|
KAMATI KUU CCM YABARIKI JK KUWAWAJIBISHA MAWAZIRI
Boniface Meena na Aidan Mhando HATIMAYE
Rais Jakaya Kikwete amesikiliza kilio cha wabunge, vyama vya siasa,
wananchi wa kawaida na wanaharakati kutaka mawaziri waliohusishwa na
kashfa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) wajiuzulu baada ya kukubali kulisuka upya baraza lake.Taarifa ya
Rais Kikwete kutaka kulisuka upya Baraza la Mawaziri ilitangazwa jana na
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipokutana na
waandishi wa habari, Dar es Salaam muda mfupi baada ya kumalizika kwa
kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya CCM.
Mawaziri ambao wizara
zao zilibainika kuwa na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma katika
ripoti hiyo ya CAG na hivyo kushinikizwa kujiuzulu ni Waziri wa Nishati
na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu; Waziri wa
Fedha; Mustafa Mkulo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi,
George Mkuchika.
Wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii,
Ezekiel Maige na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na
Waziri wa Viwanda na Biashara; Dk Cyril Chami.
Nape alisema
Kamati Kuu iliyokutana jana ilipokea taarifa mbili ikiwemo uamuzi huo wa
Rais kulisuka upya baraza la mawaziri kutokana na ripoti ya CAG.
“Kamati
Kuu imepokea taarifa kubwa mbili, taarifa ya Kamati ya Uongozi ya
Wabunge wa CCM na Kamati ya Wabunge wa CCM kwa upande mmoja na taarifa
ya Kamati ya Uongozi ya Wawakilishi wa CCM kwa Bara na Zanzibar,”
alisema Nape.
Alisema pamoja na taarifa hizo, Kamati Kuu ilipokea
taarifa ya jinsi Rais alivyopanga kuchukua hatua za kuwawajibisha
mawaziri na watendaji serikalini na viongozi wa mashirika ya umma
waliobainika kuhusika na ubadhirifu ulioainishwa na CAG, kamati za
kudumu za Bunge na wabunge.
“Kamati Kuu inatambua na kuheshimu
haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa Serikali yao. Inapongeza
juhudi za Serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya CAG inajadiliwa kwa uwazi
na hivyo kuibua upungufu uliojadiliwa,” alisema Nape.
Alisema
kutokana na hilo, Kamati Kuu imeridhika na imebariki uamuzi wa Rais
kulisuka upya baraza la mawaziri na taasisi nyingine zilizoainishwa
katika ripoti hiyo ya CAG.
“Kamati Kuu imesisitiza utekelezaji wa
uamuzi huo wa Rais ufanywe mapema iwezekanavyo," alisema na kuongeza
kwamba Rais anaweza kuwabadilisha mawaziri na kuwawajibisha wale ambao
kutokana na uzito wa tuhuma zilizopo kwenye ripoti ya CAG, wanapaswa
kuwajibishwa.
"Taarifa ya CAG ndiyo ambayo ukiipitia inaonyesha nani atawajibishwa kutokana na uzito wa tuhuma,” alisema Nape.
Alipoulizwa lini Rais amepanga kulisuka baraza hilo la mawaziri, Nape alijibu: “Wakati wowote na haraka iwezekanavyo.”
Alisema
kabla ya Rais kutoa uamuzi huo, alikutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
juzi ambaye alimpa ripoti nzima ya mambo yaliyojiri bungeni.
Alisema
CCM hakijatikiswa na sakata la mawaziri hao na kwamba suala lililopo
mbele yao ni kuwawajibisha... “Tunajivunia tumelifikisha suala hili hapa
kutokana na mfumo."
Katika Mkutano wa Saba wa Bunge la 10
mawaziri hao walishinikizwa wajiuzulu kiasi cha wabunge kumkalia kooni
Waziri Mkuu, Pinda baada ya ripoti hiyo ya CAG kubainisha ubadhirifu wa
fedha za umma kama ilivyowasilishwa bungeni na wenyeviti wa kamati za
tatu za Bunge.
Taarifa za ndani ambazo zilipatikana baada ya
kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika Dodoma zilieleza kuwa wabunge wa
chama hicho waliagiza mawaziri hao wajiuzulu kutokana na kushindwa
kufanya kazi zao kikamilifu.
Baada ya kikao hicho Katibu wa
Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama aliwaambia waandishi wa habari kuwa
wamekubaliana kwamba uamuzi uliofikiwa katika kikao cha wabunge wa CCM
ungetolewa baadaye na Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda.
Vyanzo vya ndani ya kikao hicho vilimnukuu Pinda
akiwataarifu wabunge kwamba mawaziri wanane walitakiwa kuandika barua za
kuachia nafasi zao.
Chami ajikosha
Wakati akiwa amekalia
kuti kavu, Dk Chami amesema amemwandikia barua Rais Kikwete akitaka
amwajibishe Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),
Charles Ekelege. Hatua hiyo ya Dk Chami imekuja baada ya wabunge
kuchachamaa bungeni wakitaka Waziri Chami ajiuzulu kwa kile kinachodaiwa
kumkingia kifua mkurugenzi huyo.
