilimia 12 kwenye 44

gesi uanze kutozwa kwa mujibu wa sheria na isitishe mara moja
utaratibu wa baadhi kuachiwa kutokulipa malipo husika kwa mujibu wa wa
sheria. Mapitio ya kitabu cha mapato yameonyesha kwamba wakati kwenye
kifungu cha 2001 cha madini kuna mrabaha hakuna kasma hiyo kwenye
kifungu 3001 kinachohusika na gesi na mafuta.

Mheshimiwa Spika; Matumizi ya Kawaida yanaombewa Jumla ya Shilingi
110,078, 868,000 kati ya fedha hizo shilingi 17, 292, 347,000 ni kwa
ajili ya mishahara (P. E) ya Wizara na Mashirika yaliyo chini yake na
Shilingi 92,786, 521, 000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC).
Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa rai kwa wabunge na bunge kuungana
pamoja kabla ya kupitisha matumizi haya makubwa ya kawaida kwenye
matumizi mengineyo pamoja na kuitaka Wizara ya Nishati na Madini
kubana matumizi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, Serikali
itakiwe kutoa maelezo ya kina kuhusu matumizi ya kifungu cha 1005 cha
Kitengo cha Sheria ambacho kina kasma ya 229900 ambayo kwa mwaka wa
fedha 2012/2013 kimetengewa kiasi cha Shilingi 4,000,000,000 kama
gharama za utetezi wa Serikali katika kesi ya IPTL ikiwemo kwa ajili
ya kuilipa kampuni ya Mkono &Co. Advocates . Izingatiwe kwamba katika
mwaka wa fedha 2011/2012 Serikali ilifanya uhamisho wa fedha wa kiasi
cha Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya gharama za kuendesha kesi
zilizopo mahakamani zinazoihusu Wizara. Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kueleza jumla ya fedha zilizotumiwa na Wizara kati
ya mwaka 45

1995 mpaka 2011 kwa ajili ya kulipa makampuni binafsi ya uwakili
kwenye kesi kubwa za kitaifa na za kimataifa pamoja na kutaja orodha
ya makampuni hayo. Aidha, Serikali ieleze mkakati wa kudhibiti
ongezeko la gharama za kisheria ambazo ni mzigo mkubwa kwa mashirika
ya umma na wananchi walipa kodi kwa kuwa yamekuwepo mazingira ya kesi
kuendelezwa kwa muda mrefu na kugeuzwa kuwa vitega uchumi vya watu
wachache. Mifano ya kesi zilizodumu kwa muda mrefu ni ya IPTL ambayo
Serikali inawakilishwa na Mkono and Co. Advocates na ile ya Dowans
ambayo Serikali imekuwa ikiwakilishwa kwa nyakati mbalimbali na Rex
Attorneys.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2011 Benki ya Standard Hong-Kong ambayo ni
mdeni mkuu katika sakata la IPTL ilifungua kesi ya madai katika
mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICSID case Na. ARB/10/20)
inayodai kiasi cha dola za Kimarekani milioni 225, pamoja na riba
katika kuendesha kesi hiyo. Katika muendelezo wa Serikali kampuni ya
uwakili ya Mkono ilipewa zabuni ya kuitetea Serikali katika shauri
hilo, na kwa kujiamini iliishauri Serikali kuwa kesi hiyo kama
Serikali tungeshinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na maoni
kinzani kuhusu suala hilo. Lakini kutokana na uroho na kutaka maslahi
binafsi kwa Kampuni ya Mkono inaishauri Serikali isifanye usuluhishi
nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai kupitia kwa Mfilisi wa Mali na
Madeni za IPTL wanakubali kusuluhishwa nje ya mahakama. 46

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliona hili kuwa
ni mchezo wa kuihujumu Serikali ambao umekuwa ukifanywa na makampuni
binafsi ya uwakili kuchelewesha kesi ili yeye aendelee kulipwa
mabilioni ya fedha za walipakodi. Huu ni uhujumu wa kodi za wavuja
jasho wa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, katika muendelezo huo huo Kampuni ya Mkono
&Advocates kwa sababu ya uzoefu wake wa kazi hiyo na ushawishi wake
mkubwa kwa viongozi wa Serikali imekuwa ni kawaida kwa kampuni hiyo
kuingia mikataba kuzitetea Kampuni za nje zenye kutiliwa shaka kama
ilivyo Kampuni ya matangazo inayotoka bara Asia inayojiita Asia
Business Channel inayodai kutengeneza matangazo ya biashara. Kampuni
hiyo yenye mwelekeo wa kutaka kutapeli ilitambulishwa kwa Mtendaji
Mkuu wa TMAA na Waziri wa Nishati kipindi hicho Mheshimiwa William
Ngeleja kwa barua yenye Kumb. Na. AB 88/233/01 ya tarehe 8 Desemba,
2011. Lengo lilikuwa ni TMAA kuingia mkataba wa kutangaza sekta yetu
ya madini nje ya nchi.

Katika biashara hiyo ya kulazimisha, kampuni hiyo iliitumia Kampuni ya
Mkono &Advocates kuandika barua ya kusudio la kuishtaki TMAA kama
itashindwa kuilipa kampuni ya ASIA BUSINESS CHANNEL kiasi cha paundi
za Kiingereza 35,500 kwa kazi ambayo majadiliano yalikuwa hayajafikia
hatua ya mwisho. Kambi ya Upinzani inajiuliza Kampuni hii kweli ni ya
wazalendo au ni ya watu ambao wanasukumwa na dhamira ya kufilisi
rasilimali za Watanzania? 47

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo ina mamlaka ya kuiwakilisha
Serikali katika kesi zote zinazoihusu Serikali ieleze imechukua hatua
gani kuhusu hali hii na ifungulie mashtaka Kampuni zote zenye
kuonyesha uzembe na hujuma katika kuishauri serikali kwenye kesi
mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinazohusu nishati na madini.

Mheshimiwa Spika, aidha, kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu itashindwa
kutekeleza hilo ni wazi Mshauri huyo Mkuu wa Serikali katika mambo ya
sheria atakuwa na yeye ameshindwa kazi na hivyo ni bora awape nafasi
watu wenye uwezo wa kuangalia na kusimamia maslahi ya umma.

Mheshimiwa Spika, Miradi ya Maendeleo imetengewa Jumla ya Shilingi
531, 190, 861,000 kati yake Shilingi 431,190, 861,000 ni fedha za
ndani na Shilingi 100,000,000,000 ni fedha za nje. Kati ya hizo
kifungu cha 2001 cha Madini kimetengewa katika Kasma 3152 Shilingi
240,000,000 tu tena za nje kwa ajili ya Uwazi katika Tasnia ya
Uziduaji (Tanzania Extrative Industries Transparency Initiatives
–TEITI) hivyo kutokana na umuhimu wa asasi hiyo katika kuweka mfumo wa
uwazi katika usimamizi na uvunaji wa rasilimali za madini, mafuta na
gesi asili ni muhimu kiwango cha fedha kikaongezwa na kuhakikisha
kwamba Sheria ya TEITI inatungwa katika mwaka wa fedha 2012/2013.
Aidha, Taarifa zote tatu za TEITI (Reconciliation Reports)
ziwasilishwe na kujadiliwa bungeni. Kwa upande mwingine, bunge
lisikubali kupitisha kiasi cha Shilingi 40,000,000,000 kinachoombwa 48

kwenye Kasma 3160 kwa ajili ya kulipia madeni ya Kiwira (KCPL) mpaka
uhakiki ufanyike juu ya uhalali wa viwango vya madeni husika kwa kuwa
mradi mzima uligubikwa na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya
madaraka.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Miradi ya Maendeleo ya Nishati na
Petroli kifungu cha 3001, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
itoe maelezo kuhusu sababu za kutekelezwa taratibu kwa mradi wa TEDAP
(Kasma 3132) ambao iwapo utaharakishwa utakuwa na mchango katika
kuboresha mfumo wa gridi pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati
jadidifu kama vyanzo mbadala katika uzalishaji umeme nje ya gridi.
Aidha, pamoja na nyongeza ya fedha za miradi ya maendeleo kwa ajili ya
Wakala pamoja na Mfuko wa Umeme Vijijini (REA/REF) (Kasma 3113); Kambi
Rasmi ya Upinzani inasisitiza umuhimu wa kuongeza kiwango cha fedha za
ndani ili kufikia bilioni 150 ili kuharakisha kasi ya uzalishaji na
usambazaji wa umeme vijijini. Pia, kutokana na kasi ndogo ya
usambazaji wa umeme, pamoja na kuondoa kodi katika vifaa vya umeme wa
jua, serikali ieleze hatua ilizochukua katika kuweka mazingira wezeshi
kwa vifaa vya umeme wa dharura kuweza kupatikana kwa urahisi mathalani
vifaa vya kuhifadhia umeme (invertors). Kupitia Kasma 3147 Wizara ya
Nishati na Madini inaomba 47,959,861,000 kwa mwaka wa fedha 2012/2013
kwa ajili ya kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya dharura, hivyo ni
muhimu maelezo yakatolewa kuhusu matumizi ya fedha za mafuta ya 49