Licha ya shinikizo hilo, Waziri
Chami alikuwa akijitetea kuwa asingeweza kumchukulia hatua mkurugenzi
huyo bila kuwa na tuhuma ambazo zingempa nguvu ya kumshauri Rais.
Dk
Chami alikuwa akisema kuwa hadi bunge linamalizika mjini Dodoma wiki
hii alikuwa hajaiona ripoti ya Kamati Ndogo ya Bunge iliyomchunguza
Ekelege ambayo ingemsaidia kupata tuhuma zinazomkabili.
“Hata
ripoti maalumu ya ukaguzi iliyofanywa na CAG mpaka wabunge wanapaza
sauti pale bungeni sikuwa nimeiona na Ekelege ni mteule wa Rais
nitamwambia Rais amefanya nini?”
Mkurugenzi huyo mkuu anatuhumiwa
kuisababishia Serikali hasara ya Sh18 bilioni kutokana na utendaji
mbovu katika kusimamia ukaguzi wa magari yanayoingia nchini uliokuwa
ukifanywa na mawakala nje ya nchi.
Dk Chami alithibitisha jana
kuwa baada ya kupokea taarifa ya CAG Aprili 18, mwaka huu siku
iliyofuata alimwandikia barua Rais akimuomba amsimamishwe kazi Ekelege.
Alisema
amemuomba Rais afanye mambo mawili, kumpa likizo ya malipo ili kupisha
uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili na pia airuhusu Bodi ya Wakurugenzi
kuteua kaimu katibu wake.
LHRC nao washinikiza
Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jana asubuhi kiliitisha mkutano na
waandishi wa habari na kumtaka Rais Kikwete awawajibishe mawaziri wote
na watendaji wa Serikali wanaohusika katika tuhuma za ubadhirifu wa
fedha za umma.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen
Kijo-Bisimba alisema baada ya uchunguzi wa CAG kubaini kuwepo kwa
matumizi mabaya ya fedha za umma, ni wakati wa Rais Kikwete kufanya
uamuzi wa haraka ya kuwawajibisha wote waliohusika.
“Kwa sasa
tunaona wazi kwamba deni la taifa limeongezeka kutoka Sh10.5 trilioni
mwaka 2010/2011 na mpaka kufikia mwaka deni hilo limeongezeka mpaka
Sh14.4 trilioni na kwamba bado kuna misamaha ya kodi kiasi cha Sh1.02
trilioni jambo ambalo ni la hatari kwa uchumi wa taifa,” alisema Bisimba
na kuongeza:
“Kama fedha hizi zingepata usimamizi mzuri,
zingeweza kujenga kilometa 1,000 za barabara bila kuomba misaada kutoka
kwa wafadhili. Jambo jingine la kushangaza ni kuwepo kwa mishahara hewa
iliyolipwa kwa walimu wa vyuo vikuu 17 ambapo Serikali imepoteza Sh1.9
bilioni ambazo zingeweza kutumika kuwakopesha wanafunzi zaidi ya 1,000.”
“Tunamuomba
Rais Kikwete alitilie uzito suala hili kwani kuna mambo mengi
yamejitokeza wazi na kuonyesha kwamba mawaziri wake siyo watendaji
makini kwani imefikia wakati wao kwa wao wanatofautiana katika uamuzi
jambo ambalo sisi kama Watanzania linatushangaza.”
“Tumeshangazwa
sana kuona utovu uliokithiri wa nidhamu na kukosekana kwa uwajibikaji
unaofanywa na mawaziri kwani wamekuwa wakitofautiana wao kwa wao jambo
ambalo hata viongozi wa juu kama Waziri Mkuu wamelinyamazia bila
kuchukua hatua zozote hali ambayo inazidi kutuchanganya.”
Bisimba
alizipongeza Kamati za Bunge kwa kile alichoeleza kuwa zimefanya kazi
yake vizuri na kusaidia kufichua baadhi ya mambo ambayo yalikuwa
yamejificha.
“Tukiwa watetezi wa haki za binadamu tunajiuliza
kwamba mawaziri hawa walikuwa wapi kipindi chote hicho mpaka wabunge
wasimame ndipo wawajibike?” alisema.
Aliwataka wabunge
kutanguliza mbele maslahi ya wananchi waliowaweka madarakani na badala
ya kujali maslahi ya vyama vyao au ya mtu binafsi.
Kamati Kuu Chadema
Kwa
upande wake, Kamati Kuu ya Chadema nayo ilikutana Mbezi Beach, Dar es
Salaam jana ambako pamoja na mambo mengine, ilijadili namna
itakavyoendesha maandamano nchi nzima kumshinikiza Rais Kikwete
awawajibishe mawaziri hao.
Baadhi ya vyama vya siasa na taasisi
nyingine zimeshaweka bayana msimamo wake wa kuungana na Chadema katika
maandamano hayo. Hizo ni pamoja na Chama Cha Wananchi (CUF), Shirikisho
la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na baadhi ya viongozi wa dini,
wasomi na wanaharakati. |