mitambo ya dharura kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ili kujenga uhalali wa
matumizi ya mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini inaomba shilingi
62,000,000,000 kwa ajili ya Mradi wa Kuboresha Mifumo ya Umeme Katika
Jiji la Dar es salaam (Kasma 3154). Pamoja na mradi huo kuweka mkazo
katika kufunga transfoma kubwa zaidi na njia kubwa za umeme za msongo
wa kV 33 kwa ajili ya wateja wakubwa wa katikati ya Jiji; mradi uweke
mkazo pia katika usambazaji wa umeme pamoja na kuongeza nguvu ya umeme
katika maeneo ya pembezoni ya Jiji la Dar es salaam. Izingatiwe kwamba
matatizo ya miundombinu ya umeme katika Jiji la Dar es salaam
kutoendana na kasi ya ongezeko la mahitaji ya umeme hayapo katikati ya
jiji pekee bali pia yapo maeneo ya pembezoni yenye ongezeko la wakazi
na vitega uchumi mbalimbali. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na
Malambamawili, Kwembe, Goba Matosa, Msakuzi, King’ongo na mengineyo
katika Manispaa mbalimbali za Jiji la Dar es salaam. Aidha, Wizara
ieleze iwapo kiasi cha 10,000,000,000 kilichotengwa ajili ya kulipa
fidia wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayozunguka mitambo
ya kuzalishia umeme ya Ubungo kitatosha kukamilisha kazi hiyo kwa
mwaka wa fedha 2012/2013 ili kuepusha uwezekano wa gharama kuongezeka
kutokana na riba ya kuchelewa kufanya malipo kama ilivyotokea kwa
miaka iliyopita. 50

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kutokana na
Mpango wa Dharura wa Umeme uliopitishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011
Serikali imepanga kuanza utekelezaji wa miradi ya MW 240 Kinyerezi
ambao umetengewa shilingi 5,000,000,000 katika Kasma 3163 na MW 150
Kinyerezi ambao umetengewa shilingi bilioni 13,000,000,000 katika
Kasma 3164. Hata hivyo, kwa miradi yote hiyo Serikali iko katika hatua
ya majadiliano na kufunga mikataba ya mikopo na Kampuni za SUMITOMO na
Jacobsen wakati ambapo michakato ya miradi hiyo ilianza toka mwaka
2009. Kambi Rasmi ya Upinzani inarejea kuitaka Serikali kutangaza
matatizo ya nishati ni janga la taifa ili kuweka mfumo wa dharura wa
kushughulikia kwa haraka kwa usimamizi wa uongozi mkuu wa nchi tofauti
na sasa ambapo miradi hiyo inachukuliwa kuwa ni ya kawaida chini ya
Wizara ya Nishati na Madini. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka
uhakika toka kwa Serikali iwapo mitambo hiyo inayotarajiwa kutumia
gesi itakamilika lini na iwapo itapata nishati husika kwa wakati na
kwa uhakika kwa kuzingatia kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa bomba la
gesi. Pia, Serikali itaje miradi mingine ya nyongeza ambayo
utekelezaji wake unakusudiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2012/2013
ili kufidia pengo la mwaka wa fedha 2011/2012 na kuhakikisha kwamba
kila mwaka wastani wa MW 360 za mitambo isiyokuwa ya kukodi zinaingia
katika Gridi ya Taifa katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa
Taifa wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Taifa wa miaka mitano (2011/2012-51

2015/2016) umelenga kuongeza uzalishaji wa umeme mpaka kufikia MW 2780
kwa kuongeza MW 1788 kwa mujibu wa miradi iliyotajwa kwenye mpango
kipengele A.1.3 kuhusu nishati. Lengo hili ni dogo ukilinganisha na
rasilimali ambazo zipo katika taifa letu; hivyo Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kueleza imefikia hatua gani katika kufanya
mapitio ya mpango huo na kuongeza miradi mingine mikubwa ukiwemo wa
Stiggler Gorge ambao una uwezo wa kuzalisha MW 2100 kama
nilivyopendekeza bungeni tarehe 14 Juni 2011 na kuingiza pia makadirio
ya ujumla ya MW zinazotokana na miradi midogo midogo itakayoanzishwa
katika maeneo mbalimbali kama tulivyoshauri tarehe 15 Julai 2011.

Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza miradi iliyosalia kwa wakati Kambi
Rasmi ya Upinzani inarudia kuitaka Wizara ya Nishati na Madini kueleza
mazingira wezeshi ambayo yanakusudiwa kuandaliwa ili miradi ifuatayo
iweze kupata rasilimali kwa wakati na makubaliano kukamilishwa mapema:
Iringa-Mchuchuma na Ngaka (Makaa ya Mawe-300), Kiwira (MW 200) ,
Singida (Upepo) na Morogoro/Iringa- Ruhudji (Maji- MW 358).

Mheshimiwa Spika, ni aibu kwa taifa kuendelea kutegemea vyanzo ambavyo
vilianzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Hayati
Mwalimu Nyerere, na awamu zilizofuata sio tu zimeshindwa kuongeza kasi
ya kuzalisha umeme bali pia 52

zimeshindwa kukarabati mitambo hiyo na hivyo kuzalisha chini ya
kiwango. Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2010 ilionyesha kwamba
vituo vya kuzalisha umeme vilikuwa vikifua umeme kwa wastani wa 53.5
tu ya uwezo wake; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka pia Serikali
kueleza imechukua hatua gani kwa mwaka 2011/2012 na inapanga kuchukua
hatua gani za dharura kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kuhakikisha uwezo
wa vyanzo vilivyopo kuzalishaji unaongezeka sanjari na kupunguza
upotevu wa umeme kutokana na ubovu wa mifumo ya usafirishaji na
usambazaji.

Mheshimiwa Spika; ili kujiandaa kitaalamu kama taifa kwa mipango
kabambe ya gesi wakati nchi ikisubiri Sera ya gesi, Sheria ya Gesi na
Mpango Kabambe wa Gesi (Gas Master Plan) vinavyopaswa kuwasilishwa
katika Mkutano wa Tisa wa Bunge. Pia Kambi Rasmi ya Upinzani inataka
Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua iliyofikiwa katika
kukamilisha mtaala wa uhandisi wa gesi na mafuta ili fani hizo ziweze
kutolewa kwenye Chuo Cha Madini Dodoma. Aidha, wakati wa kuhitimisha
mjadala wa mpango wa mpango wa taifa wa miaka mitano tarehe 14 Juni
2011 serikali ilikubali pendekezo la kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara.
Hata hivyo hicho hakijaingizwa kwenye Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano
toleo la mwezi Juni 2012 kifungu cha A.1.5. Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kueleza ni hatua zipi zitaanza kuchukuliwa kwenye
mwaka wa fedha 2012/2013 na Wizara ya Nishati na Madini kwa
kushirikiana na mamlaka nyingine zinazohusika kuwezesha kuanzishwa kwa
Chuo 53

Kikuu hicho muhimu ambacho kitatoa mchango mkubwa kwa taifa katika
masuala ya mafuta na gesi na bidhaa zitokanazo na gesi na mafuta.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha sekta ya gesi na sekta kuwa na
manufaa kwa nchi yetu, narudia tena mapendekezo kama tulivyoyatoa
katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kama ilivyowasilishwa na
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika hotuba yake Ofisi ya Waziri Mkuu
nanukuu kama ifuatavyo:

"Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inatoa mapendekezo yafuatayo
katika kuimarisha na kuboresha sekta ya gesi na mafuta hapa nchini ili
kuitayarisha nchi kwa utajiri huu mkubwa:

i. Wananchi wanaozunguka maeneo yanayopatikana au yanayopitia gesi
asili wawe sehemu ya mipango ya maendeleo ya gesi asili na hivyo
kunufaika na matumizi ya gesi badala ya kuachwa, hali inayoleta
manunguniko na tishio la uendelevu wa sekta husika na haswa
ikizingatiwa kuwa uwekezaji unaofanywa katika sekta hii kama wananchi
hawataona kuwa na wao ni wafaidika ni rahisi sana kuweza kuhujumu
miundombinu hii na kuhatarisha usalama na hata uhai wa wananchi
wengine .

ii. Ujenzi wa miundombinu ya gesi uwe unazingatia mahitaji ya muda
mrefu ili kupunguza gharama na kuondokana na uhaba na uharibifu wa
maliasili, mfano bomba la Songosongo liliwekwa bila kuzingatia
mahitaji asili ya gesi na

54

hivyo kujikuta kuwa wanashindwa kusafirisha gesi ya kutosha kutumiwa
na wahitaji wote;
iii.
Tuwekeze kwenye kuwapa elimu na maarifa vijana wa Kitanzania na haswa
kwenye Sekta ya gesi ili waweze kupata utaalamu wa jinsi ya kusimamia
sekta hii kama ambavyo nchi majirani zetu wa Uganda na Msumbiji
wamefanya kwa kuwapeleka vijana wao nje ya nchi ili kupata utaalamu
juu ya uendeshaji wa sekta hii.

iv. Serikali iliahidi kwa Shirika la Fedha la Kimataifa kwamba Sheria
ya usimamizi bora wa Fedha za Mafuta na Gesi (Petroleum Revenue
Management act) italetwa Bungeni mnamo mwezi Novemba. Kambi ya
Upinzani inasisitiza kwamba Sheria hii iletwe haraka ili kuweka wazi
mapato yatokanayo na utajiri huu na namna bora ya kutumia fedha hizi
ili kuzuia uchumi kuathiriwa na pia kuzuia ufisadi. Hatutaki Tanzania
iwe kama nchi nyingine za Kiafrika ambazo utajiri wa Mafuta na Gesi
umekuwa ni laana badala ya Neema.


v. Serikali iweke mazingira bora ya kujenga uwezo wa Watanzania kutoa
huduma kwenye kila hatua ya utafutaji wa Mafuta na Gesi. Hivi sasa
kuna zaidi ya wageni 1200 kwenye Meli za kutafuta Mafuta na Gesi
katika Pwani ya Mtwara, Lindi na Pwani. Kwa masikitiko makubwa sana
wageni hawa wanakula hata nyanya, mchicha na vitunguu kutoka nje ya
Tanzania.

55 vi.
Vile vile tudhibiti makampuni ya Ulinzi kutoka nje kuwa na silaha kali
kali kwa kujenga uwezo wa Jeshi letu la Majini (Navy) ili liwe na
kikosi maalumu kwa ajili ya kulinda meli za kutafuta mafuta na Gesi na
Makampuni haya yatozwe tozo maalumu. Ni hatari sana makampuni ya
kigeni kuwa na masilaha makubwa ndani ya ramani ya nchi yetu".

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea
kusisitiza kwamba muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2012 uhakikishe
misamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za utafutaji wa mafuta na Gesi
inaondolewa. Izingatiwe kuwa uzoefu kutokana na misamaha ambayo
imekuwa ikitolewa kwa makampuni ya madini unadhihirisha kwamba
makampuni mengi yanatumia mwanya huo kuleta mafuta yasiyo na kodi na
kuyaingiza kwenye soko la ndani la reja reja. Hivyo, misamaha hii
haina maslahi kwa taifa na ni mianya mingine ya uhujumu uchumi kwa
kuwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi zinayo fursa kwa mujibu wa
mikataba (PSA) kurejeshewa gharama zao mara baada ya mafuta
kupatikana. Aidha, uamuzi huu uhusishe pia kampuni za madini bila
kujali mikataba (MDA) kwa kuwa imethibitika kampuni hizi zote
hutengeneza faida nono bila kulipa kodi inavyostahili.

Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti hali hii ya ukwepaji kodi na kuongeza
mapato ya serikali katika mwaka wa fedha 2012/2013 Kambi Rasmi ya
Upinzani inarudia kuitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze 56

hatua mahususi ambazo itazichukua kutekeleza mapendekezo yafuatayo:
kutunga Sheria ya kuhakikisha kwamba mikopo kwenye makampuni ya
uwekezaji wa madini katika mahesabu ya kodi isizidi 60% ya mtaji;
kutunga Sheria kuhakikisha kwamba riba ya mikopo kwenye makampuni
yanayohusiana haitaondolewa kwenye mahesabu ya kodi; kufanya
marekebisho ya sheria kuhakikisha kwamba kodi ya mtaji (capital gains)
inatozwa katika mauziano ya makampuni yote ya madini ambayo mali zake
au uwekezaji wake uko nchini hata kama mauziano hayo yamefanyika nje
ya nchi kwa kuzingatia kuwa mapendekezo yaliyoingizwa kwenye muswada
wa sheria ya fedha wa mwaka 2012 hayakuzingatia kwa ukamilifu msingi
wa mapendekezo yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani mwaka 2011.
HITIMISHO

Mheshimimiwa Spika; kambi rasmi ya upinzani inapenda kuhitimisha kwa
kusisitiza kwa mara nyingine kwamba kwa sehemu kubwa matatizo katika
sekta za nishati na madini yamechangiwa na sababu za kibinadamu za
kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa
viongozi wa kiserikali wenye dhamana na watendaji wengine na hivyo
kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi.
57

Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya kimfumo yanahitajika ili kuwezesha
hatua za haraka za kusimamia sera sahihi, uongozi makini na taasisi
thabiti katika sekta nyeti za nishati na madini sanjari na kuchukua
hatua kali dhidi ya ufisadi uliofanyika katika sekta hizi, kufanya
mapitio ya mikataba na kuharakisha utekelezaji wa mipango kwa
ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kuwashukuru wananchi wa Ubungo kwa
ushirikiano wao katika kazi nifanyazo za kuwawakilisha kwenye vyombo
vya maamuzi na kuhamasisha maendeleo Jimboni. Kwa namna ya pekee
nitambue mchango wa madiwani wote tunaoshirikiana katika kipindi
ninachokuwa kwenye majukumu mengine ya ujenzi wa taifa. Nawashukuru
viongozi wa dini washauri wangu wa kiroho na wanafamilia yetu ya
Dalali kwa upendo na kuniasa kuendeleza ujasiri na uadilifu katika
kusimamia ukweli, haki na ustawi wa Jamii.

Mheshimiwa Spika,
natambua kwa shukrani mchango wa viongozi wenzangu wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) makao makuu, Mkoa wa Kinondoni Kanda
Maalum Dar e salaam, Jimbo la Ubungo na wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni katika wajibu wa kuwatumikia Watanzania na kuhamasisha
mabadiliko katika taifa letu. Hali tete na tata ya sasa inatutaka tuwe
na mshikamano zaidi mpaka kieleweke. 58

Mheshimiwa Spika;
nawashukuru baadhi ya viongozi katika mamlaka mliotambua kwamba "siasa
siyo uadui" na kunipa ushirikiano kwenye serikali kuu, Wizara ya
Nishati na Madini, Manispaa ya Kinondoni, katika kamati ya nishati na
madini na wabunge wengine kwa ujumla katika kutekeleza majukumu ya
kibunge kwa manufaa ya taifa letu na watu wote.

Mheshimiwa Spika
, baada ya kusema hayo naomba bunge lako lijadili mapitio ya
utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya
matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013
kwa kuzingatia maoni tuliyoyatoa ya kuongeza bajeti ya wizara husika;
kupokea mapendekezo ya kuzingatiwa katika muswada wa sheria ya fedha
wa mwaka 2012 na kupitisha maazimio mahususi ya kuhakikisha sekta za
nishati na madini zinachangia kikamilifu katika kuinua uchumi wa nchi
na kuboresha maisha ya wananchi;

Mheshimiwa Spika; kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha

John Mnyika (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Wizara ya Nishati na Madini
27/07/2012